Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SIMULIZI YA HADITHI: Bomu Mkononi - 4

Muktasari:

  • Siku ya pili ikawadia. Nikaisubiri saa kumi kwa hamu. Mpaka ilipofika saa tisa na nusu nilikuwa nimeshajitayarisha. Nilivaa nguo yangu nzuri na kujitia manukato ya kuvutia, nikatoka.

NILIKUWA nimepanga maswali yangu ya kumuuliza nitakapokutana naye. Majibu yake ndiyo yangekuwa vigezo muhimu kwa upande wangu vya kuamua kuwa naye au kuacha kuwa naye.

Siku ya pili ikawadia. Nikaisubiri saa kumi kwa hamu. Mpaka ilipofika saa tisa na nusu nilikuwa nimeshajitayarisha. Nilivaa nguo yangu nzuri na kujitia manukato ya kuvutia, nikatoka.

Mwendo wa robo saa tu ukanifikisha kwenye kituo cha daladala. Nilitaka tukutane hapo kwa sababu sikuwa na mahali pengine ambapo ningemtajia na yeye akaweza kupaelewa kwa urahisi.

Kabla hata ya kufika saa kumi kamili Musa akashushwa na pikipiki. Nilihisi ilikuwa bodaboda kwani mara tu baada ya kuteremka alimlipa mwenye pikipiki. Alikuwa hajaniona mpaka nilipomfuata na kumgusa bega.

Musa akagutuka na kugeuka upande niliokuwa nimesimama.

“Oh Mariam. Nilikuwa nataka nikupigie simu,” akaniambia. Mkono wake tayari ulikuwa mfukoni.

Alikuwa bado akiniita Mariam baada ya kumdanganya siku ile.

“Unipigie simu ya nini?” Nikamuuliza kivivu.

“Nikwambie nimeshafika.”

“Kwani si tulipatana tukutane hapa saa kumi.”

“Kwa hiyo?”

“Ni wajibu wangu mimi nije hapa na wewe uje hapa, si suala la kupigiana simu tena.”

“Nilikuwa sijakuona.”

“Twenzetu,” nikamwambia. Ilikuwa kidogo nimshike mkono kama vile tayari tulikuwa wapenzi.

Tukafuatana kuelekea upande wa Buguruni.

“Tunakwenda wapi?’ Akaniuliza.

“Kwani wewe unataka twende wapi?” Na mimi nikamuuliza.

“Sehemu yoyote tu ya kupumzika.”

“Ndiyo tunakwenda.”

Pakapita kimya kifupi kabla ya Musa kuniuliza.

“Vipi sabufa linatoa vizuri?”

“Sana. Tangu asubuhi nilikuwa nasikiliza miziki tu.”

Tulikwenda kwenye hoteli moja, tukaingia na kukaa kwenye viti. Musa akaniuliza nilikuwa nahitaji kinywaji gani.

Sikutaka kutaja kilevi chochote, nikaagiza soda tu. Na yeye akaagiza soda.

Tukaanza mazungumzo. Mazungumzo yetu yalikwenda mpaka yakafika mahali ambapo niliweza kumuuliza Musa kama alikuwa ameshaoa.

“Nimeshaoa,” akanijibu.

Hicho kingekuwa kigezo cha kutosha cha kumkataa Musa japokuwa nilishaanza kumpenda.

Nikajidai natabasamu nilipomuuliza tena.

“Una watoto wangapi?’

“Mtoto wangu alikuwa mmoja na alishafariki. Kwa sasa sina mtoto.”

“Kwani mke wako hana ujauzito tena?”

“Tulishaachana muda mrefu.”

“Uliponiambia umeshaoa nilijua una mke.”

“Ulikosea kuniuliza. Ungeniuliza una mke ningekwambia sina lakini umeniuliza umeshaoa, ndio maana nikakujibu nimeshaoa lakini haikuwa na maana kuwa nina mke.’

“Hapo nimekuelewa. Mliachana lini na mke wako?’

“Karibu miaka mitatu sasa.”

“Kwa nini mliachana?”

“Ni kwa sababu za kibinafsi.”

“Niambie.”

“Riziki inapokwisha watu mnaachana tu.”

Nikatikisa kichwa.

“Lazima kuna sababu. Inaonekana wewe una matatizo.”

“Hapana. Yule mwenzangu ndiye aliyekuwa na matatizo. Wivu aliuzidisha kupita kiasi. Kila siku tulikuwa tunagombana kwa sababu ya wivu wake.”

“Kwa hiyo ndio ukaona umuache?”

“Sio kwamba niliona nimuache, sote wawili tulifikia uamuzi kuwa tuachane kwa sababu tusingeweza kuishi katika hali ile ya kugombana kila siku.”

“Sasa kwanini hujaoa kipindi chote hicho?”

“Bado nipo nipo kwanza.”

Aliposema hivyo tukacheka.

“Unajua Musa unaonekana una mabibi wengi, vinginevyo ungelikwishaoa. Huwezi kukaa kipindi chote hicho bila mke.”

“Unaweza kunidhania hivyo kwa vile hujui tabia yangu lakini mimi ni mtu ninayejichunga sana. Sina tabia za kipuuzi puuzi, ndio maana nimechelewa kuoa tena. Ninataka ninapooa niwe nimeoa mke sio jike.”

“Lakini msichana wa nje huwezi kukosa japokuwa mmoja.”

“Nataka uwe wewe. Wewe ndio chaguo langu.”

“Unataka kunioa au…”

“Kuoana ni matokeo tu kama tutaonyeshana tabia nzuri na mapenzi ya dhati baina yetu.”

“Unaishi wapi?’

“Mimi niko Kimara.”

“Unaishi katika nyumba yako au ya kupangisha?”

“Ni nyumba ya kupangisha.”

“Unaishi peke yako humo ndani?”

“Tuko familia mbili, mimi na mwenzangu lakini hatukutani. Kila mtu yuko upande wake.”

“Kama unaishi hivyo ni vizuri kwa sababu unaepukana na umbea.”

“Tatizo linakuwa ninaposafiri, inabidi nimlete ndugu aje alale hadi ninaporudi.”

“Kwa sababu ya kulinda nyumba, siku hizi wezi ni wengi.”

“Ndio hivyo. Je wewe mwenzangu unaishi kwenu au…?” Musa naye akaniuliza.

“Kwanza mimi wazazi wangu wote wawili walishafariki, ninaishi na shangazi yangu.”

“Uliwahi kuchumbiwa au kuolewa?’


“Masomo yenyewe nimemaliza mwaka jana tu, kidato cha nne.” Hapo nilisema uongo ili aone nimesoma na bado ni mdogo.

“Kumaliza masomo mwaka jana si hoja kwamba usipate mume akakuchumbia.”

“Labda nikwambie sijachumbiwa wala sina mume.”

“Sasa unashughulika na nini?”

“Kwa sasa nipo nyumbani tu.”

“Mbona sikuelewi, nakumbuka siku ile tulipokuwa tunatoka Kigoma uliniambia kuwa unaleta mchele kutoka Mbeya?’

Ndio maana unaambiwa njia ya muongo fupi na ukiwa muongo usisahau. Nilikuwa nimeshasahau kama nilimdanganya hivyo. Kumbe mwenzangu bado anakumbuka. Nikatunga uongo mwingine.

“Wewe umeniuliza kwa sasa ninashughulika na nini, ndio nikakujibu niko nyumbani. Hiyo biashara ya mchele ninayo, sema kwa sasa nimepumzika kidogo.”

Pakapita kimya cha sekunde kadhaa. Musa alikuwa ameukubali uongo wangu. Alikuwa akinywa soda huku akipepesa macho yake akitafuta la kuniambia.

Mimi nilikuwa nimeinamia chupa ya soda huku nikiivuta kwa mrija taratibu. Hakuwa akijua kwamba nilikuwa namtazama kwa pembeni mwa macho yangu.

“Sasa Mariam utakuja lini kunitembelea nyumbani?’ Akaniuliza ghafla baada ya kuuchomoa mrija midomoni.

“Wewe unataka nije lini?”

“Mimi nataka hata leo.”

“Kwa leo haitawezekana, tupange siku nyingine.”

“Kama lini?”

“Nitakwambia siku ya nafasi yangu, usijali.”

“Kwanini usiniambie hii leo?”

“Musa mbona una haraka hivyo?’

Musa akacheka. Nikayaona meno yake. Licha ya kula mirungi na kuvuta sigara, yalikuwa meupe na yenye mwanya wa juu. Niliyapenda.

“Unacheka nini?” Nikamuuliza kwa mzaha ingawa nilishajua kilichomchekesha.

“Nimecheka kwa hivyo ulivyoniambia kuwa nina haraka.”

“Haraka haraka haina baraka,” nikamwambia.

“Ninajua lakini ngojangoja nayo huumiza matumbo!”

Hapo na mimi nikacheka. Musa aliponiona nacheka naye akacheka.

Mpaka tunaondoka hapo hotelini sikuwa nimempa ahadi yoyote ya kwenda kwake zaidi ya kumwambia asubiri.

Nikamsubirisha sana. Zilipita wiki kadhaa. Nilikuwa nikimsumbua tu na yeye hakukata tamaa wala kuonyesha kuchukia. Katika kipindi chote hicho tulikuwa tukiwasiliana na alikuwa akinipa pesa pamoja na zawadi mpaka nikawa namtegemea yeye kipesa kwani sikuwa na mwanaume mwingine.

Napenda niseme kuwa kwa mtindo wake huo alinilegeza nikawa mdogo kama nukta na nikalegea kama mnyoo. Nilikuwa kama mbuzi niliyekwishatiwa mikononi na kusalimu amri, nilichokuwa nasubiri ni kuchinjwa tu!

Hivyo ndivyo nilivyoanza uhusiano na Musa dereva wa malori. Uhusiano wetu haukukaa sana ukawa uchumba. Siku ile ambayo Musa aliifikisha barua ya uchumba kwa shangazi yangu nilifurahi sana.

Barua yake ilipokewa na siku ya pili yake akarudishiwa majibu ya kukubaliwa kwani uhusiano wetu ulikuwa ukifahamika.

Mwezi mmoja baadaye Musa alilipa mahari yangu, sasa tukajiandaa kufunga ndoa.

Wakati ule wa maandalizi ya ndoa ndipo nilipomtonya rafiki yangu Amina. Nilimpigia simu nikamuita nyumbani. Alipokuja ndipo nikamueleza kwamba nataka kuolewa.

Amina akashituka.

“Unaolewa na nani?” Akaniuliza kwa shauku.

“Naolewa na Musa.”

“Musa huyu mwanaume wako, dereva wa malori?”

“Ndiye huyo huyo dada.”

“Mbona mmeharakisha hivyo?’

“Ah mwenyewe ndivyo alivyoaka.”

“Ni hatua nzuri. Sasa ndoa yenyewe itakuwa lini?”

“Ndio tuko kwenye maandalizi, hatujapanga siku lakini haitachukua muda mrefu.”

“Nawapa hongera kwa kufikia uamuzi huo lakini nataka uje unitambulishe kwa mchumba wako kabla hamjafunga ndoa. Unajua sijawahi kukutana naye!”

“Basi subiri Jumapili, tutakuwa hoteli fulani nitakuita.”

“Hapa hapa Ilala?”

“Ndiyo, itakuwa hapa hapa Ilala.”

“Saa ngapi?”

“Itakuwa mida mida ya usiku.”

“Poa. Nataka nimuone tufahamiane kabla ya ndoa yenu.”

“Usijali.”

Baada ya mazungumzo yetu na Amina tuliagana, Amina akaondoka.

Kwa kawaida kila siku ya Jumapili, kama Musa hakwenda safari huwa tunakutana katika hoteli moja pale Ilala. Tunakula chakula cha usiku na kuzungumza machache kisha anaenda zake.


Jumapili ilipowadia Amina akanipigia simu kunikumbusha juu ya ile ahadi yetu. Nikamwambia kuwa ninaikumbuka.


“Tutakapokuwa wote nitakupigia,” nikamwambia nilimaanisha nitakapokuwa na mchumba wangu Musa nitampigia ili aje.