Neymar aandaliwa mkakati Santos
Muktasari:
- Hivi karibuni kumekuwa na tetesi kuhusu Neymar kuondoka timu hiyo, Januari mwakani na kama ikishindikana atasubiri hadi msimu utakapomalizika.
SAO PAULO, BRAZIL: SANTOS inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Brazil imeweka mkakati ili kuhakikisha Neymar anajiunga nayo mwakani baada ya kumaliza mkataba na Al-Hilal unaotarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.
Hivi karibuni kumekuwa na tetesi kuhusu Neymar kuondoka timu hiyo, Januari mwakani na kama ikishindikana atasubiri hadi msimu utakapomalizika.
Santos ndio timu iliyomlea inaamini mkakati waliouweka itakuwa ngumu Neymar kukataa kutokana na anayopitia tangu atue Saudi Arabia ambapo majeraha yamekuwa sehemu ya maisha yake.
Neymar amekuwa na wakati mgumu Al-Hilal tangu alipojiunga kutoka PSG msimu uliopita ambapo alicheza mechi kadhaa kabla ya kukaa nje kwa mwaka mzima na kurejea mwezi uliopita, na sasa amepata jeraha lingine ambalo litamuweka nje kwa wiki nne hadi sita.
Kwa ujumla kipindi chote alichocheza timu hiyo amecheza mechi saba za na kufunga bao moja.
Rais wa Santos, Marcelo Teixeira alisema ingawa bado hawajaanza kupanga kitakachotokea, lakini ikiwa atakuwa huru wanaweza kufanya kitu kwani wana uhusiano wa karibu na wawakilishi wake.
“Ikiwa atakuwa huru, basi tuna uhusiano na familia na mchezaji mwenyewe. Tunamfuatilia na tuna mipango halisi ambayo tumeshaijadili mara kadhaa juu ya namna tunavyoweza kumsajili. Lakini bado tunaendelea kusubiri,” alisema Marcelo.
“Huu sio wakati wa Santos kufanya haraka hilo. Kwanza tunahitaji kupanda Ligi Kuu ifikapo mwakani kisha kila kitu kitabadilika kuanzia bajeti, vipaumbele na miradi. Tukisema tunamsajili sasa bado haitakuwa na afya kwa timu.”
Santos ilifanikiwa kupanda daraja Jumatatu, wiki hii baada ya kushinda dhidi ya Cortiba mabao 2-0 ugenini.
Al Hilal imeripotiwa kutaka kuachana na Neymar lakini inataka aamue kuvunja mkataba ili kutopata gharama ya kumlipa fidia.