Angeweza! magwiji Man United wamtaka Van Nistelrooy
Muktasari:
- Magwiji hao wanaamini uwepo wa nyota huyo wa zamani wa mashetani hao wekundu, ungesaidia kuirudisha timu kwenye makali yake hasa kutokana na kuifahamu vyema klabu yake hiyo ya zamani na angesaidia zaidi eneo la ushambuliaji alilokuwa akicheza.
MANCHESTER, ENGLAND: MAGWIJI wa Manchester United wameponda kitendo cha timu hiyo kumwachia aliyekuwa kocha wa mpito, Ruud van Nistelrooy na ni kosa kubwa wamefanya.
Magwiji hao wanaamini uwepo wa nyota huyo wa zamani wa mashetani hao wekundu, ungesaidia kuirudisha timu kwenye makali yake hasa kutokana na kuifahamu vyema klabu yake hiyo ya zamani na angesaidia zaidi eneo la ushambuliaji alilokuwa akicheza.
Tangu apewe timu kwa muda kutoka kuwa kocha msaidizi, Van Nistelrooy amesimamia michezo minne na hajapoteza hata mmoja akishisnda mitatu na sare moja.
Kutokana na hilo, magwiji hao wakiongozwa na Rio Ferdinand kwa nyakati tofauti wamemzungumzia Ruud na kuona bado angefaa kuwepo katika benchi la Man United licha ya ujio wa kocha mpya, Ruben Amorim.
Baada ya kutua katika Jiji la Manchester juzi, Amorim alikutana na Van Nistelrooy mwenyewe na kumweka wazi hatakuwa naye katika benchi lake la ufundi alilotoka nalo Sporting Lisbon ya Ureno na hiyo kuashiria hatokuwepo tena kwenye klabu hiyo.
Rio ambaye ni beki wa zamani wa timu hiyo, alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema: “Wachezaji walihitaji kuwa na mtu kama yeye. Tuko katika wakati ambao kulikuwa na misukosuko mingi, uhusiano wa kocha aliyepita na baadhi ya wachezaji ulionekana kuvunjika na usingeweza kurekebishwa na hata mashabiki waliona hilo, chini ya Ruud wachezaji walikuwa wakimpenda sana, Walifurahishwa sana na namna alivyokuwa akiwaongoza na kuwafundisha, kuanzia timu kwa jumla na hata mchezaji mmoja mmoja.”
Kiungo wa zamani wa Man United, Owen Hargreaves alisema alipaswa kumbakisha Van Nistelrooy kwa sababu ndiye anayefahamu msingi na asili hasa ya timu hiyo, kwani ameshawahi kucheza hapo tena kwa kiwango kikubwa.
Owen alisema uwepo wa Van Nistelrooy angesaidia sana kuboresha viwango vya washambuliaji Rasmus Hojlund, Alejandro Garnacho na Marcus Rashford kwa sababu aliwahi kucheza eneo hilo na kuwa tegemeo kikosi cha kwanza.
“Walihitaji kujifunza kutoka kwake kwa sababu ni mmoja kati ya wachezaji bora kuwahi kutokea, angewasaidia kuwafuzza vitu vidogo vidogo mbali ya kuwafundisha uwanjani.”
Ruud ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa Man United kati ya mwaka 2001 hadi 2006, kabla ya kuajiriwa kama kocha msaidizi Julai mwaka huu chini ya Erik ten Hag mara kadhaa amewahi kusema angetamani kuendelea kuitumikia timu hiyo hata baada ya Amorim kuwasili.
“Nilikuja kama msaidizi kusaidia klabu kusonga mbele. Ukocha mkuu ni kazi ya muda mfupi, hilo linaeleweka, nafurahi kuifanya hii kazi na baada ya hapa nitarejea kwenye mkataba wangu kama kocha msaidizi nilionao hapa kwa msimu huu na ujao. Nitazungumza na kocha mpya na kuona itakavyokuwa.”