Prime
Simba, Yanga lolote litatokea
Muktasari:
- Wakati timu hizo zikijiwinda na michuano hiyo mikubwa Afrika, Mwanaspoti limemulika wapinzani wote waliopangwa na wawakilishi hao wa Tanzania katika michezo yao ya Ligi za ndani waliyocheza na kugundua wakipambana vizuri, timu hizo zinaweza kutoboa mbele ya wapinzani wa makundi waliyopo.
VIKOSI vya Simba na Yanga zilizotinga hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika kwa sasa viko katika mawindo kwa michezo ya awali ya hatua hiyo itakayopigwa kati ya Novemba 26-28 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini zikiwa na nafasi kubwa ya kufanya vizuri.
Wakati timu hizo zikijiwinda na michuano hiyo mikubwa Afrika, Mwanaspoti limemulika wapinzani wote waliopangwa na wawakilishi hao wa Tanzania katika michezo yao ya Ligi za ndani waliyocheza na kugundua wakipambana vizuri, timu hizo zinaweza kutoboa mbele ya wapinzani wa makundi waliyopo.
Katika Ligi ya Mabingwa, Yanga imepangwa Kundi A na Al Hilal ya Sudan, MC Alger (Algeria) na TP Mazembe ya DR Congo.
Yanga iliyocheza michezo 10, imeshinda minane na kupoteza miwili ikiwa nafasi ya pili na pointi 24, nyuma ya watani zao wa jadi Simba inayoongoza na pointi 25 na kikosi hicho cha Jangwani kimefunga jumla ya mabao 14 na kuruhusu manne.
Al Hilal ambayo itaanza kucheza na Yanga mchezo wa kwanza wa kundi hilo, inaongoza ligi ya Mauritania na inashiriki kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyopo Sudan, imecheza michezo saba na imeshinda mitano na kutoka sare miwili tu.
Katika michezo hiyo, Al Hilal imekusanya pointi zake 17 ikiwa kileleni mwa msimamo baada ya kufunga mabao 15 na kuruhusu mawili.
Wapinzani wengine ni TP Mazembe inayoshiriki Ligi ya DR Congo ‘Linafoot’, ambayo huchezwa kwa mfumo wa makundi ambapo timu hiyo iko nafasi ya nne kundi ‘A’ na pointi 10, ikicheza michezo mitano, ikishinda mitatu, sare mmoja na kupoteza mmoja.
Mazembe ambayo sio wageni wa Yanga kutokana na kukutana nao katika michuano hiyo, katika Ligi ya DR Congo imefunga mabao 10 na kuruhusu mawili hadi sasa, ikiwa nyuma kwa pointi mbili tu na vinara wa Kundi A, FC Lupopo yenye 12.
MC Alger anayoichezea aliyekuwa nyota wa Azam FC, Kipre Junior ni wapinzani wengine wa Yanga ambao katika Ligi Kuu ya Algeria ‘Ligue 1’, imecheza michezo saba, ikishinda mitatu na kutoka sare minne ikishika nafasi ya tatu na pointi 13.
Katika michezo hiyo saba, kikosi hicho kimekuwa hakina uwiano mzuri wa kufunga kwani kimefunga mabao sita na kuruhusu matatu.
Kwa upande wa Simba inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika, imepangwa kundi ‘A’ na timu za CS Sfaxien ya Tunisia, CS Constantine ya Algeria na Bravos do Maquis ya Angola iliyoitoa Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ kwenye hatua iliyopita.
Simba iliyopo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi 25, baada ya kucheza 10, imeshinda minane, sare mmoja na kupoteza mmoja, ikifunga mabao 21 na kuruhusu 3, ikiwa na wastani mzuri tofauti na wapinzani wao katika kundi lake.
Bravos ambayo itacheza na Simba Novemba 28 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, katika Ligi Kuu ya Angola imecheza michezo minane hadi sasa na imeshinda mitatu, sare minne na kupoteza mmoja, ikiwa nafasi ya tano baada ya kukusanya pointi 13.
Timu hiyo iliyofunga mabao 10 na kuruhusu saba, imezidiwa pointi tisa na vinara, Petro Atletico iliyojikusanyia pointi 22.
CS Constantine ya Algeria inayonolewa na Kocha Mkuu, Kheireddine Madoui anayetajwa kujiunga na Yanga, inaongoza ‘Ligue’ ikiwa imecheza michezo minane na kati ya hiyo imeshinda minne, sare mitatu na kupoteza mmoja ikiwa kileleni na pointi 15.
Kikosi hicho licha ya kuongoza ila kimefunga mabao 10 katika michezo hiyo minane ikiwa na maana hakina safu kali sana ya ushambuliaji, huku eneo la ulinzi likiruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba hali inayoonyesha pia sio wazuri kuzuia.
Wapinzania wengine wa Simba ni CS Sfaxien inayoshiriki Ligi Kuu ya Tunisia ‘Ligue Professionnelle 1’ ambayo imecheza michezo saba, ikishinda miwili, sare minne na kupoteza mmoja, ikishika nafasi ya nane baada ya kukusanya pointi zake 10.
Katika michezo hiyo, Sfaxien imefunga mabao sita na kuruhusu manne ikizidiwa pointi tisa na vinara, Zarzis yenye pointi 19.
Simba itaanza kuingia kambini leo kwa ajili ya maandalizi hayo ya kupambana na FC Bravos, huku kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids akisema, hawana muda wa kupoteza hivyo, baada ya mapumziko mafupi wanarejea tena ili kufanyia kazi mikakati yao.
“Baada ya mchezo wetu wa mwisho na KMC, tulitoa mapumziko mafupi kwa wachezaji wote ambao hawakupata nafasi ya kuitwa timu zao za taifa, naamini wamekuwa na kipindi kizuri cha kufurahi kwa pamoja na ndugu, jamaa na marafiki zao,” alisema.
Nyota wa Simba walioitwa timu zao za taifa ni Moussa Camara (Guinea), Steven Mukwala (Uganda), Joshua Mutale (Zambia), Valentin Nouma (Burkina Faso), Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kibu Denis na Abdulrazack Hamza waliopo Stars.