Ney wa Mitego: Ukiwa muoga hutoboi
Muktasari:
- Wa Mitego aliliambia Mwanaspoti kwamba, uoga wa baadhi ya wasanii wa kujitengenezea brandi inayoeleweka imekuwa ikiwafanya wasitoe ngoma za maana za kuwabeba kibiashara.
MKALI wa Bongo Flava, Nay wa Mitego amesema kila msanii ni lazima ajitathmini na kuacha uoga katika fani na badala yake ajigengenezee mazingira ya kipekee kwa sababu hiyo ndio biashara yake, la sivyo hatoboi.
Wa Mitego aliliambia Mwanaspoti kwamba, uoga wa baadhi ya wasanii wa kujitengenezea brandi inayoeleweka imekuwa ikiwafanya wasitoe ngoma za maana za kuwabeba kibiashara.
“Ukiwa msanii, lazima uwe na thamani yako, usiwe tu wa kawaida, hiyo ndio biashara siku zote. Mie nimekuwa najiwekea mazingira mazuri na kunifanya niogopeke, hata ukija unakuja na ngoma basi ni lazima kazi itakuwa bora na itakubeba,” alisema staa huyo anayefahamika kama Rais wa Kitaa, aliyeongeza;
“Hata muziki wangu nauchukulia siriazi zaidi, kila ninachokifanya lazima ni kiogope na nikiheshimu, sijichukulii poa, wa kutambua hii ni biashara na kila msanii anapaswa kuwa hivyo.”
Staa huyo ambnaye amekuwa akikumbana na misukosuko kutokana na ngoma zake nyingi kuwa na mistari tata inayotikisa nchini, kwa sasa anatamba na kichumba cha wimbo wake mpya uitwao 'Hustler' aliomshirikisha Darassa.
Mbali na ngoma hizo, lakini mkali huyo amekimbiza na nyimbo kama Jiangali, Amkeni, Bachela, Atakuoa Nani, Hunijui, Rais wa Kitaa, Pale Kati, Mungu Yu Wapi, Shika Adamu Yako na nyinginezo kibao.