Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga inakwama wapi kwa Simba?

Yanga Pict
Yanga Pict

Muktasari:

  • Tangu mwaka 2018, Yanga Princess ilipojiunga na Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) imekuwa ikichezea vichapo kutoka kwa mnyama wa kike, kama ilivyokuwa tena juzi Jumatano zilipokutana kwenye Uwanja wa KMC Complex na ilichapwa tena bao 1-0, kwenye mchezo wao wa kwanza wa ligi msimu huu.

HII sasa imekuwa kawaida. Siyo stori tena kusikia Simba Queens imeshinda dhidi ya Yanga Princess.

Tangu mwaka 2018, Yanga Princess ilipojiunga na Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) imekuwa ikichezea vichapo kutoka kwa mnyama wa kike, kama ilivyokuwa tena juzi Jumatano zilipokutana kwenye Uwanja wa KMC Complex na ilichapwa tena bao 1-0, kwenye mchezo wao wa kwanza wa ligi msimu huu.

Bao hilo lilitokana na Yanga beki wa Yanga, Danai Bhobho kujifunga katika dakika ya 48, kutokana na presha iliyopelekwa langoni mwao na kiungo mshambuliaji wa Simba, Vivian Corazone.

Mechi ya ligi ya wanawake kuamuliwa kwa bao la kujifunga la beki wa Yanga, ilijibu dabi ya Ligi Kuu Bara ya kaka zao ambayo pia iliamuliwa kwa bao pekee la beki wa Simba, Kelvin Kijili kujifunga.

YA05
YA05

Kwa ushindi huo, Simba Queens imepanda kileleni kutoka nafasi ya pili ikikusanya pointi 12 na kuweka rekodi ya kuwa timu pekee ambayo haijapoteza na imeshinda mechi zote nne za ligi msimu huu.

Hapa Mwanaspoti limekuchambulia baadhi ya mambo yanayoiangusha Yanga Princess mbele ya Simba na ligi kiujumla.


TATIZO LIKO HAPA

Rekodi kwa jumla zinaonyesha kwenye ligi, Yanga imeshinda mechi moja tu dhidi ya Simba tangu mwaka 2018 na zimekutana mara 13, zikitoka sare tatu na imepoteza tisa ikiwamo ya juzi.

Shida ni hii:


YA04
YA04

KUKOSA MUUNGANIKO

Yanga imesajili takriban wachezaji 13 wa kigeni. Na kila eneo wapo ikiwamo mabeki, Angela Chineneri, Igwe Uzoamaka, Wema Maile na Danai Bhobho, huku viungo Nyabuong Yien, Agnes Pallangyo, Rebecca Omowumini na Adebisi Ameerat pia wakishusha straika Ariet Udong kutoka Ethiopia.

Kwa aina ya usajili waliofanya timu hiyo ni wazi ulikuwa na malengo ya kufanya makubwa kwenye upande wa wanawake ambao hawajawahi kubeba ndoo ya ligi.

Shida sio wachezaji, Yanga ina kikosi kizuri kuanzia kwa mabeki wake wa kati hadi mshambuliaji, lakini imekosekana namna nzuri ya kuwatumia kwenye ligi.

Mfano mzuri ni straika wake Udong ambaye ukimtazama unaona ana sifa zote za kuwa mshambuliaji kwani ana nguvu, kasi na ufundi lakini anachokosa ni msaada kutoka kwa viungo wake.

Kiungo mshambuliaji wa Yanga (namba 10) anakosa ubunifu wa kutengeneza mashambulizi kwenda kwa mshambuliaji wake ili kumrahisishia kazi ya kufunga, hivyo inampa ugumu na kuishia kupoteza mipira.


YA03
YA03

MAJERUHI/ VIBALI

Timu hiyo pia haichezi na namba 10 asilia, kutokana na wachezaji hao kuwa majeruhi na wengine kukosa vibali na baadhi kutumika kama mbadala wake.

Mabeki kama Wema na Bhobho msimu huu wametumika kama viungo wakisaidiana na Pallangyo baada ya Irene Kisisa anayecheza eneo hilo kukaa nje akiuguza jeraha la goti kwa takribani miezi sita.


YA02
YA02

PASI ZA VIUNGO TATIZO

Viungo hao wanashindwa namna ya kuchezesha timu na kupiga pasi kwa ufasaha na wakati mwingine pasi zinapotea katikati ya wapinzani kutokana na uwezo wa wachezaji wa Simba.

Pia wanashindwa kuwa na jicho la wapi wapige pasi hasa wanapokosa uwezo wa kupiga mashuti ya mbali na hadi mchezo unatamatika haikupiga shuti lolote la hatari kwa wapinzani kutokea kati.

Hivyo Yanga inahitaji kiungo mshambuliaji ambaye atakuwa na uwezo wa kukukota mipira, kujua namna nzuri ya kupiga pasi na pasi za mwisho.


YA01
YA01

MABEKI WA KATI FRESHI

Licha ya udhaifu huo, Yanga Princess ina mabeki wazuri wa kati wanaoonekana kuwa na muunganiko mzuri kama ilivyo kwa Angela na Igwe waliowahi pia kucheza pamoja kule Bayelsa Queens ya Nigeria.

Kilichoonekana ni mashambulizi mengi ya Simba yalitengenezwa kutokea katikati ulipo udhaifu wa Yanga kwa kusogea karibu na lango lao, huku mabeki wa wananchi wakishindwa kufanya uamuzi wa haraka kuondoa hatari langoni mwao, ingawa mipira ya juu ilikuwa haipiti kirahisi kutokana na vimo vyao virefu.

Mabeki hao walikuwa watulivu kwenye eneo lao wakikaba kwa kutumia akili na hii ni dhihirisho la asilimia kubwa ya Yanga kufungwa mabao machache inatokana na wawili hao kuwa na muunganiko mzuri.


SIMBA BADO

Licha ya ushindi wa juzi lakini bado Simba inacheza kwa kiwango cha chini kutokana na nyota wake kutumika muda mrefu.

Wachezaji Violeth Nickolaus, Fatuma Issa ‘Fetty Densa’, Vivian Corazone, Asha Djafar ni miongoni mwa wachezaji ni ingia toka kwenye kikosi cha Simba kwa takribani misimu mitano wakicheza mechi mfululizo.

Kama Simba ingekuwa makini kwenye mechi ile ingemaliza mchezo mapema kutokana na nafasi walizokuwa wanatengeneza wakishindwa kuzitumia.

Kipindi cha kwanza Simba ilitengeneza nafasi tatu za hatari ambazo muda mwingi iliwatumia Elizabeth Wambui na Jentrix Shikangwa kufanya mashambulizi ambao walikosa utulivu kidogo.

Shikangwa ambaye alidhibitiwa na beki wa Yanga, Chineneri alikuwa mzito wa kufanya uamuzi akiwa eneo la goli.

Baada ya Simba kumkosa Daniela Ngoyi kwenye eneo la beki wa kati, Ester Mayala msimu huu ameonyesha kiwango bora na kuwa mbadala wa nyota huyo raia wa Congo akisaidiana na Violeth ambaye ameonekana kushuka kiwango hasa kwenye aina yake ya kuzuia.


MAKOCHA HAWA

Kocha wa Yanga, Edna Lema ‘Mourinho’ alisema walikosa umakini kidogo na kusababisha timu hiyo kuruhusu bao la kujifunga akikiri ameridhika na kiwango cha wachezaji wake.

“Nafikiri kila mmoja ameona kiwango cha wachezaji walichoonyesha, bado timu ipo kwenye matengenezo na naamini tutarudi uwanja wa mazoezi na kurekebisha yale tuliyoyakosea,” alisema Mourinho.

Kwa upande wa Simba, kocha wa timu hiyo, Yussif Basigi alisema ana furaha kushinda dabi yake ya kwanza.

“Yanga ina timu nzuri, nina furaha kushinda mchezo wa kwanza wa dabi na hii inatupa taswira ni namna gani ligi ngumu tofauti na nilipotoka Ghana.”