CAFCL: Al Ahly yaanza na moto ule ule
Muktasari:
- Mabao mawili ya haraka katika dakika za awali za mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Nyayo na jingine la kipindi cha pili yaliotosha kuwavuruga mapema wenyeji na kulala 3-0, ikiwa imetoka kuwang'oa Al Merrikh Bentiu ya Sudan Kusini kwa ushindi wa jumla ya mabao 5-2 mechi za raundi ya kwanza.
WATETEZI wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ya Misri imeanza na moto kwa kuikandika Gor Mahia ya Kenya ikiwa jijini Nairobi ikiendeleza pale ilipoishia msimu uliopita ilipotwaa taji la pili mfululizo na la 12 katika historia ya michuano hiyo.
Mabao mawili ya haraka katika dakika za awali za mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Nyayo na jingine la kipindi cha pili yaliotosha kuwavuruga mapema wenyeji na kulala 3-0, ikiwa imetoka kuwang'oa Al Merrikh Bentiu ya Sudan Kusini kwa ushindi wa jumla ya mabao 5-2 mechi za raundi ya kwanza.
Rami Rabia alifunga dakika ya 14 kabla ya Percy Tau kuongeza la pili sekunde chache baadae kwa makosa ya mabeki wa Gor aliyekuwa akirudisha mpira kwa kipa Kevin Omondi na mfungaji kukwamisha katika lango jeupe kuandika bao la pili.
Kuingia kwa mabao hayo kuliifanya Gor Mahia kutulia na kutengeneza nafasi kadhaa ambazo hata hivyo zilipotezwa na washambuliaji wake, Enock Morrison, Rooney Onyango, Chris Ochieng' na Boniface Omond na kufanya hadi mapumziko kuwa nyuma kwa 2-0.
Kipindi cha pili timu zote zilicheza kwa kutengeneza mashambulizi ya kupokezana, ambayo hata hivyo yaliishia kutoka nje au mikononi mwa makipa timu hiyo klabla ya Tau kupigia msumari wa mwisho dakika ya 74 baada ya mabeki wa Gor Mahia kujichanganya.
Kupoteza kwa Gor Mahia nyumbani ni kama muendelezo wa gundu kwa timu za Kenya, kwani juzi Ijumaa, Polisi Kenya ilikandwa bao 1-0 na watetezi wa Kombe la Shirikisho, Zamalek ya Misri katika mechi ya mkondo wa kwanza wa raundi ya pili ya michuano hiyo kwa bao la Abdallah Sayed.
Timu hizo zote zitakuwa na kazi ngumu kupindua matokeo hayo ugenini wikiendi ili kutafuta nafasi ya kutinga makundi, kutokana na rekodi nzuri ilizonazo Zamalek na Al Ahly kwenye viwanja vya nyumbani jijini Cairo.
Msimu uliopit Al Ahly ilitwaa taji kwa kuwafunga Esperance ya Tunisia, huku Zamalek ikiifumua RS Berkane ya Morocco.
Gor Mahia iliyoanza; Kevin Omondi, Philemon Otieno, Kenedy Onyango, Sylvester Owino, Geoffrey Ochieng, Alphonce Omija, Enock Morrison, Austin Odhiambo, Rooney Onyango, Christopher Ochieng', Bonface Omondi.