Prime
Zahir Zorro: Siumwi chochote, siachi muziki...
Muktasari:
- Ndivyo anavyosema mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Zahir Ally ‘Zorro’, baada ya kusikia habari watu wakisema anaumwa Kisukari na wengine kumwambia ana HI.
Mimi siumwi sukari, siumwi moyo, siumwi presha, siumwi HIV, figo, wala vidonda vya tumbo. Yaani niwaambie Watanzania siumwi chochote miye.”
Ndivyo anavyosema mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Zahir Ally ‘Zorro’, baada ya kusikia habari watu wakisema anaumwa Kisukari na wengine kumwambia ana HI.
Ni katika mahojiano maalum na mwanaspoti yaliyofanyika nyumbani kwake, Kigamboni, jijini Dar es Salaam, mtunzi huyo mahiri, mcharaza gitaa la solo na mwimbaji mwenye sauti nyororo, anafunguka mengi kuhusu maisha yake huku akisisitiza yeye ni mzima wa afya na kupungua kwake mwili ni kutokana na kuacha kufanya mazoezi na kupunguza kula, kwani alijua akila na kukaa ndani atanenepa na kuleta magonjwa mengine.
Anasema alilala kitandani mwaka mmoja bila ya kutokana nje, akawa anajibalansi kula sababu ni mtu wa mazoezi, maana tangu apate matatizo ya figo na nyongo kuvimba ambavyo kwa sasa ziko sawa, alikuwa anaomba mtu wa kumtoa ndani ndipo juzi kati wakatokea Fid Q, Wanene na Dash walienda kumwambia akafanye mazoezi kwa ajili ya uzinduzi wa shoo ya vionjo vya album ya Fid Q na Lord Eyes iitwayo ‘Neno’,
“Mimi najipunguza na kwa siku nakula mlo mmoja tu na hii ni kabla hata sijaacha mazoezi, nakula mlo mmoja na kula matunda, ila sasa hivi nimepata vifaa vya mazoezi nitaanza kula maana shida ilikuwa vifaa vya mazoezi ili niweze kuweka mwili sawa na kuanza kula. Ila siumwi nasisitiza mimi siumwi.”
Kifo cha Maunda sababu kunywa pombe
Anasema tangu Aprili 13, alipofariki dunia mwanaye Maunda, alisitisha shughuli zote za muziki kwani aliona ni ngumu bila yeye kutokana na kumzoea. Pia alikuwa akinywa sana pombe kali akiamini zitamuweka sawa kabla ya kuamua kuacha.
“Niwaambie kitu kimoja, maisha bila Maunda ni ngumu kumeza. Ndiyo maana tangu afariki dunia nilisitisha kufanya kazi za muziki nikajikita kwenye kumuombea dua.
“Nilimzoea sana mwanangu, ni kweli kufariki dunia imeniumiza sana. Mwanzo ilikuwa ngumu sana kukaa sawa. Nilikuwa nakunywa pombe kupitiliza hadi marafiki zangu walikuwa wameshanielewa, wakiniona nimetulia tu wananiuliza nataka nini? Mie nawaambia pombe kali, nikinywa nakuwa mchangamfu baada ya hapo naenda kulala. Hii hali ilinichukua muda mrefu kama mwezi mmoja, lakini baadae nikaja kuacha kunywa pombe kabisa, kwa sasa situmii pombe na niko poa.”
Banana, Mwana FA wampambania
Anasema alianza kuumwa siku ya msiba wa Maunda na watu walidhani ni kwa sababu ya kumpoteza mwanaye. Hata hivyo, anasema alikuwa na tatizo la kuvimba figo na nyongo.
“Unajua mimi mwanzo nilivyoumwa na kupelekwa hospitali na kulazwa kwa ishu ya figo na nyogo kuvimba, watu walisema ni sababu ya mwanangu Maunda namuwaza sana kwa sababu nilianza kuumwa ile siku aliyofariki dunia, Aprili 13.
“Nilikuwa natapika sana nyongo na uchafu mwingine, namshukuru Mungu, namshukuru Banana Zorro na Mwana FA walipambana kwa kusimamia vipimo na gharama zote nilizokuwa nadaiwa, wamenipigania sana kwa sababu wakati nimelazwa Muhimbili nilikuwa siwezi kula nilikuwa nakula tu matunda kama tikitimaji na juisi kwa muda wa wiki mbili.
Akuta nyumba imesafishwa
“Niliporudi kutoka hospitali nilikuta watoto wangu wametoa makochi yote sebuleni, wamesafisha nyumba, naona walijua kama nitakufa sitarudi, nilishtuka sana, sijui walifikiria nini ila nawashukuru kwa yote nilipona na kuendelea vizuri kabisa.”
Anasema ana deni kwa Mwana FA
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ alimpatia msaada wa vifaa vya mazoezi ikiwa ni sehemu ya ahadi yake kwa mzee huyo aliyotoa siku chache zilizopita akiwa kwenye uzinduzi wa vionjo vya album ya Fid Q na Lord Eyes iitwayo ‘Neno’. Mzee Zahir anasema hilo ni deni kwake.
“Kitendo alichonifanyia mwanangu Mwana FA ni kizuri sana, namshukuru sana kwa kunipatia vifaa vya mazoezi, niseme nina Deni nae kwani ameniokoa sana kwenye hili na Mwana FA ni mtoto ambaye tunaelewana naye sana kabla hata hajawa waziri, alikuwa ananisaidia mambo mengi sana, hivyo alivyoamua kunipa huu msaada Mungu azidi kumzidishia baraka.”
Banana ndio kila kitu
Anasema mwanaye Banana Zorro kwa sasa ndiye anamhudumia kila kitu, kuanzia chai, chakula cha mchana hadi usiku, hata kama haendi kumwona nyumbani, lakini mchango wake ni kubwa sana.
“Nikimzungumzia Banana, ni mtoto ambaye ananijali sana, ni mhangaikaji na mchapakazi, hata kama haji hapa nyumbani kuniona, ndiye anayejua kula yangu kuanzia asubuhi, mchana na jioni, ndiye namtegemea kwa sasa. Mungu azidi kumpa riziki kubwa mwanangu.”
Haachi muziki hadi anakufa
“Kuhusu suala la kuendelea na muziki, mimi bado nipo kwenye muziki na naimba na sitaweza kuacha muziki hadi nakufa.”
Kwa Diamond, Alikiba apata kigugumizi
Zahir kipindi cha nyuma aliwahi kufanya mahojiano na mwandishi wa makala haya na kusema anamkubali sana msanii Alikiba kuliko Diamond. Hata hivyo, kwa sasa anawakubali wote na kufichua kwa nini ilikuwa Kiba.
“Mimi bana napenda msanii anayeimba vizuri, asiyeimba matusi na nilisema namkubali Alikiba kwa sababu ni mtoto wangu, wa Kariakoo mwenzangu yule, ila hata Diamond namkubali, nimeona hivi karibuni ametoa nyimbo nzuri.”
Awapa makavu wasanii wa dansi
“Muziki wa dansi wa sasa ni tofauti na wa zamani. Hata wanamuziki wapo tofauti na wa zamani. Kwanza baadhi yao wamekuwa hawajipendi kwenye mavazi, yaani hawapo smati, utakuta mwanamuziki amevaa nguo tangu asubuhi, hiyo hiyo anayo mchana na kwenye shoo usiku anakuwa nayo, huu sio usimati bana. Ndiyo maana wanamuziki wageni wanaoingia nchini kufanya kazi wanatuzidi. Wakongo wanajua kuvaa na muziki wanafanya kama ajira kwao. Wapo smati, wanajipenda sana na wapo siriazi na kazi yao.”
Kumbe kuvaa cheni nyingi shingoni ni staili yake
“Watu wananisema sana kuhusu kuvaa cheni nyingi, wananiambia sioni uzito, mimi sioni uzito na sitaweza kuacha sababu hii ni staili ya maisha yangu. Hapa nimechelewa kutoka ndani kwa sababu nilikuwa napangilia kuvaa hii cheni kifuani na watu wasijue hizi ni gold (dhahabu), hapana, hizi ni Platnumz, naambiwa msela, ila mimi sio msela bana nina miaka 70 hadi sasa, mzee msela ni yule Seif Kisauji (kicheko).