Salah aanza mazungumzo Liverpool
Muktasari:
- Salah amekuwa akihusishwa na timu mbalimbali za Saudi Arabia ambazo zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili tangu dirisha kubwa la mwaka jana.
LIVERPOOL imeanza mazungumzo wawakilishi wa mshambuliaji wao raia wa Misri, Mohamed Salah, 32, kwa ajili ya kumsainisha mkataba mpya lakini hadi sasa hakuna dalili ya kufikia mwafaka.
Salah amekuwa akihusishwa na timu mbalimbali za Saudi Arabia ambazo zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili tangu dirisha kubwa la mwaka jana.
Al Ittihad ilikuwa ni moja kati ya timu zilizohitaji kumsajili Salah na iliweka mezani ofa ya mshahara unaofikia Pauni 70 milioni kwa mwaka lakini ilishindikana.
Licha ya mazungumzo hayo yaliyoanza hivi karibuni uwezekano wa Salah kubakia unaonekana kuwa mdogo kwani kiasi cha mshahara anachohitaji ili asaini mkataba mpya ni kikubwa.
Benchi la ufundi la Liverpool halihitaji kuona Salah akiondoka na msimu huu amecheza mechi 17 za michuano yote na kufunga mabao 10 na kutoa asisti 10.
Martin Zubimendi
ARSENAL bado inaendelea kumfuatilia kwa karibu kiungo wa Real Sociedad na Hispania, Martin Zubimendi ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2027.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta anahitaji sana huduma ya Zubimendi kwa ajili ya kuweka sawa eneo lake la kiungo ambalo kwa kipindi cha hivi karibuni limeandamwa na majeraha ya mara kwa mara.
Murillo
BARCELONA na Real Madrid zinaendelea kumfuatilia kwa karibu beki wa kati wa Nottingham Forest na Brazil, Murillo, 22, ambaye ameonyesha kiwango bora tangu kuanza kwa msimu huu.
Murillo ambaye amejiunga na Nottingham katika dirisha hili, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028. Msimu huu amecheza mechi 11 za michuano yote na kufunga bao moja.
Cristian Romero
TOTTENHAM inataka kumsainisha mkataba mpya beki wao raia wa Argentina, Cristian Romero, 26, ambaye hivi karibuni ametajwa kuwa katika rada za Real Madrid ambayo inataka kuboresha eneo lao la ulinzi katika dirisha la majira ya baridi mwaka huu.
Romero mwenye umri wa miaka 26, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Milos Kerkez
BEKI wa kushoto wa Bournemouth, Milos Kerkez amefikia hatua nzuri katika mazungumzo na wawakilishi wa Manchester United ambai wanataka kumsajili katika dirisha la majira ya baridi au kiangazi mwakani.
Staa huyu wa kimataifa wa Hungury mwenye umri wa miaka 21, msimu huu amecheza mechi 11 za michuano yote na kutoa asisti mbili.
Igor Jesus
BAADA ya kuanza vibaya msimu huu, West Ham inataka kuboresha kikosi chao kwa kumsajili mshambulaji Botafogo na Brazil, Igor Jesus, 23, ambalo kocha Julien Lopetegui anaamini ndio lina mapungufu makubwa zaidi.
Igor ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027. Msimu amecheza mechi 24 za michuano yote na kufunga mabao nane.
Son Heung-min
MABOSI wa Tottenham wanafanya mchakato wa kutumia kipengele kilichopo katika mkataba wa mshambuliaji wao raia wa Korea Kusini, Son Heung-min.
Mkataba wa sasa wa Son unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu na kipengele hicho kipya kitawaruhusu kuurefusha hadi kufikia mwaka 2026.
Sergio Ramos
BEKI wa zamani wa Real Madrid na Hispania, Sergio Ramos, 38, yupo katika hatua nzuri kwenye mazungumzo yake na Corinthians ya Brazil ikiwa ni siku baada ya kutangazwa kwamba hana mpango wa kurudi Madrid licha ya timu hiyo kudaiwa kumhitaji.
Ramos kwa sasa yupo huru baada ya mkataba wake na Sevilla kumalizika mwisho wa msimu uliopita.