Bomu mkononi - Sehemu ya 18
ILIISHIA HAPA...
“Tuna utaratibu wa kubadilishwa mara kwa mara lakini itakapokuwa hivyo nitakujulisha,” mlinzi huyo akaniambia.
“Hakuna tatizo,” nikamjibu.
Kutoka siku ile nyumba yetu ikawa na mlinzi. Alikuwa anakuja saa kumi na mbnili jioni na kuondoka saa moja asubuhi. Anapokuja ananijulisha na anapoondoka asubuhi pia ananipa taarifa. TWENDE PAMOJA...
BAADA ya mlinzi huyo kuanza kazi, siku mbili zilizofuata Musa akaondoka tena kwenda Burundi.
Wakati wote Musa alipokuwepo nilikuwa nikimpigia simu Mustafa kisiri siri na kumdanganya kwamba nilikuwa nimekwenda kwenye msiba wa rafiki yangu uliotokea ghafla huko Kisarawe.
Siku ile ambayo Musa aliondoka nikampigia na kumwambia kuwa nimesharudi.
“Mmemaliza msiba?” Musa akaniuliza.
“Tumemaliza leo.”
“Unadhani lini tutakwenda Bagamoyo?”
“Twende kesho.”
“Nilishamfahamisha mama yangu kuhusu uchumba wetu amependa nikupeleke akakuone.”
“Sawa.”
“Kwa hiyo kesho nitakufuata asubuhi twende.”
“Nifuate saa tatu mahali petu pale pale.”
“Poa.”
Nikakata simu. Siku iliyofuata niliamka mapema nikijua kuwa nina safari ya Bagamoyo. Nilifanya usafi wa nyumbani kwangu nikapika chai. Nilipoitia chai kwenye chupa nikaenda kuoga. Nilipotoka kuoga tu nikanywa chai kisha nikaenda kuvaa.
Kwa vile nilikuwa napelekwa ukweni, nilivaa nguo za heshima. Nilivaa dera la bei ghali ambalo alininunulia Musa.
Saa mbili na nusu nikatoka nyumbani. Nilifunga mlango nikaondoka. Nilikwenda katika ule mtaaa ambao mara nyingi Mustafa huniacha hapo anaponirudisha na gari.
Nilipofika hapo zilikuwa zimebaki dakika chache kuwa saa tatu kamili. Nikasimama kando ya barabara kuisubiri gari ya Mustafa. Zile dakika nilizosimama nilikuwa nikikodolewa macho na kila mpita njia.
Ili kujipa shughuli, nilitoa simu yangu nikampigia Mustafa. Simu ilichelewa sana kupokewa mpaka nikapata wasiwasi. Nikiwa nimekata tamaa ya kupokewa simu ndipo Mustafa alipopokea simu.
“Mbona hupokei simu?” Nikamuuliza bila hata salamu.
“Unajua ninaendesha na nilikuwa sehemu mbaya, sikuweza kupokea.”
“Unakwenda wapi?” Nikamuuliza tena huku sauti yangu ikiunguruma.
“Ninakufuata wewe.”
Nikanyamaza. Mustafa alipoona nipo kimya akakata yeye simu.
Baada ya sekunde chache tu nikaliona gari lake linakuja. Lilisogea hadi kando ya miguu yangu likasimama.
Nilifungua mlango wa upande wa pili wa dereva nikajipakia na kukaa kando ya Mustafa.
“Umekuja muda mrefu?” Mustafa akaniuliza baada ya kuona nimekunja uso.
“Nimekuja muda mrefu ndio, halafu hupokei simu.”
“Kwani tulipatana tukutane saa ngapi?”
Sikujibu swali hilo kwani niliyetoa muda wa kukutana nilikuwa mimi na muda aliofika ulikuwa ndio huo huo.
“Kama uliwahi kuja ni wewe mwenyewe. Tulikubaliana nikufuate saa tatu na sasa ni saa tatu na dakika mbili.”
Wakati Mustafa akisema nilitoa kioo kutoka kwenye mkoba wangu nikakiweka mbele ya macho yangu na kuuweka sawa uso wangu. Nilifanya vile kusudi ili kujipurukusha.
Nilipoona Mustafa amenyamaza nilikirudisha kile kioo kwenye mkoba.
“Si hatutalala?” Nikamuuliza.
“Sina mpango wa kulala kule. Tukimaliza mazungumzo na mama tunarudi.”
Mvua ilitunyeshea njiani. Ilianza kidogo dogo, mwisho ikawa mvua kubwa.
Wakati tunaendelea na safari mvua ikaacha. Mji huo wa Bagamoyo nilikuwa siufahamu. Niliujua siku ile nilipokwenda na Mustafa. Ulikuwa mji wa kiasili ambao tuliusoma shuleni katika masomo ya historia. Siku ile nilivutika sana kuuona.
Nilishuhudia hoteli kubwa kubwa na maeneo mengine ya kiasili yaliyowekwa kwa ajili ya watalii.
Mustafa aliniambia kulikuwa na hoteli za bei ghali kuliko zilizoko Dar es Salaam.
“Wanapangisha wazungu tu na vigogo.”
“Siku moja na sisi tuje tupangishe chumba tulale huku.”
“Ngoja nitatafuta siku tutakuja.”
Licha ya Mustafa kumiliki gari la kifahari, nyumba yao ilikuwa ya kawaida, sawa tu na ile aliyokuwa akikaa shangazi yangu.
Baada ya kulisimamisha gari, tuliingia ndani. Nilimuona mama yake. Alikuwa amekaa sebuleni. Alikuwa mwanamke mnene na mfupi. Nilimkadiria umri wake kuwa ulishafikia miaka themanini.
Alikuwa amevaa dera na alikuwa amejitanda khanga kichwani.
Baada ya kumuamkia. Mustafa alimwambia hapo hapo.
“Mama nimekuletea mkwe wako umuone.”
“Ndiye huyu uliyekuja naye?” Mama huyo aliuliza kisha akaongeza.
“Macho yangu siku hizi hayaoni vizuri kwa uzee. Karibu mwanangu.”
“Asante mama, unajisikiaje hali yako?’ Nikamuuliza.
“Sijambo kidogo. Miili ya kizee haiachi kuumwaumwa lakini sijambo. Nashukuru.”
Mustafa akanitazama mimi.
“Mishi umemuona mama yangu?” Akaniuliza.
Kabla sijajibu, sauti ya mama mkwe ikanikatiza.
“Mbona hamkai. Mustafa mkaribishe mwenzako.”
Tukakaa kwenye kochi moja. Fanicha zilizokuwa hapo sebuleni zilihitaji sana kufanyiwa ukarabati. Nilimshangaa sana Mustafa kumiliki gari zuri na kupanga katika nyumba nzuri lakini ameshindwa hata kumnunulia mama yake fanicha mpya. Wanaume wengine wa ajabu sana.
“Sasa mmepanga kuoana lini?” Mama mkwe akaniuliza.
“Hatujapanga siku, nimemleta kwanza muonane mjuane.” Mustafa akamjibu.
“Tumeshaonana tumeshafahamiana na tutafahamiana zaidi, sasa swali linakuja mtaoana lini?”
Mama alikuwa mswahili kweli.
“Ndio tuko kwenye mipango.” Mustafa akamjibu.
“Sikiliza Mustafa, wewe ni mwanangu na mimi ni mama yako. Kama umeshapata mchumba ambaye umempenda na yeye amekupenda, nataka muharakishe kuoana. Msiendelee kuishi hivyo hivyo ni haramu.”
“Mpaka nimemleta hapa ujue kuwa mambo yamekaribia. Usifikiri kwamba tunaishi hivi hivi, tumepanga kuoana na tutaoana.”
“In shaaAllah. Na wewe sema In shaa Allah.” Mama mkwe akamwambia mwanawe huku akimpa darasa muhimu la maisha: “Kila jambo jema linaongozwa na Mungu, lazima useme In shaa Allah. Usiseme tu utafanya jambo fulani, bali uongeze neno In shaa Allah yaani ‘Mungu akipenda’, kwa sababu hujui kama utafika huo muda wa kufanya hilo jambo ukiwa hai na salama. Kwani wewe ukipanga na Mungu anapanga yake.”
“In shaa Allah.” Mustafa akamfuatisha mama yake aliyeonekana kuwa mtu wa dini sana.
“In shaa Allah,” na mimi nikatia mkazo.
“Japokuwa nimekuwa mzee lakini nitafurahi sana kama mtaharakisha kuoana na nawaombea Mungu awe nanyi katika mipango yenu.”
”Tunashukuru mama, asante,” nikamwambia.
Mustafa mwenyewe alikuwa akitabasamu tu. Baada ya mazungumzo marefu na mama mkwe tulimuaga.
“Mimi nilijua mtalala hapa.” Mama mkwe akauliza.
“Tutalalaje hapa mama, si unajua kazi zetu.” Mustafa akamwambia.
“Kazi zenu zina nini?”
“Yaani tukilala huku kazi zetu zitaharibika.”
“Wewe kila siku ni kazi tu, huna siku unayosema nikalale kwa mama. Kazi mpaka lini mwanangu?”
“Nitatafuta siku mama, nitakuja kulala. Usijali.”
Tukaondoka kurudi Dar. Mustafa alikuwa amefurahi kwa sababu mama yake alikuwa amempa baraka zote za ndoa yetu.
“Sitamuarifu tena, siku tukienda tena ninamwambia tumeshafunga ndoa.” Mustafa akaniambia.
“Kwa hiyo tutaoana peke yetu?”
“Watakuwepo ndugu na jamaa.”
“Lakini usisahau nilivyokwambia.”
“Vipi?”
“Tuoane hivyo hivyo kimya kimya, sherehe tutafanya baadaye.”
“Kwanini hupendi tuchanganye na sherehe pamoja?’
“Tutachelewa kuoana, mambo yatakuwa mengi. Tuoane kwanza halafu ndio tupange sherehe.”
“Sawa.”
Ingawa Mustafa alinikubalia, hakuelewa maana yangu hasa ya kutaka tufanye sherehe hizo baadaye na pia kutaka ndoa yetu ifanyike kimya kimya.
Tayari nilikuwa mke wa mtu na sikuwa nimeachika hivyo sikutaka ijulikane kuwa ninaolewa tena, ndo sababu nikataka ndoa hiyo ifanyike kimya kimya.
Na pia akili yangu ya kutaka sherehe ifanyike baadaye ni kuwa atakaponioa suala la sherehe nitalipotezea mbali. Hatutaifanya tena kwani sherehe itahusisha watu wengi, huenda wakawepo wanaonifahamu.
Kutoka siku ile niakawa namuhimiza Mustafa kuhusu suala la ndoa kwa vile Musa alikuwa bado yuko Burundi.
“Unasikia Mustafa, tuharakishe kufunga ndoa kwanza, ndoa haina gharama ni kupanga siku tu. Baada ya hapo ndio tutapanga mambo mengine,” nilikuwa nikimwambia Mustafa.
Siku moja Mustafa akanipa nusu ya mahari yangu shilingi milioni moja na nusu akaniambia kesho yake ndio tutaoana. Nilikwenda kuziweka benki zile pesa.
Kwa vile nyumbani kwangu kulikuwa na mlinzi, katika kipindi hicho nilikuwa nalala kwa Mustafa. Mlinzi nilikuwa nampa posho ndogo ndogo ili anitunzie siri.
Kwa hiyo ilikuwa rahisi kukamilisha mipango ya ndoa yetu. Ile siku ambayo Mustafa alipanga kunioa nilikwenda saluni asubuhi kutengezwa nywele na kupambwa kisha nikarudi.
Niliporudi Mustafa akaja na sheikh pamoja na mashahidi wawili.
Wakaniuliza jina langu. Nilipowaambia wakaniuliza walipo wazazi wangu.