LICHA ya Yanga kupoteza kwenye mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mabao 3-0 dhidi ya CR Belouizdad, Miguel Gamondi na vijana wake wameonyesha wana kitu baada ya kutawala sehemu kubwa ya mchezo huo huku makosa yao ya kupoteza mipira, mbinu sahihi za wenyeji za kushambulia kwa kushtukiza na maamuzi ya utata vikiwanyima Wananchi nafasi ya kuambulia hata bao la kufutia machozi kwenye Uwanja wa July 5, 1962.
Yanga ilimaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza ikiwa na asilimia 61 za umiliki wa mpira dhidi ya 39 za wenyeji, lakini haikuwaokoa kutanguliwa 2-0 hadio wakati wa mapumziko.
Wakaruhusu bao jingine la shambulizi la kushtukiza katika dakika za majeruhi na kujiweka katika wakati mgumu katika mechi yao ijayo nyumbani dhidi ya mabingwa mara 11 wa Afrika, Al Ahly kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Desemba 2.