Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hii ndio Simba tunayoitaka sasa

Muktasari:

  • Mashujaa wa pambano hilo lililokuwa tamu na la kusisimua walikuwa ni Kibu Denis, Lionel Ateba na Edwin Balua waliotupia mabao hayo yaliyoiangamiza Al Ahli Tripoli mbele ya kocha wa timu ya taifa ya Libya, Milutin Sredojevic ‘Micho’ anayedaiwa kukodiwa kwa muda na timu hiyo, kama ilivyoripotiwa na Mwanaspoti, akiwa jukwaani.

HII ndio Simba tunayoitaka. Ndivyo baadhi ya kauli za mashabiki waliojazana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, wakati Simba ikiing’oa Al Ahli Tripoli ya Libya kwa mabao 3-1 na kutinga kibabe katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mashujaa wa pambano hilo lililokuwa tamu na la kusisimua walikuwa ni Kibu Denis, Lionel Ateba na Edwin Balua waliotupia mabao hayo yaliyoiangamiza Al Ahli Tripoli mbele ya kocha wa timu ya taifa ya Libya, Milutin Sredojevic ‘Micho’ anayedaiwa kukodiwa kwa muda na timu hiyo, kama ilivyoripotiwa na Mwanaspoti, akiwa jukwaani.

Kibu na Ateba walianza pamoja katika kikosi cha kwanza jana na ushirikiano wao na nyota wengine walioanzishwa waliizima kabisa Al Ahli na kuifanya Simba itinge makundi kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1, kwani mechi ya kwanza iliyopigwa jijini Tripoli wiki iliyopita ilimalizika kwa suluhu.

Simba sasa inakuwa imetinga makundi kwa mara sita ndani ya misimu saba ya michuano yote ya CAF ngazi ya klabu, lakini ikiwa ni mara ya mbili katika michuano hiyo ya Shirikisho baada ya msimu wa 2021-2022 ilipokwamia robo fainali.

Katika mchezo wa jana uliohudhuriwa na mashabiki wengi wa Msimbazi, Simba iliupiga mpira mwingi na kuonyesha wazi ilikuwa na dhamira ya kuifuata Yanga iliyotanguliza makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika juzi kwa kuing’oa CBE ya Ethiopia na kuifanya kwa misimu mitatu mfululizo Tanzania kuingiza timu mbili.


HALI ILIVYOKUWA

Simba ililazimika kutoka nyuma na kutengeneza ushindi huo baada ya Ahli kutangulia kupata bao katika dakika ya 17 mfungaji akiwa straika kutoka Angola, Cristivao Paciencia ‘Mabululu’  aliyefunga kirahisi baada ya mabeki wawili wa Simba, Che Malone Fondoh na Abdulrazack Hamza kushindwa kuokoa mpira na kumtengea njiani mfungaji.

Shambulizi hilo lilitokana na mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na nahodha wa timu hiyo, Hamdou Houni kisha beki Ahmed Eltrbi kupiga krosi safi ya kichwa iliyokwenda kuwakuta mabeki wa Simba waliojichanganya na mpira kutua kwa Mabululu.

Hata hivyo, Simba ilisawazisha bao hilo katika dakika ya 36 kwa shambulizi la adhabu kama la wageni, likiwekwa kimiani na Kibu Denis aliyepiga tik tak flani hivi, akipokea mpira wa kichwa wa Che Malone aliyepokea mpira wa adhabu ya Jean Ahoua.

Sekunde chache kabla ya mapumziko Simba iliongeza bao la pili kupitia kwa Lionel Ateba akipokea pasi mkaa ya kiungo wa Ahli, Mourad Hedhli aliyekuwa akirejesha nyuma mpira, kisha mshambuliaji huyo kwenda kufunga kirahisi na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-1.


KIBU, ATEBA, CAMARA WAMOTO

Kama kuna mchezaji wa Simba aliyeiweka Al Ahli katika wakati mgumu basi, wa kwanza ni Kibu ambaye hapana shaka mashabiki wa Simba watamsamehe kwa kosa la kutaka kuwatoroka katika dirisha la usajili lililopita.

Kibu alikuwa wa moto akiwakimbiza mabeki wa Ahli, hasa kipindi cha pili na kuipa nguvu Simba ikisaka mabao zaidi, pia Ateba alikuwa mwiba kwa Walibya akitengeneza mashambulizi makali akijaribu kupiga mashuti na hata kichwa, huku akibebwa na nguvu na akili alizonazo.

Kipa Camara wa Simba, aliibakisha timu mchezoni katika dakika ya 86 alipookoa kishujaa shuti la juu la Mabululu, ambaye alidondoshewa mpira miguuni akiwa ndani ya boksi, tukio ambalo lingebadili kabisa upepo wa mechi.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids alikianzisha kikosi kinachofanana na kile kilichocheza Libya, ukimuondoa Kibu na aliona faida ya winga huyo asiyechoka aliyewavuruga mabeki wa Al Ahli.


BAO LA ATEBA

Mwamuzi wa pembeni, Yamousa Syla kutoka Guinea, aliinua kibendera pale Joshua Mutale aliyekuwa katika eneo la kuotea alipoingilia mchezo kabla ya Ateba kufunga katika dakika ya 64 akitumia pasi safi na Ahoua. Hata hivyo, wakati hadi skrini ya Azam TV ilishaandika 3-1, Tripoli walianzisha mpira haraka kwani mwamuzi alishaamua sio bao.

Baadaye bao la kwenye skrini ya Azam likafutwa na kurudishwa kuwa ni 2-1, hadi pale mtokea benchini Edwin Balua alipofunga bao la juhudi binafsi akikimbia na mpira kutokea katika eneo la Simba wakati timu nzima ya Tripoli ikiwa imepanda mbele kutafuta bao la kusawazisha.