Mbappe yamemkuta ya Aziz Ki
Muktasari:
- Baada ya mwendo wa kiwango kibovu msimu huu na hivyo kuachwa nje ya kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa, Mbappe angetamani kuwa na mapumziko tulivu ya kipindi hiki cha kupisha ratiba ya FIFA ya mechi za timu za taifa ili aweke nguvu katika kujipanga kurejea katika makali yake.
KYLIAN Mbappe huenda akawekwa kiti moto na klabu yake ya Real Madrid baada ya paipu ya shisha kuonekana nyuma ya picha yake ambayo straika huyo ameiposti kwenye ukurasa wake wa Instagram, siku chache tu baada ya kuzagaa kwa video za staa wa Yanga, Stephane Aziz Ki akivuta kitu kama shisha.
Baada ya mwendo wa kiwango kibovu msimu huu na hivyo kuachwa nje ya kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa, Mbappe angetamani kuwa na mapumziko tulivu ya kipindi hiki cha kupisha ratiba ya FIFA ya mechi za timu za taifa ili aweke nguvu katika kujipanga kurejea katika makali yake.
Hata hivyo, tayari amenaswa kwenye ishu tata baada ya mashabiki kubaini kuna paipu ya shisha katika picha ambazo staa huyo mwenye umri wa miaka 25 ameziposti kwenye mtandao wa kijamii.
Mbappe aliposti picha kadhaa za tukio lake la hivi karibuni la kutembelewa nyumbani kwake na staa mwenzake wa zamani wa klabu ya Paris Saint-Germain, Achraf Hakimi na Arnau Tenas. washkaji hao wameonekana katika picha hizo wakicheza video games, huku Mbappe akiandika maelezo ya picha hizo: "Padel & Marafiki…. Mchanganyiko sahihi kabisa."
Hata hivyo, moja ya picha imezua mijadala ya mashabiki baada ya kuonekana paipu ya shisha kwa nyuma. Shabiki mwenye hasira aliandika katika ukurasa wa X: "Ukweli kwamba Mbappe anatumia muda wake wote wa mapumziko kuvuta shisha, hili ndilo jambo ambalo nilikuwa silifahamu. Huyu jamaa anatucheka Madrid wote."
Licha ya kwamba hakuna kinachothibitisha kwamba Mbappe ndiye anayeimiliki paipu hiyo ya shisha, straika huyo anajiweka matatani kuwatibua Real Madrid, hasa baada ya kuendeleza ukame wake wa mabao katika mechi ambayo wameshinda 4-0 dhidi ya Osasuna.
Mbappe amejikuta akikosolewa vikali katika siku za hivi karibuni, na picha hizo zinachochea moto wa jambo hilo. Itakuwa busara kwake kukaa mbali na mitandao ya kijamii kabla hajarejea uwanjani kuipambania Real Madrid dhidi ya Leganes Novemba 24.
Jambo kama hilo limemkuta pia mshindi wa tuzo ya Kiatu cha Dhahabu ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Aziz Ki, ambaye video zake zimezagaa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonyesha akivuta kitu kama shisha akiwa katika eneo la furaha na watu mbalimbali.
Kama ilivyotokea kwa Mbappe kuachwa nje ya kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa, Aziz Ki ambaye pia amekuwa akikosolewa sana kutokana na kuwa katika kiwango kisichoridhisha, ameachwa nje ya kikosi cha timu ya taifa ya Burkina Faso, jambo hilo likiwa ni adimu sana kwa nyota hao kuachwa nje ya timu zao za taifa.