BELLA: Kama rahisi mkopi na nyie, kiingilio kinywaji haiwezekani
Muktasari:
- Baada ya kuutazama na kuusikiliza, Dakika 5 Na... ilikutana na maoni mengi ya wasomaji kwenye mtandao wa You Tube ya msanii huyo aliyejizolea umaarufu nchini na vibao vyake vingi ikiwamo ‘Yako wapi Mapenzi’, ‘Amerudi’, ‘Natamani’, Nisamehe na nyingine nyingi.
‘UTANIUA’ ndiyo habari ya mjini kwa sasa. Ni wimbo mpya wa Christian Bella ‘King of the Best Melody’. Umeusikia? Kama bado, kausikilize. Hakika na wewe utakuwa mmoja wa watakaouzungumzia.
Baada ya kuutazama na kuusikiliza, Dakika 5 Na... ilikutana na maoni mengi ya wasomaji kwenye mtandao wa You Tube ya msanii huyo aliyejizolea umaarufu nchini na vibao vyake vingi ikiwamo ‘Yako wapi Mapenzi’, ‘Amerudi’, ‘Natamani’, Nisamehe na nyingine nyingi.
Mkali huyo wa Bongo Fleva na Rhumba, hata hivyo, baada ya kusikia kelele nyingi mitandaoni, ameamua kuwajibu na kuweka wazi kila kitu kuhusu wimbo huo ambao wengi wanadhani amekopi kutoka kwenye wimbo wa ‘May Day’ wa msanii wa DR Congo, Fally Ipupa.
Dakika 5 Na... lilipata bahati ya kukutana na msanii huyo mwenye asili ya DR Congo na kupiga naye stori kuhusu utata wa wimbo huo na kipi mashabiki wanatakiwa wakifahamu.
Kachoka masebene, albamu ya Rhumba tupu inakuja
“Nilikaa nikaona nyimbo za dansi nyingi ni Masebene tu, utakuta wanaimba katikati au mwisho kuna kuwa na sebene nyingi za kurukaruka tu, ndiyo maana nikaamua kuja na rhumba hii ya ‘Utaniua ‘. Yaani ukimsikia DJ anapiga nyimbo za dansi ni sebene tupu.”
“Sasa hii ‘Utaniua’ madj wakipiga dansi zisiwe sebene tu bali ziwe na za Rhumba. Ndiyo Oktoba 18, naachia albamu ya Rhumba tupu.”
Kama rahisi kukopi, na wao wakopi
“Hao wanaongea hivyo ni baadhi ya mashabiki wanaopenda kukosoa. Yaani wanasubiri ufanye kitu hata kama ni kizuri wao wanakosoa, kusapoti aaah!”
“Acha waseme nimekopi kwa Fally Ipupa lakini wimbo unaendelea kufanya vizuri. Acha waseme nimeishiwa lakini wimbo unaendelea kufanya vizuri huko You Tube. Kama ni rahisi na wao wakopi.”
Kapondwa sana
“Kwanza mimi hakuna wimbo naweza kuutoa mashabiki wa dansi wakaacha kuuponda. Hata ‘Nani kama Mama’ ulishapondwa sana lakini leo hii unekuwa wimbo bora ndani ya miaka 11, watu wanauimba na kuucheza. Niwaambie tu baadhi ya mashabiki waache hasira na mimi.”
Mashabiki wabadilike
“Mara utakuta mtu anakomenti tu Bella sio yule wa zamani, yaani sasa amepotea kabisa hatoi nyimbo kama za zamani, (Kicheko), kwa hiyo watu walitaka nibaki kizamani nisiende na wakati? Yaani kila siku niende na wimbo wa ‘Safari sio Kifo’, ‘Mapenzi yako Wapi’, ‘Msaliti’.. kama mimi nimebadilika basi na wao wabadilike katika komenti zao.”
Ni mwanamuziki
“Kwanza watu watakuwa wananikosea sana kuniita msanii wa muziki wa bendi au Bongo Fleva. Mimi ni mwanamuziki kwa jumla, nafanya muziki kufurahisha kila mtu, wanahiphop, wana bongo Fleva, wanadansi, wanataarab ndiyo maana naitwa mwanamuziki.”
Bongo Fleva imemtoa
“Sema kuna kitu watu hawakijua mimi bila Bongo Fleva nisingekuwa hapa nilipo. Imenisaidia sana. Muziki wa dansi ulivyoshuka mwaka 2010 nikaachana nao kabisa na nikaenda Sweden kupumzika, kabla sijaondoka nikafanya wimbo mmoja wa Bongo Fleva na Banana Zoro inaitwa ‘Usilie’, huu wimbo umefanya vizuri sana na kipindi hicho muziki wa Bongo Fleva ndiyo upo kwenye chati.
“Nikausoma upepo nikahamia kutoa nyimbo na Ali Kiba, Ommy Dimpozi ‘Nani Kama Mama’, hivyo najua kucheza na upepo na ndiyo maana sitaki kuambiwa mimi ni msanii wa fani moja.”
Hapigi shoo za viingilio vinywaji
“Ni kweli. Hii ni jinsi nilivyojibrandi na muziki wangu. Kwa wasanii wa dansi mimi ndiye ninayelipwa pesa kubwa sana kwenye shoo. Hivyo, naiwakilisha vyema dansi na kuupa thamani yake.
“Hii ndiyo tofauti ya wao na mimi, sipigi shoo ya viingilio kinywaji, sipigi shoo kwa mazoea ya sehemu moja kila siku, kila Ijumaa nitakuwa ukumbi fulani au kila Jumamosi na Jumapili nitakuwa sehemu fulani.
“mimi shoo zangu unaniita unanilipa vizuri unaweka kiingilio nafanya kazi. Hata ukiniita uswahilini, nafanya kazi ilimradi tu malipo yawe mazuri.
“Kiufupi sifanyi shoo za mkataba wa sehemu moja muda mrefu, nimeamua kuupa thamani muziki wangu na sio kingine, ndiyo maana nilijiongeza kuingia kwenye Bongo Fleva kuwapata watu wa aina nyingine ya muziki na nimefanikiwa.”
Alitaka kujaribu Amapiano
“Amapiano ni muziki mzuri, kuna kipindi nilitaka kuimba lakini nikaona kila nikitaka kuingia studio unasikia msanii katoa ngoma, nikaamua kuachana nayo. Kwanza kazi kubwa ya muziki huo ni ya projuza sio mwimbaji.”
Yule Mzungu sio, mpenzi wake ni Mtanzania
“Sina mwanamke Mzungu. Watu wengi wanafikiriaga hivyo. mimi mwanamke wangu ni Mtanzania ila anaishi Sweden, nimeanza naye na mahusiano ni tangu mwaka 2008, hadi sasa amenizalia watoto watatu, nampenda sana na kumheshimu. Anaitwa Mary. Nimetamba naye sana kipindi nipo na bendi ya Akudo.”