Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ELFADHILY: soka lina mengi, Wachezaji mtubu

Muktasari:

  • Nyota huyo ambaye amedumu na kikosi hicho kwa miaka 15 anasema muda wa kustaafu umefika na kuwapisha vijana kuonyesha uwezo wake, huku akifunguka atakachokwenda kufanya wakati akifanyiwa mahojiano na Mwanaspoti

NAHODHA wa Tanzania Prisons, Jumanne Elfadhily ametangaza nia ya kustaafu soka, lakini kabla hajafanya hivyo ameamua kuwapa neno wachezaji wenzake kutokana na yale wanayofanya ndani na nje ya uwanja. Unajua amewaambia nini? ‘Watubu’ kwani kuna mambo mengi wanayafanya na watenge muda wa kuongea na Mungu ili awasamehe.

Nyota huyo ambaye amedumu na kikosi hicho kwa miaka 15 anasema muda wa kustaafu umefika na kuwapisha vijana kuonyesha uwezo wake, huku akifunguka atakachokwenda kufanya wakati akifanyiwa mahojiano na Mwanaspoti


KWA NINI WATUBU?

Elfadhily anasema soka lina mambo mengi ndani na nje ya uwanja hivyo wachezaji wanapaswa kutenga muda kuzungumza na Mungu kwa kutoa sadaka kwa wahitaji na kwenda maeneo ya ibada. Anasema katika miaka 15 aliyotumikia soka la kulipwa nchini, ameona mambo mengi yanayofanywa na wachezaji yakiwamo ya makusudi na yasiyo ya kukusudiwa.

“Binafsi huwa nafanya hivyo, japokuwa sipendi kutangaza, natoa sadaka kwa wahitaji, najifungia kusali kumwomba na kumshukuru Mungu kwa kuwa sisi binadamu tunakosea sana, muda mwingine bila kukusudia,” anasema huku akikumbuka tukio alilowahi kumfanyia kiungo wa Simba Mzamiru Yassin timu zao zilipokutana kuwa haikuwa makusudi kumchezea rafu na ilikuwa mahati mbaya.


MAISHA BAADA YA KUSTAAFU SOKA

Anasema akistaafu tu soka anatamani kuishi na familia yake kwani imekuwa mbali naye kwa sababu ya majukumu ya soka, hata hivyo anasema hatajihusisha tena na soka kwani ana mambo mengine ya kufanya kuendeleza kipato chake. “Natamani hata leo hii nistaafu soka kwa kuwa nimelitumikia sana. Nikikamilisha hili sitaki tena mambo ya soka nitatulia na familia kwa kuwa nimekuwa mbali nayo, nifanye shughuli nyingine kama biashara na kilimo,” anasema nyota huyo.

WAAMUZI WAMSHANGAZA

Elfadhily anasema miongoni mwa changamoto zinazokatisha tamaa ni baadhi ya waamuzi ambao huingia uwanjani kuamua soka wanavyotaka huku wengine wakiwa na matokeo  kabla ya mchezo jambo ambalo lilimshangaza na kuona soka linaharibiwa.

Anasema kuna mechi tatu tofauti za Ligi Kuu Bara waamuzi akiwamo mmoja ambaye kwa sasa mestaafu kabla ya mechi waliwaambia hawatashinda. Hata hivyo, kutokana na kutokana na soka lilivyo walikubaliana na kauli zao na kweli hawakushinda michezo hiyo.

“Wapo waamuzi watatu walituambia hizi mechi hamshindi na kweli tulipoteza, mmoja wa marefa hao amestaafu wengine wapo na tunakutana nao kwenye mechi mara nyingi. Hata hivyo kuna ambazo tunashinda ila kwa hizo inaonyesha wazi kuna shinikizo.”

APATA VITISHO

Nahodha huyo anasema amekuwa mmoja wa waaathirika wa vitisho hasa wanapocheza na timu kubwa na kuwapa ushindani na amekuwa akipigiwa simu, kushambuliwa kwenye akaunti zake za mitandaoni na wakati mwingine mitaani. “Wengine wanapiga simu, mitaani na mitandaoni. Hatua ninazochukua ni kuripoti kwa uongozi wangu. Hii hutokea sana hasa tunapozipa ushindani timu kubwa.”


HAKUPANGA KUCHEZA SOKA

Anasema licha ya kipaji kumbeba, lakini ndoto zake hazikuwa kucheza soka bali kufanya biashara na hata mama awali hakupenda acheze ila kutokana na uwezo wake, alipata hadi zawadi ya Sh50,000 alipocheza mechi ya kirafiki na alimpatia mama zikamtuliza na kumruhusu aendelee.

“Tangu zamani hadi nasajiliwa Prisons nilikuwa nacheza nafasi ya kipa na pesa ya kwanza Sh50,000 niliipata huko nikampelekea mama, japo hakutaka nicheze soka, ndiyo baadaye akaanza kuruhusu nicheze.

“Hata mimi ndoto yangu haikuwa kucheza soka, nilifikiria biashara ambayo hata sasa hivi nafanya, ila kwa kuwa kipaji kilinibeba, nikaamua kuendelea na kazi hii,” anasema beki huyo na kuongeza katika mafanikio kwa muda aliofanya kazi hiyo pamoja na maisha binafsi ya kuendesha familia, lakini ajira Jeshi la Magereza ni faida kubwa kwake.

MATOKEO, MIGOGORO

Kuhusu ishu ya matokeo, Mjeda huyo anasema kwa misimu mitatu nyuma hawakuwa na mwenendo mzuri na anachojua ni michezo iliwakataa na hakuna kingine kama wengi wanavyodai.

“Wakati mwingine ni makosa ya wachezaji wenyewe. Tulipata mabadiliko ya uongozi na benchi la ufundi ya mara kwa mara. Hata hivyo, wachezaji hatukuwa na mgogoro kama ilivyoelezwa kulikuwa na makundi ya askari na wale raia ila ni matokeo yalitukataa.

“Hakuna timu inayoishi vyema na wachezaji kama Tanzania Prisons, haijalishi ni askari au raia. Ndiyo maana wengine huondoka na kurudi. Hii ni kutokana na ushirikiano mzuri tulionao,” anasema.


UKIMYA NI ASILI YAKE

Baadhi ya wadau na mashabiki wamekuwa wakishangazwa na tabia ya nyota huyo kutohangilia pale anapofunga bao au timu inaposhinda. Mwenyewe anafafanua kwamba hiyo ni asili yake tangu akiwa mdogo kwani alikuwa mpole na hakupenda kuchangamana na wenzake hadi mama’ke akawa anamlazimisha acheze na wenzake.

Kuhusu kutoshangilia bao au timu inaposhinda ni kutokana na kumfikiria kipa anayefungwa anajisikiaje kwa kuwa hata Prisons ikipoteza mechi huwa anaumia sana.

“Kwanza huwa namfikiria kipa niliyemfunga anajisikiaje, ndiyo maana sishangilii na muda mwingine nalazimisha tu kwa kuwa tumeshinda, tangu nikiwa mdogo mimi niko hivyo, sikuwa nachangamana na watu na nilipenda kutulia peke yangu.”


NIDHAMU YAMBEBA UNAHODHA

Kuhusu kitambaa cha unahodha muda wote, anasema sababu kubwa ni nidhamu, kujituma na kushirikiana na wenzake ndani na nje ya uwanja na kumthamini kila anayekutana naye.

“Sijawahi kugombana na kiongozi wala mchezaji. Ikitokea tuko uwanjani kupishana kauli huwa ni katika kuipigania timu, nidhamu na heshima ya nje na ndani ya uwanja ndiyo siri kubwa ya kudumu kama nahodha.”