Alponce Modest azidi kuteseka, amuita MO Dewji
Muktasari:
- Mchezaji huyo wa zamani wa Pamba, Simba, Yanga na Mtibwa Sugar mwili wake haufanyi kazi kuanzia shingoni kushuka mpaka miguuni, ingawa miguu yake anaweza akaitingisha, lakini siyo kusimama wala kugeuka na amelala kitandani kwa zaidi ya miaka 14.
BAADA ya Mwanaspoti kuibua taarifa kuhusu hali ya kiafya ya beki wa zamani wa Simba, Alphonce Modest, baba mzazi wa staa huyo, amefafanua kinachoendelea kwenye familia huku nyota huyo akimtaja muwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji Mo.
Mchezaji huyo wa zamani wa Pamba, Simba, Yanga na Mtibwa Sugar mwili wake haufanyi kazi kuanzia shingoni kushuka mpaka miguuni, ingawa miguu yake anaweza akaitingisha, lakini siyo kusimama wala kugeuka na amelala kitandani kwa zaidi ya miaka 14.
Muda wote uso wa staa huyo umeangalia kwenye paa la nyumba ya mzazi kutokea katika kitandani alicholala. Baba mzazi wa staa huyo, Modest Alphonce Sr ameliambia Mwanaspoti hali ngumu ya kiuchumi wanayoipitia, inayomfanya asichoke kujitokeza kwa Watanzania ili kuendelea kuomba msaada wa kifedha za kusaidia matibabu ya mwanaye huyo.
Mzee Modest ameweka wazi kuwa simu nyingi alizopokea baada ya Mwanaspoti kuripoti hali yake ni za wachungaji wakimuombea na kuahidi kuendelea kufunga na kuomba kwa ajili ya mchezaji huyo wa zamani wa Taifa Stars.
"Nashukuru Watanzania ambao wanatupigia simu, kutupa moyo kama watumishi wa Mungu ambao wanakuwa wanamuombea, lakini bado niendelee kuwasumbua kwa kuwaomba msaada wa kifedha, kwani yapo baadhi ya mambo ambayo siwezi kuyatatua nje na pesa, kabla hajaumwa alikuwa tegemeo la familia na sasa kalala kitandani anatutazama sisi, ambao hatuna uwezo kiuchumi.
"Nafahamu hali ya kiuchumi ni ngumu kwa kila mtu, ila ambao wataguswa kwa chochote tutashukuru, wapo ambao wameahidi wakipata watatusaidia."
Anasema matibabu yanayotakiwa kwa kijana wake ni ya kumlipa daktari wa kumfanyia mazoezi na mwanasaikolojia wa kuijenga akili yake inayosubiri kifo, kwani amekataa tamaa kutokana na kuumwa na kulala muda mrefu kitandani. Lakini vilevile anahitaji chakula bora ili kumweka katika mazingira mazuri kiafya.
"Mzazi yoyote anayepitia hali kama yangu anaweza akaelewa, kwani ni ngumu kuona mtu mzima kama mimi, mwanangu wangu amelala kitandani nashindwa kumpa msaada, wakati kwa hali ya kawaida nilitarajia angekuwa msaada kwangu, ila mipango ya Mungu haina makosa," amesema.
Anaendelea kusimulia anavyoyashuhudia mateso ya mwanaye, inapofikia hatua ya misuli yake kukaza, kiasi kwamba anashindwa hadi kuzungumza zaidi ya kuugulia maumivu, jambo ambalo kama mzazi anajikuta anaumia moyo.
"Kuna wakati nakaa dirishani, namwangalia anavyougulia maumivu na kusikia sauti ya kilio, ukimuongelesha hawezi kukujibu zaidi ya kumuona machozi yamemjaa usoni, kama baba najisikia vibaya sana, nakuwa natamani ningekuwa na pesa basi ningemsaidia," anasema.
ALIVYOANZA KUUMWA
Mwanaspoti limezungumza na Modest anayeishi Kigoma, anasimulia jinsi ambavyo alianza kusumbuliwa na sasa amekuwa mlemavu wa kulala kitandani, huku matumaini ya kuishi yakipotea.
Akiwa amelala kitandani, hawezi kugeuka hadi msaada wa ndugu zake, anasimuliwa dalili ya ugonjwa ulivyomuanza, anakumbuka ilikuwa mwaka 2005, kuna usiku mmoja, akiwa amelala aliota ndoto ambayo ikaja kuonyesha uhalisia wake baada ya kuamka asubuhi.
"Kuna siku niliota paka watatu, mmoja alikaa kichwani, mwingine alikaa ubavu wa kushoto na mwingine wa kulia, wakawa wametoa macho makali sana, kisha nyama ilikuwa mbele yangu sikujua ni nyama ya nini.
"Nikawa naamrishwa kula nyama, wakati nagoma wale paka wakawa wanataka kunirarua, nikawa napambana sana, ikanibidi nile ile nyama, kuamka baada ya kula nikawa nimetoka jasho jingi sana, mwenzangu niliyekuwa nimelala naye, akaniuliza umepata shida gani, maana ulikuwa unaweweseka na unatiririka jasho, nikamsimulia ile ndoto.
"Wakati nashuka kitandani miguu ikaanza kuniuma sana, nikawa nakanyaga kwa shida, sikuacha kwenda kazini, nikawa nanunua dawa nakunywa, najitahidi kufanya mazoezi na kuchua lakini wapi, nikawa naenda hospitalini napata dawa narudi, kuna wakati niliambiwa ute wa kwenye magoti umeisha.
"Kuna siku nikazidiwa nikapelekwa hospitali ya kiwanda cha Mtibwa, baada ya kupimwa nikaonekana nyonga yangu imeachia, wakasema hawawezi kunitibia, ikabidi nipewe rufaa ya kwenda hospitali ya taifa Muhimbili, ambako nikapokewa na kufanyiwa vipimo zaidi, ilikuwa mwaka 2018.
"Baada ya kupata matibabu, nakumbuka kuna upasuaji nilitakiwa nifanyiwe ndipo mmoja wa madaktari bingwa wa magonjwa ya mifupa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi), akaniambia usipoteze pesa yako, unapaswa ufanye mazoezi ili nyonga yako iweze kuunga na kwa tatizo lako unaweza ukapata ulemavu wa kudumu.
"Nikawa nafanya mazoezi ndio kwanza hali ikawa inazidi kuwa mbaya, basi nikawaambia ndugu zangu hatuna budi kurudi nyumbani, tukachangiwa nauli nikarejea Kigoma, usione naongea sana, nilikuwa mkimya ninayependa utulivu, ila kwa sasa ugonjwa umenifunza kuongea, maana ninapotembelewa na watu inakuwa ndio muda wangu wa kupata faraja, wakiondoka nabakia kimya muda mrefu."
"Wakati natoka Dar es Salaam, nilikuwa na uwezo wa kukaa kwenye kiti cha walemavu, kujilisha mwenyewe, kadri muda unavyokwenda nikashindwa, nipo hapa kitandani kwa zaidi ya miaka mitano, siwezi kila kitu zaidi ya kuongea."
ANACHOHITAJI
Anasema anahitaji madaktari wa kumfanyia mazoezi ya viungo, kwani kuna wakati misuli yake inakuwa inakaza, anasikia maumivu makali yanayomfanya ashindwe kuzungumza kabisa.
Kinachomuumiza zaidi, hata akisikia maumivu, mikono yake haiwezi kushika popote, wala miguu yake kutembea, anajikuta akiishia kulia na kusubiri maumivu yapoe.
"Kuna wakati natamani mikono yangu ingekuwa na nguvu ama ingekuwa inafanya kazi, kwamba naweza kushika panaponiuma, naishia tu kupata maumivu ambayo hayaelezeki.
Anaongeza: "Natamani siku moja itokee niweze kutoka nje nione jua, kama wenzangu wanavyoliona, natamani mikono ikae sawa niweze kula mwenyewe, kuliko ninavyolishwa kila siku na ndugu zangu.
"Nikipata madaktari wa kunifanyia mazoezi ya mwili nitajihisi mwepesi zaidi, tofauti na ninavyojisikia kwa sasa. Sitaki kuwasumbua kabisa watu, ninachoomba nisaidiwe kupata NSSF yangu, baada ya kustaafu soka nilikuwa nafanya kazi katika kiwanda cha Mtibwa Sugar, ingawa nilikuwa napokea kiasi kidogo, nikafanikiwa kupata pesa hiyo itanisaidia, kwa maana hata ya kupata matibabu."
Anasema kama baba wa watoto watatu, anajisikia vibaya kuona hawezi kuwajibika kwa watoto wake na kujiona kabakia baba jina.
"Ndio maana nikipata kiasi kilichopo NSSF, angalau nitaweza kuangalia namna gani ya kuwasaidia, mfano nina binti yangu anaitwa Vicky ambaye nilizaa mapema kabla ya kuoa, angalau nije nimpe mtaji."
AMLILIA MO DEWJI WA SIMBA
Anafurahia ugeni wa Mwanaspoti, kuona unakwenda kutimiza ndoto yake kubwa ya kupata nafasi ya kuzungumza na mfadhili wa Simba, Mohammed Dewji 'MO', ingawa anachotaka kumwambia ni siri yake hakutaka kuweka wazi.
"Natamani nipate nafasi ya kuzungumza na MO nikiwa hai, ila kutokana na mikono yangu kutoshika chochote na sina simu, kupitia gazeti hili, naamini anaweza akaona mwenyewe ama waliokaribu naye wakamwambia ombi langu.
"Ikiwezekana naomba uende ofisini kwake, umwambie namhitaji zaidi nizungumze naye, MO ni msikivu ana roho ya kibinadamu, naamini atakusikia na atanipa nafasi ya kuzungumza naye, angali nipo hai."
Anaulizwa nje na kuhitaji kuzungumza na MO, unataka Watanzania wakusaidie kitu gani? Anajibu "Sitaki kuwachosha ndio maana miaka 14 ya kuumwa kwangu hujawahi kunisikia mitandaoni wala popote, sitapenda kutukanwa, wengi hawajui nilichopitia nyuma ya pazia, ninachosubiri ni kazi ya Mungu itimie juu ya maisha yangu".
Akibahatika kuzungumza na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu atamwambia nini?; "Nitamuomba awakumbuke mabinti wanaocheza soka, nimeona Simba, Yanga zinapocheza kimataifa huwa anatoa pesa za bao, ili kuzipa moyo, namuomba afanye hivyo kwa mabinti ambao soka ni kazi yao.
"Unaona ninachokipitia, mfano akipitia mchezaji wa kike ambaye hawapati pesa nyingi kama wanaume, atakuwa na hali gani? Mimi ni baba nina watoto wa kike ndio maana nawaza mbali, sitaki kuwa mbinafsi, kwanza sitaki kumsumbua Rais Samia ana majukumu mengi ya nchi."
AHADITHIA MIKASA YAKE
Staa huyo alikuwa na nyumba mbili jijini Dar es Salaam, wakati anaanza kuumwa, aliyekuwa mkewe aliyezaa naye watoto wawili, anasema alimshauri wauze ili wapate pesa za matibabu, kilichofuata hakutaka kufafanua sana, badala yake akarudia kauli yake ya wanawake ni wakatili sana.
"Siwezi kusema sana eneo hilo, kwa sababu nina watoto naye wawili, Kelvin na Rachael, hivyo acha hilo libakie ndani ya moyo wangu, labda ninachotamani kingine angalau niwaone wanangu, ambao tangu walipoondoka na mama yao, sijawahi kuwatia machoni.
"Nilichojifunza, kabla sijapata umarufu nikiwa bado nipo Kigoma, nilikuwa na mdada ambaye alikuwa ananipenda sana, sikuwahi kumpa hata sumni, nikaenda mjini nikapata vinavyong'ara ila mwisho wa siku nikapigwa tukio.
"Ajabu yule mwanamke ambaye sikuwahi kumjali, alizalishwa mtoto mmoja na mwanaume mwingine lakini hajaolewa, ndiye anayekuja kunisaidia, kunijulia hali, kuna muda aliniomba akaniuguzie nyumbani kwake maana amefanikiwa kujenga, nilikataa kwa sababu sikuwahi kumtunza hata ndugu zake wataniona mtu wa hovyo kabisa, nilimuomba msamaha sana, aliniambia alishanisamehe na moyo wake una huruma na mimi ndio maana anataka akaniuguze."
Kutokana na mkasa huo, anawashauri watu maarufu, kutambua wanawake wanaokutana nao kwa sasa asilimia kubwa wanafuata pesa na umaarufu wao, wala hawana mapenzi ya dhati.
"Kwa mfano wachezaji waige alichokifanya staa wa Al Nassr, Msenegal Sadio Mane ambaye wakati anavuma sana, hakutaka kuoa, amekuja kuoa kipindi hiki tena binti wa kijijini kwao.
"Wale ambao wana watu wao walioanza nao chini basi, wasiwapuuze, maana wakilia machozi ya kweli yanaweza yakageuka laana katika mahusiano yao mengine, mastaa wengi wana vilio vya mapenzi baada ya umarufu wao kupungua."
Jambo jingine analoliona linavunja uhusiano kwa wachezaji ni umbali na majukumu yao ya kutotulia nyumbani. "Unapomlisha vizuri mwanamke chakula kinafanya kazi, unategemea anapohitaji tendo la ndoa atalipata wapi kama muda mwingi hushindi naye, umempendezesha, lakini huna muda wa kukaa naye karibu, anajikuta anaingia kwenye uhusiano na masharobaro wanaoshinda dirishani kwako wanaangalia TV, kisha wanamtamani anaanza 'kukuchiti' nao, uhusiano kwa mastaa ni mgumu sana."
Kitu kingine anachoona wachezaji wakifanye, wajue kutofautisha ushikaji na familia zao, ili kuepuka kuchukuliana wanawake na kujenga visa ama visasi.
"Ni kweli kuna urafiki ule ambao mnaweza mkawa kama ndugu, ila kuna maisha mengine ya wachezaji kuzoeana sana kwenye familia, mwisho wanaanza kuchukuliana wanawake, jambo la kufanya wanaweza wakajiepusha kwa kuweka kando ushikaji na ndoa."
Anaongeza: "Chunguza asilimia kubwa ya mastaa wengi ndoa zao, zinawasumbua, ama wanawake walioanza nao mwanzo hawapo nao, halafu wamebakia na wachuna pesa, wakizipata wanasepa."
KINACHOMFANYA AJISIKIE VIBAYA
"Mfano mazingira haya uliyonikuta nayo, lazima nitaonekana nilikuwa mpenda starehe, ndio maana naishi maisha duni, kuna wakati nawasikiaga watu wakiongea, jamaa alikuwa na jina kubwa, ila anaishi kimaskini sana, najisikia vibaya kwani naona naitukanisha familia na wanaonisema hawafahamu mapito yangu."
Anasema alinunua uwanja nyumbani kwao Kigoma, ambao ulikuwa karibu na barabara, lakini baada ya kuanza kupata changamoto, akatokea mwingine aliyesema alitangulia kulipia.
"Nilikuwa na lengo la kuwajengea wazazi wangu, baada ya kuona eneo hili tulilopo ni dogo ambalo pia nililinua, sasa mwisho wa siku kila kitu nimekosa, kwani sikuwa na nguvu ya kufuatilia tena," anasema.
KINACHOMLIWAZA CHUMBANI
Katika chumba chake kuna runinga ndogo, ambapo akilipia king'amuzi anakuwa anaangalia soka la ndani na nje, wakati mwingine muvi za Kinigeria, jambo linalokuwa linampa faraja kubwa.
"Tv ndio mke wangu, ndio rafiki yangu, kikiisha king'amuzi basi nabakia mpweke sana, kulala chini zaidi ya miaka mitano mchana na usiku, siyo mchezo ndio maana najiona ifike siku tu, niondoke duniani," anasema kwa uchungu.
KATIKATI YA MAHOJIANO MKUDE APIGA SIMU
Kati ya watu ambao walimsaidia Modest ni pamoja na kiungo wa Yanga, Jonas Mkude, jambo lililomfanya mwandishi kumtumia ujumbe staa huyo wa Wanajangwani ambaye akaamua kupiga simu.
Mkude bila kusita akapiga 'video call' akapewa Modest ili kuzungumza naye, jambo lililoibua tabasamu kwenye uso wake, kuona bado anakumbukwa na mdogo wake.
Mazungumzo yao yalikuwa: "Nashukuru sana bwana mdogo kwa upendo wako, huwa nafarijika nikikuona katika tv unacheza, nakuombea kwa Mungu azidi kukubariki, una moyo wa kipekee sana, tofauti na baadhi ya watu katika jamii wanavyokuchukulia."
Majibu ya Mkude: "Nimefurahia kukuona, nakuombea kwa Mungu akupe afya njema, azidi kukubariki kaka yangu, hiyo ni mitihani, itapita na utaendelea na maisha mengine ya furaha." Wakamaliza.
Mazungumzo ya mwandishi na Modest yakaendelea, akaulizwa mbona unamshukuru sana Mkude? Akajibu: "Kuna kipindi Mkude alinitumia Sh500,000 wakati nikijiuguza Dar es Salaam, alikuwa ananijulia hali na kunipa moyo kwamba yatapita."
Huku na kule, staa wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella akampigia simu mwandishi baada ya kujua yupo Kigoma, kisha kuomba kuzungumza na Modest, mazungumzo yao yakaanza.
Modest: "Kaka nimepokea simu yako kwa heshima kubwa, kulingana na kazi ya soka, uliyoifanya katika nchi hii, binafsi kwa uwezo wako sikuwahi kuufikia, nimefurahia sana kukusikia, vipi habari za Morogoro?
Majibu ya Mogella; "Morogoro naendelea na mapambano ya maisha, pole kwa changamoto, usikate tamaa utapona, pia mpe ushirikiano huyo binti, ili Watanzania waweze kukusaidia hasa kwa wale watakaoguswa na tatizo lako, wewe ulikuwa mchezaji mkubwa na uliichezea Taifa Stars, acha kukata tamaa na uamuzi wako wa kufikiria kifo usitishe, kwani Mungu anamchukua amtakaye."
Kisha wakaanza kutaniana hapa na pale, kuhusu mambo ya uwanjani, ikawachukua kama dakika tatu katika maongezi yao.
Nje na Mkude na Mogella, anamtaja Kkatibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kidao Wilfred kwamba akienda kutembelea Kigoma, mara nyingi anakwenda kumtembelea.
SAFARI YAKE YA MAFANIKIO
Anasema wakati amekwenda kufanya majaribo Pamba, hakuchukuliwa kama mchezaji wa maana, ambapo kuna kiongozi alimpa Sh20,000 na akasema kabisa haoni kama ni mchezaji mzuri.
"Nikarudi nyumbani mara moja, wakati narejea kambini ilibidi baba yangu mzazi anipe nauli, kitendo kilichoniua sana, maana wenzangu walipewa pesa ndefu na niliona, baada ya kufika kambini kocha aliniambia wazi kwamba haoni kama nitapata nafasi ya kucheza kirahisi kwani alikuwa haniamini, jambo ambalo lilinitia hasira ya kufanya mazoezi sana."
Anaongeza: "Nilivyoanza kuaminiwa na safari yangu ya mafanikio kuanza, Pamba ilicheza michuano ya CAF, mechi ya kwanza dhidi ya Al Ahly iliyopigwa Misri, tukafungwa mabao 5-0, mimi sikupangwa, mechi ya marudiano kwenye Uwanja wa Kirumba, kocha akanipanga tukatoka suluhu, wakati huo Sanduy Kayuni alikuwa kocha wa Stars, akaniona na akaniambia umecheza vizuri sana.
"Baadaye akamfuata Nico Bambaga akamwambia yule kijana ni mchezaji mzuri, wakati anaita kikosi cha Stars likawemo na jina langu, ambapo nilichezea Stars tangu mwaka 1991 hadi 1998, pia nikawa nahodha wa Taifa Stars kwa miaka miwili mwaka 1998/99 na baada ya kwenda nje ndio sikucheza Stars na unahodha ukaishia hapo."
Anaulizwa kwake nahodha anapaswa kuwa na sifa zipi? Anajibu: "Awe na nidhamu, akubalike na wachezaji wenzake, awe kiunganishi baina ya wachezaji na viongozi, busara, hekima na awe tayari kutetea maslahi ya timu, kwangu mimi hizo sifa ni muhimu."
Alitegemea baada ya kuonyesha kiwango katika mechi ya marudiano dhidi ya Al Ahly, kocha angempanga katika mechi ya kwanza ya msimu dhidi ya Yanga ambayo walifungwa mabao 2-1, mechi zote zilizofuata akawa anaanza katika kikosi cha kwanza.
Kutokana na kiwango chake kizuri, Simba ikavutiwa na uwezo wake mwishoni mwa mwaka 1993 ikamsajili.
"Kiwango nilichokuwa nakionyesha wakati naichezea Simba, mechi za Ligi Kuu na kimataifa, timu nyingi za nje zilileta ofa, ila viongozi hawakuwa tayari kuniachia, hivyo nikazikosa, baadaye nikaenda mimi mwenyewe kuomba kucheza timu ya Township Rollers ya Botswana ambako nilisaini bure miaka miwili na mshahara nikawa napewa Sh200,000.
"Lengo langu la kusaini Township Rollers nilitaka iwe njia ya kuonekana na timu ya Jomo Cosmos ya Afrika Kusini ambayo iliwahi kuhitaji huduma yangu nikiwa Simba ni kweli ikapendezwa na huduma yangu, ila ikawa ngumu kupata barua ya kuachiwa huru kutoka Botswana.
"Baada ya kumaliza mkataba na Township Rollers 2001, nikampigia simu Jamal Byser nikamwambia maisha huku ni magumu, nashindwa hata kununua kiatu cha kuchezea, akanitumia Sh1,000,000 ila haikuwa na maelezo, nikamwambia napanda basi narudi, akanishauri kwa kuwa mkeo katoka kujifungua mtoto wa pili apande ndege, mimi nikarudi na basi.
"Baada ya kufika Mtibwa Sugar, kuonana na Byser nikamuuliza pesa uliyonipa ilikuwa ya nini, akajibu ya usajili wa mwaka mmoja, sikuwa na cha kufanya kwa kuwa sikuwa na pesa kabisa, akanisaini mwingine akanipa Sh1,000,000 na akaniahidi nikifanikiwa kupata namba mbele ya wanaocheza, ataniongeza maslahi.
"Nikacheza vizuri na kuwaweka benchi waliokuwa wanaanza kikosini, nikamfuata uliniahidi utabadilisha maslahi, akacheka tu na kuniambia tulimalizana.
"Nilistaafu kucheza soka wakati nacheza kikosi cha kwanza na kocha alikuwa ananitegemea mwaka 2003/4, sababu ilikuwa ni timu kushindwa kuchukua ubingwa, sikuona sababu ya kuendelea kucheza Mtibwa."
Anasema viongozi wa Kagera Sugar, wakampigia simu akaipandishe timu kama kocha, ambapo anataja baadhi ya wachezaji aliowasajili ambao ni Vincent Barnabas na Amri Kiemba. "Ila nikaja nikaondolewa na Shirikisho la Soka kipindi hicho ilikuwa inaitwa FAT, nilikosa vigezo, kwani sikusomea ukocha.
"Baada ya hapo nikarejea zangu kufanya kazi kiwanda cha Mtibwa Sugar, ambako nikaanza dalili za kuumwa miguu hadi kupata ulemavu unaoniona nao hadi sasa naugulia tu kitandani," anasema.
ANAMKUBALI TSHABALALA
Anamtaja nahodha wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala' kwa aina ya uchezaji wake anaona unataka kukaribiana na wa kwake, ingawa walitofautiana miili.
"Ingawa mifumo yao ya sasa ya 4-2-3-1 ni tofauti na zamani, Tshabalala anachotakiwa kukifanyia mazoezi zaidi ni anapopanda kushambulia, asisahau jukumu lake la kukaba, tofauti yangu na yeye mimi nilikuwa kipande cha mtu," anasema.
Mbali na hilo, anazungumzia uwepo wa wachezaji wa kigeni, ulivyo msaada kwa wazawa, ambao wakicheza timu ya taifa, wanapokutana na wapinzani wao hakuna kitakachowastaajabisha.
"Inawasaidia sana wanapocheza michuano ya kimataifa, wanakuwa wamepata uzoefu kupitia wageni wanaocheza nao katika ligi, nakumbuka zamani, tulikwenda kucheza Libya tukakutana na mchezaji aliyetoka kushinda tuzo ya Balon d'Or ya uchezaji bora wa dunia, George Weah, alikuwa kipande cha mtu, yaani wachezaji tunamshangaa, unaingia uwanjani unawaza mara mbilimbili jinsi ya kukabiliana naye."
Anaongeza: "Ilikuwa mwaka 1995 kama sikosei, ndio maana nasema kitendo cha uwepo wa wachezaji wa kigeni, kinasaidia sana, wazawa kuzoea."
Ukiachana na hilo, anawapa ushauri wa bure kuwa waangalifu na umarufu, unaoweza kuwajenga ama kuwabomoa maisha yao.
"Umarufu ni mzigo mzito, lazima mchezaji ajifunze kuwa mtulivu, angalau enzi zetu hakukuwepo na mitandao ya kijamii kama ilivyo sasa, ambapo kila kitu chao kwa sasa kinakuwa wazi, wasipokuwa makini umarufu unaweza ukawaumiza."
KIKOSI CHAKE CHA ZAMANI/SASA
Kikosi chake wakati anacheza ni Mohamed Mwameja, Deo Mkuki, Kenny Mkapa, Mustapha Hoza, Hussein Marsha, Nico Bambaga, Sekilojo Chambua, Edibily Lunyamila, Nteze John, Said Mwamba 'Kizota' au Madaraka Selemani na kocha anamchagua Sunday Kayuni.
Kikosi cha sasa Moussa Camara, Yao Kouassi, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Ibrahim Bacca, Abdulrazack Hamza, Yusuph Kagoma, Clatous Chama/ Debora Fernandes/ Aziz Ki/ Pacome Zouzoua hapo yoyote anaweza akaanza. Mfano Ateba akishambulia nyuma yake anaweza anasimama Pacome, kulia Aziz Ki na kushoto Chama.
"Sijamuanzisha Djigui Diarra kwa sababu atapewa changamoto na Camara, kiungo sijamuweka Mkude kwa sababu kwa sasa hachezi mara kwa mara, ila akiwa katika ubora wake lazima ataanza kikosi cha kwanza," anasema.
KAULI YA BABA YAKE
Baba mzazi wa staa huyo, anawaomba Watanzania angalau wamsaidie pesa za kumlipa daktari wa mazoezi na mwanasaikolojia, ili kuirejesha akili yake kuamini, licha ya kupitia magumu anaweza akayafurahia tena maisha yake.
"Mwaka 2018 alinipigia simu akisema, 'baba naumwa kama mtaendelea kukaa kimya na hamtakuja kuniona, basi nikifa msije nitazikwa huku huku', kauli yake ilinishitusa sana."
Anaongeza: "Nikafunga safari hadi Dar es Salaam, nikamkuta anasukumwa kwenye kiti cha wagonjwa, hali iliyonishitua sana, maana niliondoka na Sh50,000 nikijua nakwenda kumchukua na kurejea nyumbani.
"Nilikaa jijini Dar es Salaam miezi mitatu, kisha tukachangiwa nauli ingawa kuna mtu aliipiga Sh700,000 ya kwanza kabla haijatufikia na Sh500,000 ambayo pia ilichangwa bila kufika kwetu, hivyo tukaondoka na Sh200,000 ambayo tulikabidhiwa mkononi tukiitumia kama nauli kurudi Kigoma, hao watu siwezi kuwataja, maana mwenyewe hataki kuwaelezea.
"Ukiachana na ndoto yake aliyoota wakati anaanza kuumwa, miezi michache aliniambia, aliota yupo na watu wengi, ila wenzake wana vyeti yeye hana, wakati wanakimbia kuingia katika lango, kuna mmoja akadondosha cheti chake akakichukua yeye, ila alipofika getini kukaguliwa akarudishwa na kuambiwa hicho siyo cheti chako, rudi kakitafute, sasa sielewi inamanisha nini, naishia tu kumuombea kwa Mungu," anasema.
Anasema kwa sasa anamtegemea binti yake Teddy anayefundisha shule ya msingi ya binafsi, akipokea mshahara ndipo chakula kinunuliwe na kufanya matumizi mengine ya kumsaidia kaka yake.
Kwa upande wa mdogo wake, Augustino anasema alikuwa anafanya kazi katika kiwanda cha Mtibwa, alikuwa mkusanya data mashambani, kazi ambayo alitafutiwa na Modest.
"Wakati baba anakuja naye Kigoma, mimi nilirudi Morogoro kazini, baada ya miezi kadhaa, baba alinipigia simu kwamba niache kazi ili nije nimuuguze kaka yangu kama kijana wa kiume, nikafanya hivyo hadi sasa napitia changamoto ngumu ya kiuchumi."
Anaongeza: "Nimekaa na kaka tangu akiwa Mtibwa, nilimuuguza katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hivyo najua changamoto alizozipitia, lakini amekuwa hataki kabisa mambo ya media, anasema haina maana tena katika maisha yake, watu kutaka kujua maisha yake.
"Hapa tunapokaa ni yeye alinunua, alikuwa na mpango wa kupakarabati na kujenga nyumba nyingine ya familia katika uwanja ambao aliambiwa kuna mtu alitangulia kuulipia, hivyo pesa yake ikaenda bure."
Anasema kuna wakati anamwita mdogo wake na kumwambia mikono yake ingekuwa inafanya kazi, siku moja wangemkuta ameshakufa, maana amechoshwa na mateso.
"Kuna hospitali ya hapa Kigoma huwa tunakwenda, tukipata pesa kuna dawa anatumia, kama juzi tulishindwa kulipitia matibabu, hivyo akabakia na maumivu yake, ndio maana familia iliamua kuweka jambo hili wazi."
Mbali na hilo, anasema kipindi mama yao anafariki mwaka 2021, kaka yao alipata maumivu makubwa, maana ndiye alikuwa rafiki yake mkubwa.
"Mama alikwenda kuuguziwa Dar es Salaam, baada ya kusikia msiba wake, ilikuwa ngumu kumwambia kaka msiba huo, ingawa ni kama alikuwa anaweweseka na alikuwa anauliza ni kitu gani kimetokea, alipoambiwa ukweli, alikaa kimya kama wiki nzima, mkienda mnaona machozi yanamtoka tu," anasema.
JAMAL BAYSER
Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mtibwa Sugar, Jamal anasema; "Modest ni mchezaji wa kuigwa licha ya vijana wengi wa sasa hawajamuona, ila ni kati ya wachezaji bora waliowahi kutokea Tanzania, alikuwa anajitolea sana kwa ajili ya timu, popote anapokuwepo amani inatawala, alipenda kuwaona watu wanacheka.
Anaongeza: "Modest alistaafu akiwa na kiwango cha juu, aliniambia kiongozi nimecheza kwa muda mrefu naipisha damu changa, aliyekuja kumrithi nafasi yake, alikuwa Idris Rajabu. Uongozi uliona umefanya naye kazi nzuri, ukampa kazi kiwandani sehemu ya ulinzi kama afisa ulinzi, hadi pale alipoona hawezi tena anapaswa kurejea kwao Kigoma."
HASSAN DALALI
Kipindi Modest anajiunga na Simba, Hassan Dalali alikuwa mwenyekiti wa matawi Mkoa wa Dar es Salaam, anamzungumzia: "Alikuwa beki hatari, alipendwa na mashabiki, mcheshi, alijitoa kwa ajili ya timu, ndio maana Yanga waliona anaweza akawasaidia wakamwazima, kikubwa tunamuombea Mungu amponye maradhi yake."