Amorim anaanza na huyu
Muktasari:
- Jina hilo ambalo Amorim ametua nalo jijini Manchester na kwenda nalo viunga vya Carrington ni la winga wa Bayern Munich, Leroy Sane ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
MANCHESTER, ENGLAND: Kocha mpya wa Manchester United, Ruben Amorim ametaja jina moja la nyota anayetaka asajiliwe na miamba hiyo ya Old Trafford, dirisha la Januari.
Jina hilo ambalo Amorim ametua nalo jijini Manchester na kwenda nalo viunga vya Carrington ni la winga wa Bayern Munich, Leroy Sane ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka tovuti ya Daily Mail, Arsenal na Manchester United zipo katika vita ya kuiwania saini ya winga huyo na kocha wa washika mitutu wa London, Mikel Arteta anamhitaji kwa ajili ya kuzidisha ushindani eneo lao la kushoto anakocheza Bukayo Saka ambaye katika miezi ya hivi karibuni amekuwa akiandamwa na majeraha ya mara kwa mara.
Mpango wa Man United, kutaka kumsajili uliripotiwa kuanza tangu dirisha lililopita lakini kulikuwa na wasiwasi baada ya Amorim kuingia ikiwa ataruhusu.
Hata hivyo, kocha huyo amekubaliana na mpango huo na kuruhusu asajiliwe ikiwa timu zitafikia mwafaka.
Kwa mujibu wa tovuti ya Bild, Bayern ipo tayari kumruhusu kuondoka katika timu hiyo wakihofia kumpoteza bila ya kupata chochote mwisho wa msimu.
Inadaiwa Amorim amekubali Sane atue kutokana na historia yake EPL na kuwa na uzoefu wa ligi hiyo na kabla ya kuachana na Man City mwaka 2020 alikuwa ameshinda mataji mawili ya EPL, Kombe la FA na Mataji mawili ya Kombe la Ligi.