Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rommy 3D: Kwa Shilole sikuwa kibenteni, najimudu

Muktasari:

  • Hata hivyo, haikuwacha kuongelewa mitandaoni na stori kumhusu Rommy, mpigapicha maarufu nchini ndizo zilizolifanya Mwanaspoti kumtafuta ili kujua nini kinaendelea.

UNAKUMMBUKA penzi la Shilole na Rommy 3D? Ni ndoa iliyodumu kwa miaka mitatu kabla ya kuachana na sasa kila mtu ana yake.

Hata hivyo, haikuwacha kuongelewa mitandaoni na stori kumhusu Rommy, mpigapicha maarufu nchini ndizo zilizolifanya Mwanaspoti kumtafuta ili kujua nini kinaendelea.

Dakika 5 Na... katika pitapita zake kunasa wasanii na kupiga nao stori kwa ufupi, ikiwa mitaa ya Sinza Mugabe uso kwa uso na Rommy na likataka kujua ukweli kuhusu stori za kama kweli akiwa na Shilole alikuwa akilelewa.

Pamoja na kuwa alikuwa na haraka, Rommy hakusita kujibu jambo hilo huku akitoa na onyo kwa watu wanaozusha mambo.

Kwa mwonekano wake wa sasa, unaweza ukashangaa, kwani amenenepa, hadi kuibua mjadala watu wakisema alipatwa na masahibu mengi kwenye ndoa ndiyo maana hakupata mwili.

Hata hivyo, mwenyewe anasema ndo maisha yake na hataki kuzungumza mengi kuhusu hilo. Msikie baada ya kukutana naye...


Rommy 3D: "Vipi Rhobi mbona unanishangaa sana halafu kucheka? Hii ndiyo iwe funzo na onyo kwa baadhi ya watu waliokuwa wanasema mimi nalelewa, yaani kula kulala. Hawajui kwenye ndoa kuna mambo mengi sana. Mimi sikuwahi kulelewa na mwanamke hata kama kipato changu ni kidogo. Najua unacheka umbea tu kuona nimepata huu mwili (kicheko) na sitaki kuzungumza chochote juu ya yaliyopita. Mie niko salama na naendelea vyema ana majukumu yangu kama kawaida."


Mwanaspoti: Unataka kusema hukuwahi kuwa 'kibenteni' maisha yako yote?

Rommy 3D: Unanifosi nizungumzie hili ila maisha yangu yote, hata kwenye ndoa yangu iliyopita sikuwa kibenteni kama watu wanavyodhani. Sitaki kuzungumzia ndoa yangu iliyopita lakini ngoja niwaambia leo watu japo najua kuna baadhi wanafahamu hili, mimi kabla sijamuoa Shilole na hajaolewa na wanaume wengine alishawahi kuwa mpenzi wangu akiwa hana pesa ya aina yeyote ile, nilikaa naye muda mrefu kwa gubangaizabangaiza, pesa tupate ndiyo tule na tuishi, tukaja kuachana kwa sababu zingine tu,  sasa piga hesabu miaka 12 iliyopita nikaja kurudiana naye na kufunga naye ndoa, yaani kiufupi sikufata pesa kwani mimi mwenyewe najiweza kipesa."

Mwanaspoti: Kwa hiyo kama uliweza kukaa miaka yote hiyo baada ya kuachana na mkaja kurudiana, hivyo watu wategemee kurudiana  kwenu tena?

Rommy 3D: No! hapana hapana, sitaweza fanya hivyo tena, kilichopo sasa ni kusubiria Mungu anipe mtu sahihi, sitaki tena kukurupuka.


Mwanaspoti: Inasemekana umepata mwanamke mwenye pesa sana ndio anakunenepesha hivyo.

Rommy 3D: Uongo, sio kweli ,siko kwenye mahusiano kwa sasa bado najitafuta. Kunenepa ni kuridhika tu.


Mwanaspoti: Vipi kazi yako ya kupiga picha bado unaendelea kufanya kazi na wasanii au wamepotea?

Rommy 3D: Najua unachotaka kuzungumza, ila mimi nimeanza kupiga picha muda mrefu na kufanya kazi na wasanii muda mrefu, sio hivyo, bado wapo sana na wameongezeka kutokana na ubora wa kazi yangu na sifanyi tu na wasanii hadi kampuni kubwa, sherehe kubwa nafanya nazo kazi Dar es Salaam na nje ya Dar es Salaam navuka.

Mwanaspoti: Unatoa ushauri gani kwa Vijana wenzako?

Rommy 3D: Kwa nini vijana (kicheko)? Ok, nawashauri tu watafute pesa, hakuna kitu kibaya kilichoumbwa kama umaskini, wapambane sana waondoe kitu umaskini katika maisha yao wataheshimika sana.


Mwanaspoti: Kwa huu ushauri kwani ulishawahi kunyanyasika kwenye ndoa yako kwa kukosa pesa?

Rommy 3D: Sijawahi fanyiwa ukatili wala unyanyasaji kwenye ndoa yangu, mimi hadi naingia kwenye ndoa nilishajipanga na kujiandaa kisaikolojia. Nimetoa tu ushauri kwa maono yangu na wala haunilengi mimi, kwa heri siku njema.