Bosi KMC ataja mambo manne yaliyomuondoa Moallin, athibitisha kutua Yanga
Muktasari:
- Ingawa Yanga bado hawajathibitisha juu ya kumchukua kocha huyo raia wa Marekani mwenye asili ya Somalia, lakini taarifa zilizopo ni kwamba anakwenda kuchukua mikoba ya kocha msaidizi, Msenegal Moussa N'Daw.
KMC wamethibitisha kwamba kocha wao mkuu, Abdihamid Moallin hatakuwa sehemu ya benchi lao la ufundi kwa michezo ijayo ya kimashindano huku wakienda mbali zaidi na kusema uelekeo wake ni kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga SC.
Ingawa Yanga bado hawajathibitisha juu ya kumchukua kocha huyo raia wa Marekani mwenye asili ya Somalia, lakini taarifa zilizopo ni kwamba anakwenda kuchukua mikoba ya kocha msaidizi, Msenegal Moussa N'Daw.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya KMC ambaye pia ni Meya wa Kinondoni, Songoro Mnyonge, kuna madai manne yamewasilishwa na Kocha Moallin juu ya uamuzi wake wa kuikacha timu hiyo.
Katika madai hayo aliyoyataja kiongozi huyo alipokuwa akizungumza jioni ya leo na Kituo cha Redio cha UFM, yanahusisha maslahi binafsi na masuala ya kiuongozi ndani ya klabu hiyo iliyoanza kucheza Ligi Kuu Bara mwaka 2018.
"Mpaka jana taarifa nilizokuwa nazo kocha alikuwa kwenye mazoezi na timu, alipokamilisha na kuagana na wachezaji ndipo akawaambia anaondoka rasmi KMC na hatorudi. Mimi taarifa nilipata usiku kutoka kwa mwenyekiti wa timu ambaye alipata mshtuko baada ya kusikia taarifa hizi kutoka kwa wachezaji, alipopigiwa simu alikuwa hapokei akaja kupatikana baadaye kabisa akathibitisha ni kweli anaondoka. Baada ya wenzangu kufuatilia wakapata taarifa anakwenda timu ya Yanga.
"Msimu huu wakati ligi inaanza tulisaini naye mkataba wa mwaka mmoja kwa hiyo angeitumikia timu msimu mzima huu wa 2024-2025. Lakini tumepata mshtuko tukiwa katika raundi ya 11 mwenzetu anaondoka bila ya kutupa notisi. Mkataba ule ulikuwa unasema wakati anataka kuondoka atupe notisi ya mwezi mmoja lakini hilo hakulifanya, ameondoka tu. Sisi limetusikitisha, limetufedhehesha.
"Lakini inaonekana kulikuwa na mpango wa muda mrefu wa yeye kwenda Yanga kwa sababu amethibitisha kwamba anaenda Yanga na taarifa mitandaoni zipo zinasema amekabidhiwa majukumu ya kocha msaidizi. Sisi kama viongozi wa timu kesho tutakutana Bodi walau kulijadili hili kuona nini cha kufanya, tunasema kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi, wapo watu wengi ambao kwa sasa wameanza kuwasiliana na sisi kuja kuchukua hiyo mikoba iliyoachwa na Moallin, ingawa hatuwezi kufanya uamuzi lazima kwanza tukae Bodi tuzungumze, baadaye tutangaze kwa umma nini hatua inayofuata.
Mambo manne yaliyomuondoa
"Nimeona kuna madai kama manne hivi ambayo Moallin ameyasema yaliyomfanya aondoke KMC. Moja ya madai anasema anaingiliwa na Bodi kwenye aina ya mchezo anaotumia, mimi ninakataa, sisi kama Bodi, kama viongozi tuna uwezo wa kumshauri pale ambapo tunaweza kuona mambo yanakwenda sivyo inavyostahili kwenda lakini hakuna mtu aliyewahi kumuingilia katika kupanga timu yake.
"Pili anasema wachezaji waliopo hajafurahishwa na namna walivyosajiliwa. Mimi nakataa. Usajili wa kwanza hakushiriki, lakini usajili wa safari hii alishiriki na wapo wachezaji ambao wameingia KMC kutokana na mapendekezo yake mwenyewe.
"La tatu anazungumza habari za kuchelewa kwa mshahara, angezungumza kwamba hajalipwa kwangu ningeona ni hoja ya msingi. Sisi KMC ni timu ya serikali na serikali inaendeshwa na mifumo inawezekana mwezi huu ulipata mshahara mwezi wa tatu mwezi ujao mifumo ikagoma ukapata mshahara tarehe 30, ndiyo umechelewa lakini umepata.
"Mwisho anasema kuhusu usafiri tulimuahidi gari jipya na tumechelewa kumpa, lakini cha msingi unao usafiri, inaonekana labda Yanga wameonyesha kwa uwezo wao wanaweza kuyafanya yote haya na ndiyo kitu ambacho kimetumika kumshawishi kwenda huko alikokwenda.
"Tumesema sawa acha aende lakini kesho na wenzangu tutakaa kuangalia kama kuna njia za kisheria za kuchukua walau tulipwe kile ambacho tunastahili kwa kuvunja mkataba bila ya kutupa notisi basi ifanye hivyo lakini pia niombe mamlaka zinazosimamia michezo idhibiti huu uhuni unaoendelea ambao pengine unafanywa na timu kwa uwezo wa kifedha na kadhalika.
"Yanga hawajatutafuta, unajua kuna mambo mengine lazima tufike mahala tuache mambo ya uhuni kwenye mambo ya msingi. Yule ni muajiriwa, ana mkataba na sisi, kama Yanga walikuwa wanamuhitaji walistahili kuongea na sisi waangalie tulimuajiri kwa misingi ipi.
"Yupo hapa nchini ana vibali vya kuishi na vya kufanya kazi hapa nchini, sisi kama KMC ndiyo tumelipa hivyo vibali vya yeye kuishi hapa nchini na kufanya kazi, sasa kumchukua kihuni katika hali ambayo wamefanya sio jambo jema, ni jambo ambalo halitengenezi mahusiano mazuri.
"Yanga ni timu kubwa, hivyo inapaswa kuheshimu timu zingine zinazoshiriki katika haya mashindano, sivyo walivyofanya, hata kama wana fedha wasitumie kufanya jambo lolote, tushirikiane na tuheshimiane," alibainisha kiongozi huyo.
Moallin anaondoka KMC akiwa amejiunga na timu hiyo msimu uliopita ambapo aliiongoza timu hiyo kumaliza ligi nafasi ya tano huku msimu huu akiiacha nafasi ya saba baada ya kucheza mechi 11 na kukusanya pointi 14.
Kwenda kwake Yanga, itamfanya Moallin kuifundisha timu ya tatu inayoshiriki Ligi Kuu Bara baada ya kuanza na Azam FC aliyojiunga nayo Julai 2021 na kuondoka Agosti 2022 kisha Julai 2023 akatua KMC ambayo ameachana nayo Novemba 2024.