Mwanamke ajinyonga baada ya kuliwa Sh1.2 milioni kwenye ‘betting’, aviator yatajwa
Muktasari:
- Mwili wa mwanamke huyo ambaye ni mfanyabiashara mdogo umekutwa ukining’inia ndani ya duka lake lililopo eneo la Kambiri Jimbo la Kakamega nchini humo jana Jumanne Oktoba Mosi 2024.
Mwanamke ambaye ni mkazi wa Jimbo la Kakamega nchini Kenya amejinyonga hadi kufa muda mfupi baada ya kupoteza fedha kiasi cha Sh1.26 milioni (Ksh60,000) kwenye mchezo wa kamari maarufu kama ‘betting’.
Mwili wa mwanamke huyo ambaye ni mfanyabiashara mdogo umekutwa ukining’inia ndani ya duka lake lililopo eneo la Kambiri Jimbo la Kakamega nchini humo jana Jumanne Oktoba Mosi 2024.
Kiongozi wa eneo la Kambiri lilipo duka la marehemu amethibitisha kutokea kwa kifo hicho huku mmoja wa wateja ambao walihudumiwa na marehemu muda mfupi kabla ya kukutwa amejinyonga amesema alikuwa anaonekana asiye na utulivu kichwani mwake.
“Nilienda dukani kwake mwanzoni alionekana yuko sawa, tulikuwa na mazungumzo mazuri lakini kadri muda ulivyozidi kwenda tukizungumza alianza kubadilika hadi nilipoondoka na baadaye nikaja kuambiwa kwamba amejinyonga,” amesema mteja huyo.
Shuhuda mwingine amesema mwanamama huyo amekuwa akijihusisha na kamari kwa muda mrefu sasa huku akishuhudiwa akitumia simu yake kuweka mikeka.
Shuhuda amesema kupitia utaratibu huo wa kuweka mikeka mwanamke huyo alipoteza kiasi cha Sh60,000 za Kenya ambazo ni zaidi ya Sh1.2 milioni kwa pesa za Kitanzania.
Kiongozi wa eneo ulipotokea msiba amewataka wananchi kutokaa kimya wanapopitia changamoto badala yake washirikishe ndugu jamaa na marafiki huku mwili wa mwanamke huyo ukichukuliwa na Polisi kwa ajili ya uchunguzi na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika jimbo hilo.
Ikumbukwe hili ni tukio la pili baada ya mwalimu wa sekondari ya Wavulana ya Nyamira nchini humo Kevin Omwenga kukutwa amefariki kwa kujinyonga nyumbani kwake Alhamisi Juni 7, 2024, huku ikidaiwa kuwa alipoteza Ksh50,000 (Sh1 milioni) kwenye kamari maarufu kama aviator au kindege.
Msaidizi wa chifu wa eneo hilo, Johnson Manyara alithibitisha kifo cha mwalimu huyo wa masomo ya kemia na hisabati.