Halaand na Drogba tafsiri ya wengine hutoboa mapema, wengine huchelewa
Muktasari:
- Kuelekea mchezo huo, macho na masikio ya watu yalielekezwa kwa Jamie Vardy, mshambualji wa Leicester City aliyekuwa akifukuzia rekodi ya ligi ya kufunga mechi nyingi mfululizo.
NOVEMBA 28, 2015, Manchester United waliikaribisha Leicester City katika mwendelezo wa Ligi Kuu England msimu wa 2015/16, ule ambao Leicester City ya maajabu iliwashangaza wengi kwa kutwaa ubingwa.
Kuelekea mchezo huo, macho na masikio ya watu yalielekezwa kwa Jamie Vardy, mshambualji wa Leicester City aliyekuwa akifukuzia rekodi ya ligi ya kufunga mechi nyingi mfululizo.
Awali, rekodi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na nyota wa zamani wa Manchester United, Ruud van Nistelrooy aliyekuwa amefunga katika mechi 10 mfululizo na Vardy alishaifikia. Wakati timu zinaingia uwanjani, Steve Wilson, mtangazaji wa kandanda wa BBC Sports aliyetangaza mechi hiyo alisema “when Wayne was 17 he was becoming England’s youngest ever scorer, when Jamie Vardy was 17 he was playing for Wickersley and dreaming for a big move to Stockbridge Park Steels...some make it early some make it late.”
Akimaanisha, “wakati Wayne Rooney alipokuwa na miaka 17, akawa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuifungia bao England. Wakati Jamie Vardy alipokuwa na miaka 17 alikuwa akiichezea Wickersley akiota kupata uhamisho mkubwa kwenda Stockbridge Park Steels...wengine hutoboa mapema wengine huchelewa.”
Vardy aliingia kwenye mchezo huo akizungumzwa zaidi kuliko hata Wayne Rooney, nyota na nahodha wa Manchester United. Mtangazaji akatumia historia zao kufikisha ujumbe wa kutokata tamaa maishani.
WAYNE ROONEY
Akitokea akademi ya Everton, Rooney aligonga vichwa vya habari akiwa na miaka 16 baada ya kuifunga Arsenal 2002 kwenye Ligi Kuu England. Arsenal ilikuwa imecheza mechi 30 bila kupoteza hadi ilipokutana na kitu kizito kutoka kwa Rooney. Mwaka 2003, akiwa na miaka 17, Rooney akaifungia bao timu ya taifa ya England na kumfanya kuwa mfungaji mwenye umri mdogo zaidi.
JAMIE VARDY
Alianzia soka kwenye akademi ya Sheffield Wednesday lakini akiwa na miaka 16 akatemwa. Akajiunga na akademi ya Wickersley na akiwa na miaka 17, mwaka 2007 akajiunga na klabu ya Stocksbridge Park Steels iliyokuwa Daraja la Nane...mchangani (non league)! Alicheza mchangani hadi 2012 alipojiunga na Leicester City iliyokuwa Daraja la Kwanza, na 2014 akacheza Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza.
WAKAKUTANA
Licha ya Rooney kutoboa mapema na Vardy kuchelewa, lakini walikutana kwenye mechi hiyo, huku Vardy akizungumzwa zaidi ya Rooney, na katika mchezo huo Vardy akafunga bao na kuweka rekodi ambayo inadumu hadi sasa.
Rooney alitoboa mapema na kucheza Ligi Kuu akiwa na miaka 16. Vardy alichelewa na akacheza akiwa na miaka 28. Rooney alitoboa mapema na kuichezea timu ya taifa kwa mara ya kwanza akiwa na miaka 17 tu, Vardy alichelewa na akaichezea timu ya taifa kwa mara ya kwanza akiwa na miaka 29. Huu ni sawa na mkasa wa urais wa Marekani. Barack Obama alistaafu urais akiwa na miaka 55, Donald Trump alianza urais akiwa na miaka 70, na Joe Biden akachukua kijiti akiwa na miaka 78.
DROGBA, HAALAND
Nimeanzia mbali kote huko ili nikujengee picha ya rekodi za Didier Drogba na Erling Halaand kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Wiki iliyopita Erling Haaland wa Manchester City alifikisha mabao 44 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya kufunga mawili dhidi ya Sparta Praha ya Jamhuri ya Czech.
Mabao hayo yanamfanya raia huyo wa Norway amfikie nyota wa Ivory Coast, Didier Drogba, mwenye mabao 44 pia. Haaland amefikia idadi hiyo ya mabao akiwa na miaka 24 tu wakati Didier Drogba alipokuwa umri huo alikuwa hajacheza hata mechi moja ya Ligi ya Mabingwa.
DIDIER DROGBA
Licha ya kukulia Ufaransa tangu akiwa na miaka mitano, lakini Drogba ni mmoja wa wachezaji ambao hawakupata bahati ya kupitia akademi kuendeleza vipaji. Ukiacha kucheza barabarani kama ilivyo kawaida watoto wengine duniani kote, Drogba alianza kucheza mpira akiwa na miaka 15 baada ya kujiunga na timu ya mtaani kwao. Akawa anabadili timu tu za uswahili hadi alipofikisha miaka 18 pale alipojiunga na timu ya Levallois ambako alishindwa kung’ara. Wakati wote huo Drogba alikuwa akicheza mpira huku akisoma shule na baada ya kumaliza akaenda kusomea uhasibu katika Chuo Kikuu cha Le Mans. Katika mji huo kulikuwa na timu ya daraja la pili ya Le Mans, ambayo alijiunga nayo huku akiendelea na masomo yake ya uhasimu.
Masomo hayo yakamfanya akose muda wa kutosha kuhudhuria mazoezi kiasi kwamba ilimchukua miaka minne kuanza kuhudhuria mazoezi ya kila siku na kuanza kucheza mpira kila wiki. Drogba alisaini mkataba wake wa kwanza na Le Mans 1999 na kuwa mwanasoka wa kulipwa akiwa na miaka 21. Na hii ni baada ya kupata mtoto wake wa kwanza, Isaac ambaye analingana umri na Erling Haaland.
Mtoto huyu aliyezaliwa mwaka 2000 baada ya Drogba kumaliza masomo ya uhasibu ndiye aliyemfanya atie juhudi kwenye mpira ili kuweza kuihudumia familia yake. Juhudi zake zikalipa kwani kwenye dirisha dogo la 2001/02 akasainiwa na timu ya Ligi Kuu Ufaransa ya Guingamp, iliyokuwa inapigania kukwepa kushuka daraja. Hakufanya vizuri katika siku zake za kwanza ambapo alimaliza nusu ya msimu iliyobaki kwa kufunga mabao matatu, japo timu hiyo ilinusurika kushuka. Lakini ulipoanza msimu mpya wa 2002/03, Drogba alikuja kivingine ambapo alimaliza na mabao 17 na kuisaidia timu kumaliza ligi katika nafasi ya saba, ambayo ilikuwa rekodi ya klabu. Stori ya Drogba ikaanza kubadilika kwani mabao yakaivutia Marseille ikamnasa kwa ajili ya msimu wa 2003/04. Akiwa na Marseille, Drogba akaanza kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na miaka 25. Ilikuwa Septemba 16, 2003 dhidi ya Real Madrid. Japo walifungwa 4-2, lakini yeye ndiye alikuwa wa kwanza kufunga. Bao lake la mwisho alilifunga Novemba 25, 2015 dhidi ya Schalke 04 ya Ujerumani katika ushindi wa ugenini wa 5-0.
ERLING HAALAND
Mtoto wa nyota wa zamani wa Manchester City, Aalf Inge Haaland, Erling Haaland alizaliwa kwenye soka na kukulia kwenye soka. Wakati anazaliwa 2000, baba yake alikuwa akiichezea Leeds United ambayo ilikuwa moto wakati huo. Akiwa na miaka mitano alijiunga na akademi ya klabu ya Bryne ya kwao Norway, mji aliozaliwa na kukulia baba yake. Alipofikisha miaka 15 akapandishwa timu ya wakubwa iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Nne. Katika umri wa miaka 15, Drogba ndiyo alikuwa anaanza kucheza. Akiwa na miaka 16, Haaland akasajiliwa na timu ya Ligi Kuu Norway, ya Molde, iliyokuwa ikifundishwa na Ole Gunnar Solskjaar. Akiwa na miaka 17, Haaland akasajiliwa na RB Salzburg ya Austria. Katika umri huo, akacheza mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kufunga bao dhidi ya KRC Genk ya Ubelgiji ya kina Mbwana Samatta.
Katika umri huo, Drogba alikuwa bado anasomea uhasibu hata mpira wenyewe hajaanza rasmi. Wengine hutoboa mapema, wengine huchelewa kutoboa!