KUTOKUWA na wachezaji wake nyota, ilikuwa sababu ya Yanga kushindwa kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns uliopigwa jana usiku.
Yanga ikicheza kwa mbinu za hali ya juu ilitoka suluhu na Mamelodi kwenye mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Mkapa, siku moja baada ya Simba kulala kwa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly kwenye hatua hiyo. Marudio ya mechi zote ni wikiendi ijayo.
Kipindi cha kwanza mchezo huo ulianza taratibu, huku Mamelodi ikionekana kucheza kwa kujilinda zaidi sawa na ilivyofanya Yanga.
Siku moja kabla ya mchezo huu kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema ana wachezaji ambao wanasumbuliwa na majeraha na hawezi kuwatumia kwenye mchezo huu.
Kikosi cha Yanga cha jana kilianza bila mastaa watatu wakubwa Pacome Zouazoa, Khalid Aucho na Yao Kouassi ambao wamekuwa wachezaji tegemeo kwenye timu hiyo katika michezo ya kimataifa na ni miongoni mwa sababu iliyochangia kutopata ushindi.