Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kizz Daniel ni mkali kuliko Kiss Daniel!

Muktasari:

  • Mathalani katika Bongofleva wapo waliofanya hivyo, kutoka Maromboso kwenda Mbosso, Saraphina kwenda Phina, Dogo Baraka kwenda Barakah The Prince, Lil K kwenda Young Killer, Nikki Jay kwenda Nikki Mbishi, Sarah kwenda Shaa na kadhalika.

KUNA wakati wasanii hulazimika kufanya mabadiliko madogo katika majina kwa sababu mbalimbali ila mara nyingi imeonekana wanafanya hivyo ili kupendezesha na kukuza upya chapa zao mbele ya mashabiki.

Mathalani katika Bongofleva wapo waliofanya hivyo, kutoka Maromboso kwenda Mbosso, Saraphina kwenda Phina, Dogo Baraka kwenda Barakah The Prince, Lil K kwenda Young Killer, Nikki Jay kwenda Nikki Mbishi, Sarah kwenda Shaa na kadhalika.

Kwa Afrika miongoni mwa waliofanya hivyo ni staa wa Nigeria, Kizz Daniel ambaye awali alijulikana kama Kiss Daniel ila mchakato wa kubadilisha jina lake ulimpitisha katika tanuru la moto kutokana na kughubikwa na migogoro ya kisheria.

Staa huyu wa Afrobeats aliyetamba na kibao chake, Buga (2022), kipindi akijulikana kama Kiss Daniel alisaini mkataba na lebo ya G Worldwide Entertainment ambao ndio ulipelekea hayo baada ya kuburuzwa mahakamani.

Na makala haya kwa leo yataenda kuangazia machache kuhusu Kizz Daniel, yeye ni nani?, wapi ametoka?, na mchakato mzima wa mabadiliko ya jina lake ilivyokuwa kitu kilichomfanya kuwa mkali zaidi hapo awali.

Kizz Daniel alizaliwa Mei 1, 1994 katika jimbo la Ogun nchini Nigeria na kusoma shule ya Abeokuta kisha kujiunga na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Abeokuta ambapo alihitimu 2013 akipata shahada ya uhandisi wa maji.

Akizungumza na Factory78 TV, alisema safari yake kimuziki ilianza akiwa na umri wa miaka 14 na baba yake ndiye alimpatia fedha za kurekodi wimbo wake wa kwanza kiasi cha Naira100,000 na huo ukawa mwanzo wa kuzifikia ndoto zake.

Mwaka 2013 ndipo akasainiwa na G Worldwide Entertainment na baadaye kuibuka mgogoro wa kimaslai, Kizz alidai licha ya kutoa nyimbo ambazo zilifanya vizuri kimauzo, lebo hiyo ilimpatia Naira30,000 tu kama mshahara wa kila mwezi!.

Kufikia Novemba 2017 alitangaza kuachana na G Worldwide na kuanzisha lebo yake, Fly Boy Inc lakini ndani ya muda mfupi mabosi wake hao walimfungulia kesi mahakamani kwa kukatisha mkataba kinyume cha makubaliano.

Hata hivyo, alishinda kesi hii lakini alipoteza hakimili ya jina lake la wakati huo (Kiss Daniel) maana G Worldwide Entertainment ndio walikuwa na hakimiliki ya jina hilo kwa mujibu wa mkataba waliosaini mwaka 2013.

Ndipo Mei 2018, akaweka wazi kubadilisha jina lake la kisanii kutoka Kiss Daniel kwenda Kizz Daniel, hivyo hivyo kwenye kurasa zake za mitandao na akaunti za majukwaa mbalimbali ya kidijitali aliyoweka nyimbo zake kama Spotify, Apple Music, YouTube na kadhalika. Kitendo cha kubadilisha jina kilimpa njaa ya kufanya kazi kwa bidii kwani alitoa kazi nyingi na zilizofanya vizuri kuliko zile za mwanzo, hivyo tunaweza kusema Kizz Daniel ni mkali kuliko Kiss Daniel. Kivipi?

Chini ya lebo yake ya Fly Boy Inc, Kizz Daniel akatoa albamu yake ya pili, No Bad Songz (2018) yenye nyimbo 20 na kuwashirikisha wasanii kama Nasty C, Philkeyz, Demmie Vee, Dj Xclusive, Wretch 32, Diplo, Sarkodie na Diamond Platnumz. Hiyo inatajwa kama albamu yake iliyofanya vizuri zaidi sokoni kwa kuongoza kwenye chati za iTunes nchini Marekani. Kwa jumla ametoa albamu sita za New Era (2016), No Bad Songz (2018), King of Love (2020), Barnabas (2021), Maverick (2023) na TZA (2024).

Kufika Mei 4, 2022 akatoa wimbo wake maarufu ‘Buga’ ambao ameshirikiana na Tekno kutoka Nigeria pia, aliachia video yake Juni 22, 2022 na kupata mapokezi makubwa ikifikisha ‘views’ milioni 40 YouTube ndani ya mwezi mmoja.

Buga yenye ‘views’ milioni 220 ikiwa ni video yake ya kwanza kupata namba hizo, iliikaribia redio ya video ya wimbo, Jerusalema (2019) wake Master KG wa Afrika Kusini ambayo ilifikisha milioni 50 ndani ya mwezi mmoja na hadi sasa ikiwa milioni 623.

Kufuatia mafanikio hayo, wimbo wa Buga ulikuja kushinda tuzo ya Soundcity MVP 2023 kama Wimbo Bora wa Mwaka, pia ameshinda tuzo nyingine kama The Headies na Nigeria Entertainment huku akiwania MTV Africa 2016 bila mafanikio. Na Februari 2023 Kizz Daniel alitangazwa na Audiomack kuwa miongoni mwa wasanii wanaofanya vizuri akiwa amesikilizwa (streams) zaidi ya mara milioni 990 na kupata wafuasi milioni 5.3 katika jukwaa hilo. Wengine ni Snazzy the Optimist, 1ucid na Asake.

Ikumbukwe mtandao wa Audiomack ulianzishwa 2012 kwa lengo la kuwawezesha wasanii kusambaza nyimbo, mixtapes na albamu, huku J.Cole kupitia albamu yake, Yours Truly 2 (2013) akiwa msanii wa kwanza maarufu kuweka katika jukwaa hilo.