Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jeuri ya Chama kimfumo Yanga

CHAMA Pict
CHAMA Pict

Muktasari:

  • Chama aliyejiunga na Simba mara ya kwanza Julai 1, 2018 akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia amekuwa mmoja wa viungo bora nchini na kitendo cha kujiunga na Yanga kimekuwa na manufaa kwa benchi la ufundi katika matumizi dhidi yake.

MOJAWAPO wa usajili uliogonga vichwa vya habari katika msimu huu ulikuwa ni wa aliyekuwa kiungo wa Simba, Mzambia Clatous Chama kuihama timu hiyo aliyoichezea kwa misimu sita na kutua kwa watani wao wa jadi, Yanga.

Chama aliyejiunga na Simba mara ya kwanza Julai 1, 2018 akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia amekuwa mmoja wa viungo bora nchini na kitendo cha kujiunga na Yanga kimekuwa na manufaa kwa benchi la ufundi katika matumizi dhidi yake.

Mwanaspoti linakuletea jinsi nyota huyo anavyolipa jeuri benchi hilo katika harakati za kuusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu na mashindano mengine inayoshiriki ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho la FA.


CH01
CH01

MIFUMO TOFAUTI

Msimu uliopita Yanga ilipitia changamoto kubwa hasa baada ya kuumia kwa kiungo Pacome Zouzoua, jambo lililosababisha kuyumba kwa baadhi ya michezo hasa ule wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Uwepo wa Chama, Stephane Aziz Ki, Pacome na Maxi Nzengeli unalipa wigo mpana benchi la ufundi juu machaguo tofauti ambapo linaweza kutumia mfumo wa 4-3-3 ili kuendana na wachezaji hao na kutengeneza uwiano mzuri wa kushambulia na kuzuia.

Katika mfumo huo, Prince Dube ambaye hajaanza vizuri tangu asajiliwe msimu huu akitokea Azam FC, anaweza kusimama mshambuliaji wa kati akishirikiana na Pacome, Nzengeli, Clement Mzize ama Mudathir Yahya. Benchi la ufundi linaweza kumtumia Mzize, Dube au Kennedy Musonda katika eneo la ushambuliaji, huku Khalid Aucho akisimama kiungo pekee mwenye jukumu la kukaba wakati kushoto akicheza Chama na kulia Aziz KI kwa mfumo huo na kuleta matokeo chanya.

Nyota hao watakuwa huru kuchezesha timu, jambo litakaloifanya Yanga kutengeneza safu bora ya wachezeshaji kutokana na rekodi za wachezaji hao kwani wote wamekuwa wazuri katika kufunga na kutoa asisti kwa sababu ya ubora walionao.

Mfumo mwingine ni wa 4-4-2 ambao unatoa viungo wanne na ikiwa kocha atataka kuanza na wawili wenye uwezo wa kukaba, basi anaweza kuwatumia Khalid Aucho na Mudathir Yahya, huku Chama na Aziz Ki wakipeleka mashambulizi kupitia pembeni.

Ikiwa kocha atataka kuanza na kiungo mmoja mwenye sifa nzuri za kuzuia zaidi, basi Aucho au Mudathir mmoja atasubiri benchi hivyo kutoa nafasi kwa Pacome au Nzengeli kuungana na Chama na Aziz KI kwa ajili ya kunogesha katika eneo hilo.

Kocha Miguel Gamondi alitumia mfumo huo dhidi ya Mamelodi Sundowns katika Ligi ya Mabingwa Afrika akiwatumia washambuliaji wawili kiasili ambapo Mzize na Joseph Guede walianza ingawa walikuwa na majukumu tofauti uwanjani.

CH02
CH02

Jeuri nyingine ambayo kocha anaipata ni katika mfumo wa 4-2-3-1 ambao unatoa nafasi kwa mabeki wanne, viungo wawili wa ukabaji na watatu wanaoshambulia huku mshambuliaji wa kati akiwa mmoja ambaye anaweza kusimama Jean Baleke, Mzize, Musonda au Dube.

Katika safu ya viungo washambuliaji wanaweza kucheza Chama, Aziz KI na Pacome au Nzengeli huku uwepo wa mshambuliaji wa kati ukimfanya Mudathir kushirikiana na Aucho ilhali Jonas Mkude na Salum Abubakar ‘Sureboy’ wakipambania kupenya.

Mfumo mwingine ambao kocha anaweza kuutumia ni wa 3-5-2 ambapo anaweza kuwatumia mabeki watatu Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na viungo watano ambao kazi yao kubwa itakuwa kusaidia timu pindi inaposhambuliwa.

Yanga inaweza kucheza hivyo ikimkosa beki wa kulia, Yao Kouassi huku ikitoa nafasi kwa Nzengeli kutokea upande wa kulia kati ya viungo watano, mfumo ambao tunaweza kumuona Chama, Aziz KI, Pacome, Aucho na Mkongomani huyo wakicheza pamoja.

Katika mfumo huo pia wa 3-5-2, washambuliaji wanaweza kusimama ni Dube na Mzize, Musonda au Baleke.


CH03
CH03

REKODI ZINAMBEBA

Yanga haijakosea kumsajili Chama kwani rekodi zake zinambeba hata kabla ya kutua katika kikosi hicho cha Jangwani ambapo akiwa na Simba aliyoitumikia kwenye michezo 179, ya mashindano yote alifunga mabao 42, na kuasisti 60.

Rekodi zake tamu kwa nyota huyo ni za msimu wa 2022/2023 alipohusika katika mabao 18, akifunga manne na kuasisti 14 na ile ya msimu wa 2020/2021, alipokuwa wa moto zaidi kufuatia kuhusika na mabao 23, akifunga manane na kutoa asisti 15.

Misimu ambayo namba za Chama katika Ligi Kuu Bara zilikuwa chini ni za msimu wa 2021/2022, aliporejea Simba akitokea RS Berkane ya Morocco, ambapo alifunga mabao matatu pekee huku msimu wa 2019/2020, akifunga mabao mawili na kuchangia 10.

Katika msimu wake wa kwanza akiwa na kikosi hicho cha Msimbazi 2018/2019, alihusika katika mabao 16, ya Ligi Kuu Bara ambapo alifunga saba na kuasisti tisa, huku akiipeleka timu hiyo robo fainali ya michuano ya CAF mara tano.

Michezo ya kimataifa imempa sifa na umaarufu mkubwa kutokana na kuibeba kwa asilimia kubwa timu hiyo mabegani mwake hasa katika hali ambayo mashabiki wamekata tamaa, huku akiwa amefunga mabao 15 na kuchangia sita kwenye mechi 44, za hatua ya makundi.

Ukiachana na rekodi hiyo akiwa na Simba hata alipojiunga na Yanga aliendeleza moto uleule kwani katika mechi za awali za kufuzu hatua ya makundi za timu hiyo, nyota huyo alihusika kwenye mabao manane kati ya 17, yaliyofungwa na kikosi hicho.

Yanga ilianzia hatua za awali kwenye michuano hiyo ikicheza mechi nne na kati ya hizo imefunga mabao 17 ikianza kuichapa Vital’O ya Burundi mabao 4-0 ugenini, 6-0 nyumbani, pia ikiichapa CBE SA ya Ethiopia ugenini bao 1-0, ilhali nyumbani 6-0.

Katika mabao hayo 17, Chama alifunga matatu na kuasisti mara tano na kukiwezesha kikosi hicho cha Kocha, Gamondi kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara yake ya pili mfululizo baada ya msimu uliopita kuishia robo fainali.

Kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, nyota huyo amehusika na mabao mawili ya kikosi hicho akifunga moja na kuasisti moja.


MSIKIE GAMONDI

Kocha Gamondi aliwahi kukaririwa akieleza kuwa uwepo wa Chama umemuongezea balansi ya timu eneo la kiungo mshambuliaji, kwa sababu mbali na kusaidia hupeleka mashambulizi na pia ana uwezo mkubwa wa kufunga. “Mchezaji mzuri huwa anajieleza mwenyewe kutokana na kile alichokifanya au anachoendelea kukifanya, Chama ni mmoja wa wachezaji bora na kocha yoyote angetamani uwepo wake kwenye timu, ameongeza ubora wa kikosi chetu,” alikaririwa Gamondi.