Krismasi vicheko, vilio EPL
Muktasari:
- Mechi hizo nane zinaonekana kuwa ndio zitaamua timu nafasi ambazo timu itakuwa nazo kufikia Krismasi.
MANCHESTER, ENGLAND: LIGI Kuu England itarejea tena Novemba 23, ambapo kuanzia hapo hakutakuwa na mapumziko tena hadi mwakani na katika kipindi chote hadi kufikia Desemba 30, kila timu itakuwa imecheza mechi nane za ligi hii.
Mechi hizo nane zinaonekana kuwa ndio zitaamua timu nafasi ambazo timu itakuwa nazo kufikia Krismasi.
Mara nyingi rekodi zinaonyesha timu inayomaliza mwaka ikiwa kinara wa ligi huwa na nafasi kubwa ya kutwaa taji, pia zile zinazomaliza nafasi ya juu, humaliza hapo hapo.
Liverpool ambao ndio vinara wa ligi wanaonekana kuwa watakuwa na wakati mgumu baada ya ligi kurejea hadi kufikia Krismasi kutokana na ratiba yao.
Kwanza majogoo hawa wa Jiji la Liverpool watakuwa na mechi tatu kubwa za michuano yote zilizokaribiana sana ukiiondoa Southampton itakayocheza nao Novemba 24 baada ya kurejea kwenye ligi kutoka katika michuano ya timu za taifa ya kalenda ya FIFA.
Baada ya hapo itakutana na Real Madrid katika Ligi ya Mabingwa, kisha Manchester City na Newcastle United.
Ugumu wa majogoo hawa unaonekana katika mechi hizo tatu za mwanzo ambapo wastani wa kupumzika kutoka mechi moja hadi nyingine ni kati ya siku moja hadi mbili.
Liverpool ambayo inaongoza ligi ikiwa na pointi 28 baada ya kushinda mechi tisa kati ya 11 ilizocheza hadi sasa - mechi tano nyingine kati ya nane ambazo majogoo hawa wanatarajiwa kucheza, ngumu zaidi zinaonekana kuwa ni mbili ambazo ni dhidi ya Tottenham (Desemba 22) na West Ham (Desemba 29).
Kuangusha pointi katika mechi hizi ikiwemo ile ya Man City kunaweza kuishusha Liverpool katika kilele cha msimamo kwani tofauti yao na timu inayoifuatia ni alama tano huku baadhi ya timu kuanzia nafasi ya tatu hadi ya tano ikiwa ni alama nane hadi tisa, hivyo kufanya vibaya katika mechi tatu tu, kunaweza kusababisha timu zilizo chini yake kuwafikia.
Man City ambayo inashika nafasi ya pili mambo yao yanaonekana kuwa magumu msimu huu ambapo katika mechi nne za mwisho imepoteza zote.
Katika mechi nane itakazocheza kabla ya mwaka kupinduka ambazo zinaweza kuamua hatma yake katika mbio za ubingwa nne kati ya hizo zinaonekana kuwa ndio ngumu zake kwake.
Mechi ya kwanza ngumu ni dhidi ya Tottenham ambayo ndio itakuwa ya kwanza kucheza mara baada ya ligi kurejea.
Jambo baya ni kwamba Spurs ambayo mechi ya mwisho ilichapika dhidi ya Ipswich, ushindi katika mechi yao dhidi ya Man City unaweza kuwapandisha hadi ndani ya nafasi tano za juu kwa sababu utofauti wa pointi kati yao na timu zilizo nafasi hizo ni mbili hadi tatu.
Mbali ya mechi hiyo, Man City itakuwa na kazi mbele ya Liverpool kwenye mchezo ambao ni muhimu sana kwao ili kupunguza pengo la alama.
Ikiwa vijana hawa wa Guardiola watapoteza mechi hii tofauti ya alama kati yao na Liverpool itapanda hadi kufikia nane jambo litakalozidi kuweka ugumu zaidi kuwapata.
Haijaishia hapo, Man City pia itakutana na mfupa mgumu wa Aston Villa inayoonekana kuwa ya moto tangu msimu uliopita na pia watacheza dhidi ya majirani zao Manchester United.
Kwa upande wa Villa inayoshika nafasi ya tisa ikiwa na alama 18, tofauti ya alama moja tu dhidi ya Chelsea iliyopo nafasi ya tatu, mechi nne za mwisho dhidi ya Man City imepoteza mbili, sare moja na kushinda moja.
Msimu huu inaonekana kuwa na moto zaidi ukilinganisha na msimu uliopita na ilikuwa inaongoza msimamo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kupoteza mbele ya Club Brugge.
Mchezo dhidi ya majirani zao, pia unatarajiwa kuwa mgumu kwa sababu ya uwepo wa kocha mpya na namna timu hiyo ilivyobadilika katika mechi nne baada ya kuondoka kwa Erik ten Hag.
Matajiri wa darajani Chelsea katika mechi nane zijazo watakutana na wapinzani wa daraja la kati na mechi kubwa pekee itakazocheza kati ya hizo ni dhidi ya Tottenham na Aston Vila.
Vijana hawa wa Enzo Maresca pia wakichanga karata zao vizuri katika mechi zao nane zijazo wanaweza kusogea hata nafasi ya pili au kuishusha Liverpool kileleni ikiwa itakuwa na matokeo mabaya.
Katika mechi nyingine itakutana na Leicester City, Ipswich, Everton, Fulham, Brentford na Southampton.
Vijana wa Mikel Arteta ambao mambo yanaonekana kuwaendea kombo msimu huu, wao wanashika nafasi ya nne wakiwa na pointi 19.
Katika mechi nane, Arsenal itakuwa na kazi kubwa ya kufanya kwenye nne huku tatu itakazoanza nazo baada ya ligi kurejea ndio zimeonekana kuwa zinaweza kuipa changamoto zaidi.
Baada ya ligi kurejea washika mitutu hawa watakutana na Nottingham Forest ambayo imeshangaza mashabiki wengi kutokana na kiwango ilichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu ambapo mbali ya sasa kuwa inashika nafasi ya tano iliwahi kuwa katika tatu bora mara kadhaa msimu huu.
Mbali ya mchezo huo, pia itakutana na West Ham inayoonekana kuwa na matokeo mazuri zaidi inapokutana na timu kubwa licha ya kuanza vibaya msimu.
Vilevile itaumana na Man United katika mchezo ambao unasubiriwa kwa hamu kutokana na ushindani wa timu zote.
Mechi ya nne ni ile dhidi ya Brighton ambayo imeichapa Man City hivi karibuni.
Ikiwa haitachanga vizuri karata zake, Arsenal inaweza kujiondoa kabisa katika mbio za kuwania taji la EPL msimu huu kwani itakuwa na pengo kubwa la alama kati yake na vinara Liverpool ambapo kwa sasa inapishana nayo pointi tisa.
Vijana wa Ruben Amorim ambao wanashika nafasi ya 13 kwa pointi zao 15, mechi zao nane zijazo zinazoweza kuamua Krismasi wanailia wakiwa katika nafasi ya ngapi, pia zitakuwa kali sana.
Man United itacheza mechi tano ngumu dhidi ya timu zinaoonekana kufanya vizuri zaidi msimu huu.
Ukiachana na mechi ya kwanza pale ligi itakaporejea dhidi ya Ipswich Town, itakuwa na mechi dhidi ya Arsenal, Nottingham Forest, Man City, Bournemouth na Newcastle United.
Timu hizi zina pointi 15 na zaidi, hivyo zinaweza kupanda kufikia nafasi tano za juu kwa kushinda mechi moja tu.
Hata hivyo, hii itakuwa ni nafasi kwa Man United kutoka katika nafasi za chini na kupanda juu zaidi, hivyo matokeo mazuri hapa yanaweza kuwapandisha hadi ndani ya nafasi nne za juu.
Spurs ambayo ipo nafasi ya 10 ikiwa na pointi 16, katika mechi nane zijazo nne ndio zinaonekana kuwa ngumu ambapo itakutana na Man City itakayocheza nao katika mechi ya kwanza baada ya ligi kurejea, pia itakutana na Bournemouth, Chelsea na Wolves.
Kufanya vizuri katika mechi hizi kunaweza kuipandisha Spurs hadi ndani ya nafasi nne za juu kufikia Krismasi ingawa pia inaweza kuondoka katika 10 bora ikifanya vibaya.