Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HADITHI: Bomu mkononi - Sehemu ya kwanza

Muktasari:

  • Kielimu sikuwa nimesoma zaidi ya ile elimu ya kufuta ujinga, yaani kujua kusoma na kuandika. Niliishia darasa la saba tu. Na nilikomea darasa hilo kutokana na utoro wangu shuleni.

SIJUI niseme ulikuwa uhuni au ni tamaa ya maisha au ulikuwa ni ujinga, sijui.

Tukio hilo nililifanya miaka michache iliyopita wakati huo nikiwa bado msichana mwenye matumaini ya maisha.

Kielimu sikuwa nimesoma zaidi ya ile elimu ya kufuta ujinga, yaani kujua kusoma na kuandika. Niliishia darasa la saba tu. Na nilikomea darasa hilo kutokana na utoro wangu shuleni.

Sikuwahi hata kufanya mtihani wa taifa, nilikuwa siendi shule. Baba yangu na mama yangu walikuwa wameshafariki dunia. Mama alikufa nikiwa darasa la tano na baba alimfuata nikiwa darasa la saba ambalo sikulimaliza.

Nilielezwa kuwa nilikuwa na akili lakini sikuwa nikipenda masomo hata kidogo. Wanafunzi wenzangu niliokuwa nao darasa la saba waliniambia laiti ningefanya mtihani wa darasa la saba ningefaulu kwenda sekondari kutokana na akili yangu.

Licha ya kuishia darasa la saba, ujanja wangu uliniwezesha kuzungumza lugha ya kiingereza kwa ufasaha mzuri ila kwenye kuandika ndio ilikuwa balaa lakini nilikuwa ninaweza kusoma vitabu na magazeti yaliyoandikwa kwa lugha hiyo.

Watu wengi wasionijua vizuri walikuwa wakinidhania nilikuwa na elimu ya chuo, kumbe ni ya msingi.

Wakati naacha masomo nilikuwa na umri wa miaka kumi na mitatu. Nilikuwa nikiishi na shangazi yangu maeneo ya Ilala jijini Dar. Shangazi alinichukua baada ya wazazi wangu wote wawili kufariki dunia.

Jina langu ni Mishi. Baba yangu alikuwa anaitwa Ramadhani Mzaka, Mdigo wa Tanga. Mama yangu  ndio alikuwa Muarusha. Alikuwa mwanamke mweupe kama mwarabu. Mimi ndiyo nilishabihiana naye kwa sura weupe na uzuri.

Vile vishawishi vya wanaume ndivyo vilivyoniingiza katika balaa nikiwa na umri mdogo. Kulikuwa na kijana mmoja aliyekuwa akiitwa Sele, maarufu kama Sele Msela. Yeye ndiye aliyeniingiza katika mapenzi.

Nilikuwa nimesoma naye katika shule ya msingi darasa moja. Mimi nilipoacha masomo, yeye aliendelea hadi akafika kidato cha nne.

Miaka miwili baadaye alifanikiwa kupata kazi Shirika la Bandari. Nilikuwa nikikutana naye karibu kila siku kwa vile tulikuwa tunaishi mtaa mmoja.

Sele alikuwa kijana wa kwanza kunitamkia kuwa alitaka kunichumbia baada ya kuchubiana naye kwa muda mrefu. Miezi michache baadaye Sele akakamatwa na vitu vya wizi bandarini. Alikuwa na mchezo wa kukwapuakwapua vitu na kuja kuviuza mjini.

Ingawa alishinda kesi, alifukuzwa kazi na kurudi kijiweni. Kwa vile alishazoea kushika pesa, maisha yalimshinda akakimbilia Sauzi kutafuta maisha. Siku za kwanza kwanza tulikuwa tukiwasiliana kwa simu akinipa matumaini kwamba dhamira yake ya kuja kunioa ilikuwa pale pale lakini siku zilivyozidi kwenda mawasiliano yetu yakakatika. Siku zikazidi kwenda. Nikamsahau Sele kwani hatukuwa na mawasiliano tena.

Siku moja nilikuwa natoka Kigoma. Basi liliharibika njiani. Tulikaa hadi usiku, basi lilikuwa bado likishighulikiwa. Likapita lori likielekea Dar. Nilikuwa nimesimama peke yangu pembeni mwa barabara.

Dereva wa lori hilo aliponiona alifunga breki akatoa kichwa kwenye dirisha na kuniuliza.

“Unakwenda Dar?”

Nilikuwa kwenye lindi la mawazo yaliyochanganyika na uchovu. Ile sauti ya dereva ikanishitua.

“Unasemaje?” Nikamuuliza.

“Unakwenda Dar?” Akaniuliza tena.

“Ndiyo ninakwenda Dar lakini basi letu limeharibika.”

“Uko tayari kusafiri kwa lori?”

“Acha lori, hata kwa trekta niko tayari. Nimechoka sana.”

“Njoo ujipakie twende.”

Kwa vile sikuwa na mzigo wowote zaidi ya mkoba wangu ambao nilikuwa nao begani nikasogea kwenye lori hilo. Taniboi alifungua mlango akashuka na kunipisha. Nikaingia kwenye lori.

Nikawekwa katikati. Kulia kwangu kulikuwa na dereva. Kushoto kwangu kulikuwa na taniboi.

Tukaanza safari.

“Unatokea wapi?”Dereva akaniuliza.

“Natoka Kigoma,” nikamjibu na kuongeza.

“Lakini najuta kupanda lile basi, limeharibika njiani mara tatu.”

“Pole sana. Sasa wewe ni mkazi wa Kigoma au Dar?”

“Ni mkazi wa Dar. Kigoma nilienda tu mara moja.”

Wenyewe walikuwa wakitafuna mahindi ya kuchemsha waliyonunua njiani. Wakanipa moja, na mimi nikawa natafuna.

Ilipofika saa mbili usiku.Lori likasimama katika kijiji kimoja. Tukashuka kwa ajili ya kupumzika na kupata maakuli. Mimi nilikataa kula kwa sababa nilikuwa nimechoka na sikuwa nikitamani kula kutokana na ile fadhaa ya safari.

Lakini dereva wa lori hilo alinilazimisha nile.

“Tutafika alfajiri, hutapata chakula tena,” akaniambia. Nikaamua nile. Nikala kuku mzima na wali. Wakati nataka kulipa pesa dereva akaniambia nisilipe.Akalipa yeye. Nikamshukuru kwa wema wake.

Baada ya kula tulipumzika kwa muda mrefu tukizungumza kile na hiki. Tulipoanza tena safari nililala ndani ya lori. Mpaka nakuja kuzinduka tupo Chalinze.

“Tuko wapi hapa?”Nikamuuliza dereva.

“Tuko Chalinze,” dereva akanijibu.

“Kumbe nimelala sana.Ni saa ngapi sasa?”

“Inakaribia kuwa saa tisa.”

Pale Chalinze lori lilisimama tena. Tukashuka.Tuliingia kwenye mkahawa mmoja tukanywa chai. Dereva akamtuma taniboi wake akanunue mirungi.

Sisi tulibaki kwenye mkahawa hadi taniboi alipokuja na bahasha iliyofungwa mirungi. Nikamsikia dereva akimuuliza taniboi huyo.

“Umepata gati au shambarungu?”

“Nimepata gati.”

Dereva akaifungua pale pale na kuitazama.

“Hii ni giza halafu ni kilalo,” akasema baada ya kuiangalia.

“Saa hizi huwezi kupata ya leo.”

Vilikuwa vichanga sita. Dereva alichagua vichanga vitatu akachukua yeye, vitatu akampa taniboi wake.

“Umenunua bigijii,” akamuuliza.

“Ndiyo hizi hapa.”

Zilikuwa kwenye mfuko. Taniboi akatia mkono mfukoni na kutoa peremende hizo za ubani zipatazo kumi.

Dereva alichukua tano na tano nyingine akamuachia taniboi.

“Turudi kwenye gari.” Dereva akwambia taniboi wake. Dereva huyo niliyekuwa nimekaa naye akanyanyuka na kuniambia.

“Twende.”

Na mimi nikanyanyuka tukatoka na kurudi kwenye gari. Hawakuondoka hapo hapo, kwanza walianza kutafuna mirungi yao huku wakivuta sigara.

Walikuwa wamenikera sana kutokana na ule moshi wa sigara. Ni vile walinisaidia tu ndio sababu niliwavumilia.

“Kwani hii mirungi inawapa ladha gani?” Nikawauliza.

“Inatupatia zaidi ya ladha.” Dereva akanijibu.

“Nini sasa?’

“Inatupatia handas!”

“Nimekuwa nikiwasikia walaji mirungi pale Dar wakitaja hiyo handas lakini sijui maana yake.”

Nilipowambia hivyo wakanicheka.

“Sasa mnacheka nini jamani wakati mimi nauliza?’

“Handas ndio kilevi cha hii mirungi. Kwanza unajisikia raha na pili inakupa hisia fulani ya kukuburudisha.” Dereva akaniambia.

“Inawapa hisia gani?”

“Kila mtu inampa hisia ya namna yake. Kuna watu wanapata hisia za utajiri wanapokula mirungi. Wanajenga majumba na kununua magari ya kifahari mawazoni mwao.”

Nikaangua kicheko.

“Yaani wanawaza tu kuwa wananunua magari na kujenga nyumba wakati si kweli?” Nikawauliza huku nikiwatazama kwa zamu dereva na taniboi wake.

“Hebu jaribu kutafuna utaona mwenyewe na hutauliza tena.” Dereva akaniambia na kunipa majani kadhaa ya mirungi.

Nikaanza kutafuna nikiwaigiza vile wanavyokula. Nilihisi ilikuwa michungu na ilikuwa na kakasi.

Nikakunja uso.

“Kumbe ni michungu namna hii?”

“Kula na bigijii.” Dereva akaniambia.

“Nipe basi.”

Dereva akanipa bigijii moja. Nikaifungua na kuimega kidogo. Utamu wake ukapunguza ule uchungu niliokuwa nikiusikia. Nikaendelea kutafuna.

“Halafu nasikia inarusha usingizi,” nikawauliza.

“Ndio maana unaona madereva wengi wa malori wanakula.” Dereva akaniambia.

“Hata baadhi ya madereva wa daladala pia wanatafuna. Nimeshawaona.”

“Ile kazi yenyewe ni pasua kichwa, lazima wale mirungi.”

Dereva akatazama saa yake kisha akasema.

“Tuondoke.”

Akaliwasha gari na kuliingiza barabarani. Tukaanza safari ya kuelekea Dar.

Dereva huyo alikuwa akiendesha huku akiendelea kula mirungi.Wakati ule ndio nilitambua kuwa mirungi ilikuwa ikifanya kazi ndani ya kichwa chake kwani mazungumzo yake yalianza kubadilika.

“Unajua tangu tumekupakia sijakuuliza jina lako, unaitwa nani?” Akaniuliza.

“Naitwa Mariam,” nikamdanganya kisha nikamuuliza.

“Na wewe unaitwa nani?”

“Naitwa Musa. Unaishi Dar sehemu gani?”

Sikutaka kumtajia mahali ninapoishi lakini niliona kama nitamtajia anaweza kunipeleka hadi nyumbani, nikamwambia.

“Naishi Ilala.”

Musa akanitazama usoni kisha akanitazama kifuani.

“Hivi unafanya shughuli gani?’

“Biashara tu,” nikaendelea na uongo wangu. Sikuwa na biashara yoyote.

“Unafanya biashara gani?”

Nikafikiri kidogo kisha nikamwambia.

“Huwa naleta mchele kutoka Mbeya.”

“Kutoka Mbeya au Kigoma?”

“Kutoka Mbeya, Kigoma nilikwenda tu kwa matatizo yangu mengine.”

Ukapita ukimya mfupi kabla ya dereva huyo kuniuliza tena.