Hatimaye Jux na Priscilla yametimia...!
Muktasari:
- Uhusiano wa Jux na Priscilla au Priscy, binti wa muigizaji wa Nollywood, Iyabo Ojo ulikuja baada ya staa huyo wa Bongo Fleva kuachana na aliyekuwa mpenzi wake, Karen Bujulu ambaye walidumu kwa takribani mwaka mmoja.
Kama ambavyo ilitegemewa Jux na Priscilla kutokea Nigeria kuna la ziada nje ya uhusiano wao, sasa ni wazi ndivyo ilivyo ikiwa ni miezi michache tangu wawili hao kuanza kuonekana hadharani pamoja na kuteka mazungumzo mtandaoni.
Uhusiano wa Jux na Priscilla au Priscy, binti wa muigizaji wa Nollywood, Iyabo Ojo ulikuja baada ya staa huyo wa Bongo Fleva kuachana na aliyekuwa mpenzi wake, Karen Bujulu ambaye walidumu kwa takribani mwaka mmoja.
Huu ni uhusiano mwingine wa Jux, mwanachama wa zamani wa kundi la Wakacha ambao ameuweka sana mtandaoni kwa picha na video kali, awali alifanya hivyo alipokuwa na Jackie Cliff, Vanessa Mdee, Nayika Thongom na Karen.
Ikumbukwe hadi sasa Vanessa ndiye mrembo pekee aliyedumu na Jux kwa muda mrefu zaidi, walikuwa pamoja tangu mwaka 2014 hadi 2019 walipoachana wakiwa amefanya mengi pamoja kama kuandaa tamasha lao, Inlove & Money Tour 2018.
Kitendo cha Jux kuwa na Priscilla kutoka Nigeria kilibeba maana nyingi kwa mashabiki, wapo wanaodhani alifanya hivyo ili kumrusha roho Vanessa ambaye amechumbiwa na Rotimi mwenye asili ya Nigeria pia, hivyo amelipiza kisasi.
Wapo pia walioona kabisa kuna mradi mkubwa unakuja nje ya mapenzi yao, na ni kweli, hiyo ni baada ya Priscilla kuonekana katika video ya wimbo wa Jux, Ololufe Mi (2024) akimshirikisha Diamond Platnumz ambayo imetoka hivi karibuni.
Hili lilitabirika kutokana na utamaduni wa Jux wa kuwatumia warembo anaokuwa nao katika video zake, kipindi yupo na Vanessa alimtumia katika video ya wimbo wake, Sisikii (2015), huku wakitoa pamoja nyimbo mbili na video zake, Juu (2016) na Sumaku (2019).
Baada ya kuachana na Vanessa, Jux alizama kwenye penzi jipya na Nayika kutokea Bangkok, Thailand ambaye alitokea kwenye video ya wimbo wake, Unaniweza (2020) ingawa muda mfupi baada ya video hiyo kutoka waliachana!.
Hata kipindi anahusishwa kuwa na uhusiano na Huddah Monroe wa Kenya, madai ambayo wote waliyakanusha, ndiyo wakati Huddah alionekana katika video ya wimbo wa Jux, Simuachi (2022). Hivyo hili la Priscilla lilikuwa ni suala la muda tu.
Katika video hiyo 'Ololufe Mi' chini ya Director Fole X, Jux na Diamond wamecheza kama watoto wa Mfalme mwenye nguvu kubwa kiutawala, baba yao huyo amewachagulia wanawake wa kuoa lakini tayari kila mmoja ana chaguo lake.
Jux amempenda wanamke anayeitwa Priscy kutoka Nigeria ambaye alijuana naye kupitia mitandaoni na anatamani kukutana naye mjini, huku Diamond akiangukia kwa mtumishi anayefanya kazi katika Ufalme wao kitu ambacho ni kinyume na matakwa ya Baba yao.
Wakati video ikiendelea wanajadili ikiwa ni sawa kuacha urithi wa Ufalme ili kufuata kule walipopenda, Diamond anamshauri Jux kuusikiliza moyo wake ingawa yeye mwenyewe mwanzoni alipanga kuheshimu chaguo la baba yao.
Mwishowe Jux na Diamond wanafuata nyoyo zao na sio matakwa ya Baba yao, kufikia hapo Mfalme anakuwa hana jinsi zaidi ya kubariki uamuzi wa watoto wake na hivyo ndoa mbili zinafungwa kwa shangwe na vifijo.
Priscilla ambaye ni muhitimu wa Chuo Kikuu cha Babcock kilichopo Ilishanremo, jimbo la Ogun, Nigeria na mshiriki wa filamu ya Beyond Disability (2014), kwa kiasi kikubwa ameitendea haki video hiyo kutokana na uwezo wake wa kuigiza kama anavyotambulika.
Huyu amesomea na kurithi kazi hiyo kutoka kwa Mama yake mzazi, Ojo ambaye tangu mwaka 1998 yupo katika tasnia ya uigizaji akishiriki katika filamu zaidi ya 150 na kutoa zake binafsi 14.
Priscilla mwenye wafuasi zaidi ya milioni 3.1 katika mtandao wa Instagram na balozi wa chapa nyingi za urembo na mitindo, tangu akiwa mdogo aliigiza katika filamu nyingi za Nigeria na baadhi zilitayarishwa na Mama yake.
Ikumbukwe Ololufe Mi (2024) ni wimbo wa tatu kwa Jux kumshirikisha Diamond baada ya kuachia, Sugua (2019) na Enjoy (2023) ambao video yake imetazamwa (views) zaidi ya mara milioni 100 katika mtandao wa YouTube.
Enjoy ni video ya kwanza ya Jux kufikia namba hizo ila ni ya nane katika Bongofleva ikiwa imetanguliwa na Yope Remix (2019), Inama (2019), Waah! (2020), Jeje (2020 na Nana (2015) zake Diamond.
Pia kuna Kwangwaru (2018) ya Harmonize na Sukari (2021) ya Zuchu ambayo ilimfanya kuandika rekodi kama msanii wa kwanza solo Tanzania na Afrika Mashariki kupiga namba hizo ikiwa ni miaka minne tangu kutolewa na WCB Wasafi.
Ni wazi kiu ya Jux na Diamond ni kuona 'Ololufe Mi' nao unagonga namba za juu kwa haraka kama ilivyo kwa 'Enjoy' ambao ulishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana ingawa Jux alidai wimbo huo ulistahili kupata tuzo sita!.