Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

JICHO LA MWEWE: Miaka 26 baadae, kutoka Mmachinga hadi Aziz Ki

Muktasari:

  • Yanga wakaenda zao makundi ya Ligi ya Mabingwa wakati huo ikimaanisha walikuwa wametinga robo fainali. Miaka 26 baadae, juzi sikuvuka geti la shule. Nilivuka Bahari ya Hindi kwenda Unguja kuitazama Yanga ikiisambaratisha CBE ya Ethiopia kwa staili ile ile ya miaka 26 iliyopita. Na kwa namna hiyo wametinga hatua ya makundi.

MIAKA 26 iliyopita, mwaka 1998 nilikatiza katika geti la Magharibi la Shule ya Sekondari ya Jitegemee kwenda uwanja wa zamani wa Taifa, (sasa Uhuru maarufu Shamba la Bibi) kushuhudia Yanga wakiichapa Coffee ya Ethiopia mabao 6-1. Bonge la mechi. Kina Mohammed Hussein 'Mmachinga' katika ubora wao.

Yanga wakaenda zao makundi ya Ligi ya Mabingwa wakati huo ikimaanisha walikuwa wametinga robo fainali. Miaka 26 baadae, juzi sikuvuka geti la shule. Nilivuka Bahari ya Hindi kwenda Unguja kuitazama Yanga ikiisambaratisha CBE ya Ethiopia kwa staili ile ile ya miaka 26 iliyopita. Na kwa namna hiyo wametinga hatua ya makundi.

Kuanzia wakati ule hadi leo, hapa katikati mpira wetu ulivurugika kidogo lakini juzi Yanga walikuwa wanaonesha ni kwanini wamerudisha lile pengo ambalo lilikuwepo miaka hiyo kati ya timu za Tanzania dhidi ya zile za Ethiopia. Kila kitu kilikuwa wazi kwa kila mtu kushuhudia. Safari hii ilikuwa staili tofauti zaidi. Mabao manne yalikuwa yamefungwa na wachezaji wa kigeni, Clatous Chama, Stephane Aziz Ki na Duke Abuya.

Mabao mawili yalifungwa na vijana wa nyumbani. Mudathir Yahaya na Clement Mzize. Uwekezaji mkubwa umefanyika kurudisha pengo lilikuwepo kati ya Yanga na timu za Ethiopia. Wameonesha tofauti. Kumbuka kwamba CBE ni Mabingwa wa Ethiopia. Yanga walikuwa bora kila idara na walidhihirisha kwamba hadhi yao kwa sasa ni kufika robo fainali na kuendelea.

Niliandika mahala kwamba Kocha wa Yanga, Manuel Gamondi aache kukariri kikosi chake. Kwamba katika mechi muhimu zaidi lazima awapange Aziz Ki na Pacome Zouzoua. Kwanini Chama asiwe anaanza katika mechi muhimu? Pambano lililofanyika Addis Ababa lazima lilimtia hasira Chama. Aziz alikuwa anafanya masikhara kwa kupoteza mipira mingi uwanjani huku Chama akishuhudia katika benchi.

Labda Gamondi aliliona hili na amebadilika. Hatimaye Chama alianzishwa na Aziz akakaa benchi. Ndani ya dakika 45 za kwanza, Chama alikuwa amemuonesha Gamondi ni kitu gani alikuwa anakikosa kwa kumweka benchi katika mechi zinazohitaji maamuzi. Alimlaza kwa amani kipa wa CBE na kufunga bao zuri la kuongoza.

Ni nyakati kama hizi ambazo Simba walijua 'wangemmiss' Chama. Wakati fulani walikubali kwamba Chama alikuwa hawafai, lakini wakati dirisha likikaribia kufunguliwa ndipo wakakikumbusha mambo kama haya ambayo Chama aliyafanya. Walijua kwamba yangehamia upande mwingine.

Na kweli jana alikuwa anadhihirisha kwamba yalikuwa yamehamia upande mwingine.

Kitu kizuri kwa Aziz Ki kuwekwa benchi na Chama kuanza na kisha kufunga ni kwamba ilimtia hasira Aziz wakati alipoingia baadae. Alionekana kuipania mechi na hakupoteza mipira ovyo. Zaidi ya yote akafunga mabao mawili mazuri kama ilivyo kawaida yake. Duke Abuya pia alijifunza kwamba tofauti yake na Mudathir ni kwamba Muda huwa anasogea mbele na kufunga.

Ni kweli, ndani ya wiki mbili Abuya amefunga mabao mawili. Aliifungia Kenya katika pambano la kufuzu kwenda Afcon dhidi ya Namibia ugenini, lakini juzi alisogea mbele na kufunga. Hata hivyo, na Mudathir aliendelea kupiga simu yake kama kawaida. Naye ni kama Abuya. Aliifungia pia Taifa Stars na kupiga simu dhidi ya Guinea pale Abidjan. Mpira wa kisasa viungo na mawinga wanafunga zaidi ya washambuliaji asilia.

Kilichomtokea Aziz kwa Chama ndicho ambacho kilimtokea Prince Dube kwa Mzize. Alipoteza nafasi nyingi za kufunga katika pambano lililofanyika vilimani pale Addis Ababa na safari hii Gamondi akaamua kuanza na Mzize. Na kama ilivyokuwa kwa Chama, Mzize naye akamuonesha Gamondi kwamba asikariri kumuweka benchi katika nafasi muhimu. Akafunga katika dakika za mwanzo za kipindi cha pili.

Khalid Aucho alikuwa katika benchi akimtazama Jonas Mkude akiitendea haki nafasi yake. Hii ni faida nyingine ambayo Yanga wanayo kwa sasa. Wana wachezaji bora wengi katika nafasi nyingi tofauti na inampa kocha uwezo wa kukipangua kikosi chake kadri anavyojisikia. Angeweza kumuingiza Aucho lakini akaamua kwenda na Duke Abuya.

Yanga walikuwa bora na walidhihirisha pengo lililopo kati ya bingwa wa Tanzania dhidi ya bingwa wa Ethiopia. Kuanzia mchezaji mmoja mmoja hadi timu kwa ujumla, kila kitu kilifanywa kwa ubora mwingi. Wahabeshi walijikuta wakifukuza vivuli. Wasingeweza kupambana na ubora wa Yanga hii.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Achilia mbali ubora wa wachezaji wao lakini kuna kitu ambacho Yanga wanacho. Wapo fiti. Kama ilivyokuwa kwa mechi nyingi za msimu uliopita, Yanga walionekana bora zaidi katika kipindi cha pili na kufunga mabao mengi zaidi kwa sababu Wahabeshi walishindwa kuendana na pumzi zao katika kipindi cha pili. Stamina na pumzi za Yanga zilikwenda juu zaidi.

Unapaswa kumsifia Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said. Kila siku anapandisha ubora wa timu. Mfano, alipoamua kuachana na Joyce Lomalisa na kwenda kwa Chadrack Boka alikuwa amefanya kitu kile kile cha kuachana na Djuma Shaban na kwenda kwa Yao Kouassi. Ubora uliongezekana maradufu. Na kule kushoto ubora umeongezeka maradufu.

Boka ni kama bodaboda. Ana kasi. Ana nguvu. Ana stamina. Upande wa kushoto wa Yanga umekuwa na nguvu zaidi. Tazama namna ambavyo alipika bao la sita. Kasi yake aliyotumia ni ile ambayo utumiwa na wachezaji katika dakika za mwanzo za mchezo. Yeye alikuwa ameitumia katika dakika za mwisho za mchezo.

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Vinginevyo ulikuwa usiku mzuri kwa Yanga. Walifanya ambacho kimetarajiwa. Matokeo mengine tofauti na hiki ambacho wamefanya basi wangeshangaza watu. Niliandika mahala kwamba sasa hivi timu zetu Simba na Yanga zimeondoka katika lile kundi la vibonde baada ya kukusanya pointi nyingi kule CAF.

Na sasa hatupangwi tena na wale rafiki zetu wa Afrika Kaskazini katika hatua ya awali ya michuano hii. Unapewa timu ambayo umeizidi kiwango kama ambavyo zamani tulikuwa tunapewa Mafarao waliotuzidi kiwango. Na zaidi unaanzia ugenini kisha unamalizia nyumbani. Ndicho kilichotokea katika mechi dhidi ya Vital'O na CBE.

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Na kilichotarajiwa ndicho ambacho Yanga wamefanya. Ushindi wa mechi zote nne. Nyumbani na ugenini. Baada ya hapo Yanga wametinga makundi na wanatarajiwa kuwa miongoni mwa timu mbili ambazo zitakwenda robo. Kinyume na hapo watakuwa wamefeli katika msimu huu.

Timu kubwa huwa zinaishi hivyo. Kina Al Ahly huwa wanaishi hivyo. Wazungu wanasema 'consistency'. Mwendelezo wa ubora. Majuzi nilimsikia nahodha wao, Bakari Mwamunyeto akidai kwamba wanaitaka fainali ya Ligi ya mabingwa. Sina uhakika na ndoto zake lakini hata wakifika nusu fainali tu itakuwa kazi nzuri.