Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TUONGEE KISHKAJI: Sanaa siyo ngazi kutengeneza maskini wenye majina makubwa

Muktasari:

  • Ngoma hiyo ilitoka miaka zaidi ya 10 nyuma, lakini ajabu ni kwamba ujumbe wake unaishi mpaka leo. Yaani ni kama vile imetengenezwa enzi hizi za kizazi cha Instagram na intaneti.

RAPA Lord Eyes ana ngoma inaitwa Sanaa. Kwenye ngoma hiyo, rapa mwenzake wa kundi la Weusi, Joh Makini anaimba kiitikio chenye mistari inayosema “sanaa isiwe kazi ya kutengeneza maskini wenye majina kubwa”.

Ngoma hiyo ilitoka miaka zaidi ya 10 nyuma, lakini ajabu ni kwamba ujumbe wake unaishi mpaka leo. Yaani ni kama vile imetengenezwa enzi hizi za kizazi cha Instagram na intaneti.

Alichokuwa anamaanisha Joh kwenye ngoma hiyo ni kwamba, Tanzania imejaa mastaa kibao hususan wa ‘mainstream’, huku wengi wakiwa wanafanya muziki na filamu.

Ukisikiliza nyimbo za wasanii hao wa ‘mainstream’ wengi wanaongelea maisha fulani ya kibosi, magari mazuri, pesa kama zote, mademu kibao, starehe, mitungi na vitu kama hivyo. Ukirudi kwenye video za ngoma zao ndo usipime wanajionyesha wakiendesha magari makali, wakila bata na kadhalika. Na ukija kwenye Instagram ndo utaomba poo, mwendo ni ule ule, mara wanapeana zawadi za ma-range kwenye birthday zao, mara wanaonyesha mijengo ya gharama wanayoishi, fujo tu.

Wasanii wa filamu nao hawapo nyuma. Kwenye filamu zao kila mwigizai ni tajiri. Ni bosi. Anaendesha magari makali. Anaishi kwenye kasri na mbanga kama hizo. Kwenye filamu, wasanii wanaishi maisha ambayo pengine mimi na washkaji zangu huku mtaani hatutakuja kuyaishi hata siku moja.

Kwenye Instagram nako hawapoi - hawaboi. Miksa kwenda kula bata Dubai, vacation za Santorini, simu kalikali za milioni sabasaba. Ni checheeee.

Tunafahamu kwamba baadhi ya wasanii wanaongopa. Magari wanayopeana kama zawadi za birthday ni maigizo. Hao hawatusumbui. Lakini wengi ni watu ambao vitu wanavyoonyesha kwenye mitandao wanavimiliki kweli. Wana magari mazuri kweli. Wanaishi nyumba kali kweli. Wanakula bata kweli na bila hicho ndo kinachotengeneza masikini wenye majina makubwa. Kwanini?

Kwa sababu ni gharama kuishi maisha ya gharama. Wasanii wanapata pesa, lakini wanalazimika kutumia yote ili kuishi maisha ya kujionyesha kwamba wao ni wasanii, wako vizuri.  Na kwa sababu hiyo wasanii hujikuta wanalazimika kufanya vitu vinavyowaumiza ili tu kuendana na kasi ya maisha wanayotaka watu waone wanayo.

Ndo hapo stori za msanii kuanza kukubali shoo ya laki mbili kila wiki kwa sababu akisubiri za milioni 20 kwa mwezi mara moja atachelewa. Huku wasanii wa filamu wakikubali kuigiza kwa kulipwa elfu hamsini hamsini kwa sababu akisubiri kazi za milioni 20 haziji.

Na uchumi huwezi kushindana nao. Kamwe huwezi kuishi maisha kuzidi kipato chako. Utajaribu kuficha we' lakini mwisho wa siku utashindwa na ukweli utakuumbua. Mwisho wa siku ndiyo sasa msanii anauza magari yake, simu na vimali vyake vya hapa na pale na kubaki na jina. Na hapo ndipo Joh Makini anapokuja na chorus yake, “Sanaa isiwe ngazi ya kutengeneza maskini wenye majina makubwa.”

Badala ya wasanii kupambana kuonyesha jamii kwamba wamejipata, ni bora wapambane kuweka sawa mifumo yao ya kujiingia kipato kupitia sanaa ili mambo kama hayo yasiwatokee kila siku maana hadithi nyingi za wasanii wa Kibongo zina mwisho usiopendeza.