Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

BIG WEEKEND! Karata muhimu za heshima Yanga, CBE

Muktasari:

  • Ni mechi muhimu za kuamua hatma na kuweka heshima.  Yanga na Simba zote ziko viwanjani leo na kesho mtawalia, na huko Ulaya Arsenal watakuwa wageni wa Man City kwenye Uwanja wa Etihad, Inter Milan itakiwasha na mahasimu wao AC Milan katika Derby ya Italia na Man United itakuwa ugenini dhidi ya Crystal Palace.   

HII ni wikiendi ya moto viwanjani! Leo na kesho kuanzia Bongo hadi majuu kote kuna mechi za maana ambazo zitakufanya ugande mbele ya TV yako.

Ni mechi muhimu za kuamua hatma na kuweka heshima.  Yanga na Simba zote ziko viwanjani leo na kesho mtawalia, na huko Ulaya Arsenal watakuwa wageni wa Man City kwenye Uwanja wa Etihad, Inter Milan itakiwasha na mahasimu wao AC Milan katika Derby ya Italia na Man United itakuwa ugenini dhidi ya Crystal Palace.   

Simba itaikaribisha Al Ahli Tripoli katika mechi ya marudiano ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 10:00 jioni kesho ambako lazima mshindi apatikane baada ya mechi yao ya awali kule Libya kumalizika kwa suluhu.

Na kama wewe ni shabiki kindakindaki wa Yanga na muda unakuruhusu, basi fanya chapu kwa kuchukua boti ili uvuke bahari hadi Zanzibar. Ukiwa huko fanya mizunguko yako, ila ikitimia saa 2:30 usiku hakikisha unakuwa ndani ya Uwanja wa New Amaan Complex kupata burudani ya soka.

Ukiwa uwanjani hapo utapata nafasi ya kuiangalia timu hiyo itakapokuwa mweyeji wa CBE ya Ethiopia. Kuna wito maalum kutoka kwa wachezaji wa timu hiyo, ukishafurahi nenda pale Forodhani katambe.

Kuna tamko wamelitoa mastaa wa Yanga kwamba:

“Tumewasikia juu ya kilio chenu njooni mtafurahi.” Wakaishia hapo, maneno machache ambayo yanaweza kuwa mazito kwa CBE ikiwa mbele ya Yanga inayoitaka mabao ya kutosha na kufuzu hatua ya makundi kibabe.

Yanga itakuwa na dakika 90 za nyumbani dhidi ya CBE katika mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku mabingwa hao wa soka wa Tanzania wakifahamu kwamba sare yoyote inatosha kufuzu, lakini wachezaji wa Yanga wanataka kurudisha heshima yao kwa kufunga mabao mengi.

Mchezo wa kwanza kule jijini Addis Ababa nchini Ethiopia, Yanga ilivunja mwiko wa kutoshinda kwenye ardhi hiyo ikishinda kwa bao 1-0 lakini hilo halikuwafurahisha wengi kufuatia timu hiyo kutengeneza nafasi nyingi za kufunga ikitumia moja tu.


MAKOSA YAFANYIWA KAZI

Baada ya timu hiyo kurudi nchini, kwenye uwanja wa mazoezi yamefanyika mengi ya tofauti lakini asilimia kubwa yakatolewa mazoezi maalum ya kufunga mabao.

Mazoezi hayo hayakuwa kwa washambuliaji pekee, wameyafanya viungo na hata mabeki wakiongezewa ubora wa kuhakikisha mipira inaokotwa nyavuni kwa wapinzani mara nyingi kwa kadri iwezekanavyo na baada ya hayo yote vikafanyika vikao vya kuwajenga wachezaji kisaikolojia hasa washambuliaji.

YANGA INATAKA REKODI

Kuna rekodi kubwa Yanga itaiweka itakaposhinda au kufuzu makundi kwani timu hiyo haijawahi kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara mbili mfululizo ingawa msimu huu wana mziki wa kuwapa jeuri hiyo.

Msimu uliopita Yanga sio tu makundi ilikwenda hadi hatua ya robo fainali ikibakiza nukta chache kucheza nusu fainali ambapo msimu huu imesuka kikosi chao imara ikitaka kufika mbali ingawa malengo yao wanataka kuingia makundi.

Nahodha msaidizi wa Yanga ambaye ni beki wa kati wa kikosi hicho, Dickson Job ametoa tamko kwa niaba ya wenzake akisema baada ya mchezo wao wa kwanza wamefahamu wapi wamekosea na wameyafanyia kazi lakini zaidi wamesikia kilio cha mashabiki wao, leo watakwenda kurekebisha.

Job alisema kuwa kila mchezaji anaitaka mechi hiyo bila kukamia lakini wanataka kupeleka ujumbe kwa mashabiki wao kwamba wao pia wanautaka ushindi mkubwa ambao watautengeneza.

“Kila mmoja aliumia kuona hatukushinda kwa mabao ya kutosha kule Ethiopia, lakini kwenye soka inatokea nyakati kama hizi, hatuwezi kuendelea kulaumiana, tumekaa chini na makocha tukarudi mazoezini na kufanyia kazi yale ambayo yalitokea kule ugenini na sasa tuko tayari,” alisema Job na kuongeza.

“Mashabiki wetu tunawaambia tumewasikia, tunajua wana imani kubwa na sisi lakini tunawaomba waje tutawapa wanachokitaka ili tufuzu kwa pamoja kwenda makundi.”

Wakati Job akiyasema hayo, kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ameongeza kuwa wamejipanga sawasawa kuhakikisha wapinzani wao hawapati nafasi ya kuharibu hesabu zao za kufuzu.

“Kila kitu kwenye soka kinawezekana, kama mliangalia vizuri mechi ya kwanza mtaona hii sio timu rahisi kivile ina ubora wake, tunaiheshimu lakini tulichofanya ni kujiandaa sawasawa ili isitokee nafasi ya kuharibu hesabu zetu, tunahitaji kushinda nyumbani tena kushinda vizuri kwa kutumia nafasi kwa wingi tulizotengeneza,” alisema Gamondi ambaye mapema juzi asubuhi alishatua na jeshi lake Unguja.


CBE

CBE ipo Unguja mapema tena kabla ya wenyeji wao kufika, ikitua Jumatano tayari kwa mchezo huo lakini ikashuka na tahadhari kubwa huku hesabu zao kubwa zikiwa kwenye mioyo yao.

Kocha wao Sisay Kumbe ameliambia Mwanaspoti kuwa hawataki kukata tamaa mapema licha ya kupokea matokeo sio mazuri kwenye mechi waliyocheza nyumbani.

Kumbe aliongeza kuwa wako tayari kwa mechi ya marudiano, wameshaifahamu Yanga na kwamba watatumia makosa yao kujaribu kupindua meza kwa kushinda ugenini.

“Mchezo wa soka unatupa imani kwamba lolote linaweza kutokea, tunajua tuko hapa kupambana na timu bora yenye wachezaji wazoefu lakini hakuna timu isiyofanya makosa, tutaamua makosa yao kujaribu kufanya kitu tofauti,” alisema Kumbe.

“Hapo kabla kuna mambo tuliyajua lakini tulipokutana nao kuna vitu tumevijua zaidi, haitakuwa mechi rahisi hasa ukizingatia hii ni timu yenye mashabiki wengi hapa, tutapambana nao tuone mwisho kitu gani kitatokea.”


YAPEWA MWAMUZI WAO

Mchezo huo utaamuliwa na mwamuzi Abdel Aziz Bouh kutoka Mauritania ambaye amewahi kuwa kwenye mechi tatu za Yanga akisaidiwa na raia wenzake Brahim H’Made, Mohamed Youssef na Diou Moussa.

Bouh aliyezaliwa miaka 32 iliyopita, alikuwa mwamuzi wa kati kwenye mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika Yanga ikishinda nyumbani kwa mabao 3-1 dhidi ya TP Mazembe Februari 19, 2023.

Mchezo wa pili ni ule ambao wa nyumbani tena ambao Yanga ilitoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly, iliyopigwa Desemba 2, 2023 lakini pia alikuwa mwamuzi wa nne mezani kwenye mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa ugenini, mabingwa hao wa Tanzania wakitoa suluhu dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na baadaye kwenda kutolewa kwa matuta 3-2 kule Kwa Madiba.


REKODI YANGA v WAHABESHI

Yanga dhidi ya timu za Ethiopia katika michuano ya CAF ina rekodi ya kuzitoa mara tatu kati ya nne walizokutana huku yenyewe ikitolewa mara mmoja hatua ya mtoano. Yanga mbali ya kuzitoa timu hizo, pia inajivunia rekodi ya kufunga mabao mengi winapocheza na Wahabeshi hao.

Yanga ilikutana kwa mara ya kwanza na klabu ya Ethiopia 1969 katika Klabu Bingwa Afrika ikaitoa Saint-George kwa mabao 5-0.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Ethiopia zilitoka suluhu na mechi ya marudiano Yanga ilishinda 5-0 na kusonga hadi robo fainali. Kisha Yanga ilikutana na Coffee FC 1998 na kuitoa kwa mabao 3-8 katika hatua ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Ethiopia Coffee FC ililazimisha sare 2-2 kisha mchezo wa marudiano Yanga ilishinda 6-1 nyumbani na kufuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa.

Katika Kombe la Shirikisho mwaka 2011, Yanga ilitolewa kwa jumla ya mabao 6-4, baada ya nyumbani na kulazimishwa sare 4-4 na Dedebit kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na marudiano Ethiopia wenyeji, Dedebit waliichapa Yanga 2-0.

Mwaka 2018, ilicheza dhidi ya Welaita Dicha katika Kombe la Shirikisho na kufuzu hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 2-1. Mchezo wa kwanza nyumbani Yanga ilishinda 2-0, ilipoenda ugenini ikalala 1-0.

Baada ya mechi ya kwanza Septemba 14, 2024 Yanga kuvunja mwiko wa kutoshinda katika ardhi ya Ethiopia kwa kuichapa CBE 1-0 katika mechi ya kwanza ya mchujo wa kutinga hatua ya makundi huku ikipoteza nafasi nyingi za kufunga, leo itakuwaje? Itaendeleza rekodi ya vipigo vya mbwakoko kwa timu za Ethiopia au kitumbua cha Wananchi kitatiwa mchanga?


TAHADHARI

Yanga inatakiwa kuwa makini na CBE ambayo licha ya kuwa timu changa kwenye historia ya mashindano ya Afrika, tayari imeshtua msimu huu ilipoichapa SC Villa ya Uganda kwa mabao 2-1 ugenini kisha iliporudi kwao ikatoa sare ya 1-1 na kutinga hatua hii ilipokutana na mabingwa hao wa soka wa Tanzania.

Ushindi wa ugenini dhidi ya SC Villa na kuivimbia Yanga ipate ushindi mwembamba wa bao 1-0 tu wakati timu hiyo ya Wananchi imetokea kuing’oa Vital’O ya Burundi kwa jumla ya mabao 10-0, sio jambo la kulichukulia poa hata kidogo.

Kitu ambacho kinafahamika ni kwamba CBE hawana cha kupoteza tena kwa vile walishafungwa kule kwao, hivyo kwenye Uwanja wa Amaan leo watafunga busta. Ile staili yao ya kutawala mechi wataiongeza mara dufu, zaidi ya ilivyokuwa kule Ethiopia na watalitafuta bao kwa nguvu zote.

Yanga haitaachwa icheze kwa amani. Licha ya kwamba kufunguka zaidi kunaweza kuwa na madhara makubwa wa CBE ambao huenda wakajikuta wanakula mvua wa mabao, lakini kuiandama Yanga kunaweza kuwalipa pia kama timu hiyo ya kitajiri itaweza kucheza kama ilivyocheza ugenini dhidi ya SC Villa.

Na kama itaweza kuishangaza Yanga kwa kupata mabao kama yale 2-1 iliyoshinda ugenini dhidi ya SC Villa, hiyo inamaanisha timu ya Wananchi itaaga mashindano. Na hata ikifunga bao 1-0 na kulazimisha mechi kuamuliwa kwa kupigiana ‘matuta’, timu hiyo ya benki ya biashara itaitingisha nchi.

Na kama itaweza kuing’oa Yanga katika hatua hii ya kwanza, hakika mashabiki hawatawasamehe viongozi wao kwa kuipeleka mechi kwenye uwanja wa ‘ugenini’ na kuuacha uwanja wao ambao wamekuwa wakiutumia zaidi kama wa nyumbani wa Benjamin Mkapa ambako timu hiyo imekuwa ikicheza vyema zaidi huku ikipata sapoti ya mashabiki wake 60,000.