Baxter: Mwamba alitisha kwa boli, pombe, mademu
Muktasari:
- Miongoni mwao ni yule anayetajika kama kiungo bora zaidi kuwahi kutokea Scotland kwa zaidi ya nusu karne, akisifika kwa michomo yake ya masafa marefu ya mguu wa kushoto.
KATI ya miaka ya 1960 na 1980 Scotland ilipata umaarufu wa kutoa wachezaji kandanda wazuri, lakini wengi waliiaga dunia wakiwa na hali mbaya ya maradhi kutokana na kutawaliwa na pombe.
Miongoni mwao ni yule anayetajika kama kiungo bora zaidi kuwahi kutokea Scotland kwa zaidi ya nusu karne, akisifika kwa michomo yake ya masafa marefu ya mguu wa kushoto.
Huyu ni James Curran Baxter aliyetamba kwa mchezo safi na kupenda pombe hata saa chache kabla ya kuingia uwanjani kucheza soka akitamba kati ya 1957 hadi 1970. Aliiaga dunia mwaka 2001 na sababu ya kifo chake ilikuwa ni pombe iliyoharibu vibaya figo zake.
Kwa kuonyesha mapenzi yake kwa pombe, Baxter alipoacha kucheza kandanda alifungua baa kwao Scotland na watoto wake kuwapa majina ya utani ya bia na pombe kali.
Licha ya mara nyingi kucheza akiwa amekunywa pombe japo kidogo muda mfupi kabla ya mchezo, Baxter aliliskata kabumbu vizuri.
Vile vile alipenda sana mabibi na ilikuwa kawaida kumkuta akinywa pombe huku akizungukwa na wanawake wanne hadi sita na wote kuwaita wapenzi wake.
Kila alipoambiwa apunguze kupenda wanawake alisema: “Mimi siwapendi isipokuwa wao ndio wananipenda na ninawakubalia sio kwa mapenzi bali kwa kuwaonea huruma. Lakini kubwa zaidi huona raha kunywa bia nikizungukwa na mabinti wazuri”.
Hata hivyo, aliwashangaza wengi alipofunga ndoa mwaka 1965 na Jean Ferguson, mfanyakazi wa saluni na kuzaa naye watoto wawili wa kiume, Alan na Steven. Ndoa yao ilivunjika maka 1981 na alimuoa Norma Morton na kuishi naye mpaka alipoiaga dunia.
Siku moja Baxter alipohisi mwamuzi hawatendei haki alimwambia ingekuwa vyema kama angeliwapa penalti wapinzani kabla ya kuanza kipindi cha pili cha mchezo.
Muamuzi alipokasirika Baxter alimwambia kama hilo lilikuwa haliwezekani basi angeliwaruhusu wapinzani wao waongeze wachezaji wawili na wawe 13 au awatoe wawili wa timu yake na wabaki 9 ili wapinzani wawe na uhakika ya ushindi.
Kutoka 1961 hadi 1967 hakukosekana katika kikosi cha timu ya taifa ya Scotland kilichocheza mara zaidi ya 10 na England na kushindwa mara moja tu katika mwaka 1965. Siku ile aliwataka Waskochi watangaze msiba wa kitaifa na wafunge vitabambaa vyeusi, kauli ambayo iliwakasirisha England.
Katika mchezo mmoja kati ya England na Scotland mwaka 1963, Baxter alionekana baa akiuchapa mpaka alfajiri na alipotaka kuzuiliwa asicheze, kocha alipelekewa ujumbe kwamba kichwa chake kitakuwa halali ya Waskochi kama timu yao ingelifungwa huku Baxter akiwa nje.
Kocha aliona afadhali ya lawama kuliko kuhatarisha maisha yake na alimchezesha Baxter ambaye alifunga mabao yote mawili katika ushindi wao wa 2-1 wakiwa na wachezaji 10 tu tangu katika dakika ya 35 ya kipindi cha pili. Siku ile baada ya mchezo Baxter alikunywa bia 21 kusherehekea ushindi wa 2-1.
Baxter alivutia mashabiki kwa chenga za maudhi na kutokata tamaa na siku zote alilumbana na waamuzi na washika kibendera. Tofauti na wachezaji na viongozi wa klabu za Glasgow ambazo zina uhasama wa miaka mingi, Baxter aliyeichezea kwa miaka mingi Rangers alikuwa rafiki wa wachezaji wa klabu ambayo ni mahasimu wao wakubwa, Celtic, na mara nyingi alikwenda baa kupiga vyombo na wachezaji wa timu hiyo.
“Mimi ni Rangers katika mchezo wa kandanda, lakini mwana wa Celtic inapokuja kufurahia pombe,” alisema.
Baxter alizaliwa Septemba 29, 1939 na kupata elimu yake katika kijiji cha machimbo ya madini cha Fife, karibu na mji wa Hill O’Beath, Scotland.
Baada ya kumaliza shule alitumia miezi minane kujifunza useremala na baadaye alikwenda kuchimba makaa ya mawe na wakati huo aliichezea klabu ya vijana ya Halbeath. Alikuwa mchezaji wa kulipwa wa Raith Rovers 1957 hadi 1960 alipojiunga na Rangers ya Glasgow ambayo aliisaidia kuchukua vikombe 10 kati ya 1960 na 1965.
Alipoumia mguu na kuwa nje ya uwanja kwa miezi minne alianza kunywa sana pombe na kuendelea hadi alipoiaga dunia.
Kabla, alihamia katika klabu ya Sunderland 1965 na kuitumikia kwa miaka miwili akitumika katika mechi 48.
Nottingham Forest ilivutiwa naye na kumsajili 1967 na akadumu nayo kwa mwaka mmoja tu huku akiendeleza tabia yake ya kunywa pombe kupindukia na hadi wakati mwingine kupoteza fahamu.
Forest, ikiwa imechoshwa na tabia yake ya ulevi, ilimhamishia bila ya malipo katika klabu yake ya zamani ya Rangers na huko ndipo alipomalizia kucheza kandanda akiwa na miaka 31.
Wakati alipong’ara uwanjani baadhi ya wakati Baxter aliwakimbia wachezaji wenzake dakika chache kabla ya kuanza mchezo kwenda kupata chupa moja au mbili za bia.
Baxter aliichezea timu ya taifa ya Scotland mara 34 akiwa na wachezaji mashuhuri wa wakati ule kama Billy McNeill, Pat Crerand, John White, Dave Mackay, Denis Law na John Greig. Aliifungia Scotland mabao matatu tu, lakini alikuwa sababu ya kupatikana zaidi ya magoli 30 akiwa mchezaji wa kiungo.
Wakati alipokuwa katika kikosi hicho, Scotland ilishinda michezo 21, ilitoka sare michezo mitatu na kufungwa 10.
Mchezo uliomtibua sana ni ule wa 1961 Scotland ilipochapwa mabao 9-3 na England kwenye Uwanja wa Wembley na aliahidi kulipiza kisasi wakati wa uhai wake na alifanikiwa 1962 Scotland ilipoifunga England 2-0, bao moja likiwa lake. Mwaka uliofuata Scotland, ikiongozwa na Baxter na rafiki yake Dennis Law iliinyuka England 1-0.
Kocha wa zamani wa Manchester United, Alex Ferguson, anasema mara nyingi hatasahau namna Baxter alivyokuwa akimtesa yeye na wenzake kwa chenga za maudhi na zaidi alivyokuwa anakucheka akishakupiga chenga.
Alipostaafu alifanya kazi ya meneja wa baa na alifunga baa yake huku akibaki ndani anakunywa ile mbaya mpaka asubuhi na kusababisha kuharibu figo zote mbili na kuwekewa nyingine alipokuwa na umri wa miaka 55. Vile vile alikuwa mcheza kamari na inakisiwa alipoteza zaidi ya pauni nusu milioni za Kiingereza kutokana na kamari.
Alipofariki mwaka 2001, akiwa na miaka 63 mazishi yake yaliyofanyika mjini Glasgow yalihudhuriwa na mamia ya wacheza soka na mashabiki wa zama zake kutoka Bara la Ulaya na Amerika ya Kusini.
Rafiki yake mkubwa na ambaye alipenda mchezo wake, Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza, Gordon Brown, wakati ule akiwa Waziri wa Fedha, aliulezea wasifu wa marehemu na kusema kama Waskochi wanatafuta nani mchezaji wao bora wa kandanda basi hakuna mwengine isipokuwa Baxter waliyeokuwa wanamuaga.
“Alikuwa mchezaji mzuri na mwenye akili, isipokuwa pombe ilimzidi akili kidogo. Ningelifurahi kama angelikuwa kazaliwa Brazil na kucheza naye timu moja. Nani kama Baxter,” alipata kusema mfalme wa soka, Pele wa Brazil.
Katika mwaka 2003, sanamu lake kama kukumbuka mchango wake katika kandanda kwa Scotland lilijengwa katika mji mdogo wa Hill of Beach, Scotland.