Sikieni! Jeremie Frimpong atajwa Manchester City
Muktasari:
- Frimpong ni miongoni mwa mastaa tegemeo katika kikosi cha Leverkusen na aliisaidia kuchukua ubingwa wa Bundesliga msimu uliopita.
KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola amewasilisha jina la winga-beki wa Bayer Leverkusen na Uholanzi, Jeremie Frimpong, 23, akitaka asajiliwe Januari mwakani.
Frimpong ni miongoni mwa mastaa tegemeo katika kikosi cha Leverkusen na aliisaidia kuchukua ubingwa wa Bundesliga msimu uliopita.
Pep anaamini Man City ambayo imepoteza mechi nne mfululizo zilizopita, moja kati ya maeneo yanayohitaji marekebisho ni lile la ulinzi.
Mkataba wa Frimpong unatarajiwa kumalizika 2028. Mbali ya Man City, huduma yake pia inahitajika na Liverpool na Man United.
Mbali ya Frimpong, Guardiola pia anataka huduma ya beki mwingine kutoka Uholanzi, Sepp van den Berg, 22, ambaye amejiunga na Brentford akitokea Liverpool.
Joshua Zirkzee
JUVENTUS inataka kumchukua kwa mkopo mshambuliaji wa Manchester United na Uholanzi, Joshua Zirkzee, 23, Januari mwakani.
Ripoti zinaeleza, Zirkzee aliyejiunga na Man United katika dirisha la majira ya kiangazi akitokea Bologna amekuwa hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha mashetani hao wekundu huku wengi wakimuona ni mzito uwanjani.
Jack Grealish
TOTTENHAM inataka kumsajili winga wa Manchester City na England, Jack Grealish, 29, katika dirisha dogo au kiangazi mwakani ambapo inaamini ina nafasi kubwa ya kumpata kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha Man City.
Grealish ambaye tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 10 za michuano yote, mkataba wake unamalizika mwaka 2027.
Jonathan David
WAKALA wa straika wa Lille na Canada, Jonathan David ameziambia timu zinazomhitaji mchezaji wake ambazo ni pamoja na Juventus, Inter Milan, Liverpool na Manchester United kuwa staa huyo anahitaji kiasi kisichopungua Pauni 5 milioni kama mshahara kwa msimu mmoja.
Staa huyu mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu Juni 2025.
Hugo Larsson
ARSENAL na Liverpool ni kati ya vigogo mbalimbali barani Ulay wanaohitaji kumsajili kiungo wa Eintracht Frankfurt na Sweden, Hugo Larsson, 20, katika dirisha la majira ya baridi mwakani.
Larsson ambaye msimu huu amecheza mechi 16 za michuano yote na kufunga mabao matatu, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Tomas Araujo
CHELSEA ni kati ya timu zinazohitaji kumsajili beki wa kati wa Benfica na Ureno, Tomas Araujo ambaye huduma yake inahitajika pia na Newcastle na Crystal Palace.
Araujo mwenye umri wa miaka 22, ni mchezaji tegemeo wa kikosi cha kwanza cha Benfica.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Christopher Nkunku
MSHAMBULIAJI wa Chelsea na Ufaransa, Christopher Nkunku, 26, ambaye anawindwa na Manchester United yupo tayari kujiunga na timu hiyo.
Nkunku hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Chelsea na kwa sababu hiyo anataka kuondoka hata kwa mkopo ifikapo Januari mwakani.
Samu Omorodion
BARCELONA inamfuatilia kwa karibu straika wa FC Porto, Mhispania Samu Omorodion, 20, ambaye imepanga kumsajili akawe mbadala wa staa wao kutoka Poland, Robert Lewandowski, 36, ambaye hana muda mrefu sana wa kuwatumikia kutokana na umri wake. Samu ametua Porto akitokea Atletico Madrid katika dirisha lililopita.