Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

LYANGA: Straika anayetembelea nyota ya CR7

Muktasari:

  • Nyota huyo aliyewahi kuzichezea timu mbalimbali nchini zikiwemo Arusha FC, Coastal Union, Geita Gold na Azam FC amefunguka mengi akieleza mipango mipya msimu huu wakati akiwa na kikosi cha JKT Tanzania. Tiririka naye.

UNAPOTAJA miongoni mwa washambuliaji wenye vipaji nchini hutaacha kulitaja jina la mshambuliaji wa JKT Tanzania, Daniel Lyanga kutokana na uhodari wake kucheza soka ndani na nje ya nchi.

Nyota huyo aliyewahi kuzichezea timu mbalimbali nchini zikiwemo Arusha FC, Coastal Union, Geita Gold na Azam FC amefunguka mengi akieleza mipango mipya msimu huu wakati akiwa na kikosi cha JKT Tanzania. Tiririka naye.


HAPENDI MAKUU

Moja ya jambo kubwa linalomchukiza nyota huyo ni kutopenda kuonyesha makuu mbele ya watu kwa sababu anaamini ili uishi vyema na watu mbalimbali waliokuzunguka ni lazima uwe katika uhalisia wako, kwani hilo husaidia katika maisha.

“Naweza nikapanda daladala na nikajiona freshi tu kwa sababu naona ni kawaida tofauti na wengine wanaojikweza kisa tu wamefanikiwa. Nimeishi maisha ya chini na naelewa namna bora ya kukaa na watu ndiyo maana sipendi kabisa kujikweza,” anasema.


MAISHA YA JKT TZ

Licha ya nyota huyo kuzitumikia klabu mbalimbali za ndani na nje ya nchi kwa nyakati tofauti, lakini anadai anafurahia maisha yake akiwa na kikosi hicho cha maafande, akiweka wazi hajutii kukichezea ingawa alikuwa na ofa nyingine.

“Ukiachilia mbali wengi wetu kujuana hapa, ila tunaishi kama familia. Kiukweli ni maisha fulani hivi ambayo yanavutia na kutia moyo. Ukiwa na shida yoyote mtu yupo tayari kukusaidia, ni jambo zuri ambalo najivunia.”

Lyanga anayezaliwa tumbo moja na nyota wa Singida Black Stars, Ayoub Lyanga huku akiwa yeye ndiye kaka, anasema licha ya kuchezea timu mbalimbali za kiraia na za kijeshi, ila haoni tofauti kubwa japo zinatofautiana kwenye maeneo machache.

“Maisha ni sehemu yoyote tu ilimradi upate kile ambacho unakitafuta, jeshini ni kweli kuna muda unaweza ukawa na hofu  lakini ukitambua kilichokupeleka na unachokipambania utaendana na mazingira halisi na baada ya muda utaona ni kawaida.”


PRESHA YA MASHABIKI

Lyanga anasema mashabiki wana nafasi kubwa kwa mchezaji ingawa ni ngumu unapocheza timu kubwa zenye presha ya matokeo chanya. “Mashabiki wanaweza wakakufanya ukazidi kupambana au ukatoka mchezoni kwa sababu siku zote huwa wao wanapenda tu furaha, kuna muda unaweza ukafanya kosa la kimchezo ila wakaona makusudi, japo napambana kukabiliana na hali ya namna yoyote.”


KUJIANDAA KISAIKOLOJIA

Anasema, moja ya jambo kubwa analofanya na kulipa kipaumbele zaidi kabla ya mchezo wowote ule ni kujiandaa kisaikolojia kwa sababu anaamini itamsaidia kukabiliana na mazingira ya aina yoyote yanayoweza kumtoa katika mstari kwa siku husika.

“Nikijua kama leo tuna mchezo wowote ni lazima nijipange vizuri kwa maana ya kujiandaa kisaikolojia kukabiliana na jambo lolote litakalotokea liwe baya au jema, hii inanisaidia kunipunguzia presha kwa sababu nakuwa nimeshajipanga mapema.”


ATOROKA UARABUNI

Lyanga anasema jambo la kusisimua ambalo hatalisahau ni kutoroka akiwa Falme za Kiarabu wakati huo akikichezea kikosi cha Fanja SC msimu wa 2017/2018, alichojiunga nacho msimu huo baada ya kuachana na Simba.

“Nakumbuka wakati niko Oman jamaa kuna kiasi cha fedha tulichokubaliana watanilipa kuanzia kwenye usajili hadi mshahara, ila baada ya kwenda kule mambo yakawa ni tofauti, baada ya kuona hivyo, iliniumiza sana kiukweli,” anasema na kuongeza:

“Baada ya muda sio mrefu nikapata nafasi ya kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ na niliporejea nchini sikutaka tena kurudi na ikawa mwisho wangu na Fanja SC, kwani nilisaini Singida United ambayo ilinipa maslahi mazuri.”

Nyota huyo anasema, sio kweli wachezaji wengi wa Tanzania wanafeli nje ya nchi kwa sababu ya kutokuwa na uwezo isipokuwa kuna mambo mengi yanatokea, ila kutokana na kutofahamu yale yaliyokuwa nyuma basi wadau huzungumza vile wanavyojisikia.


ISHU YA UBAGUZI

Lyanga ambaye amewahi kuichezea pia DC Motema Pembe ya DR Congo anasema, hajawahi kukutana na suala lolote la ubaguzi wa rangi.

“Sijawahi kukutana na hali hiyo, siwezi kusema haipo kwa sababu baadhi ya Watanzania wenzetu waliopata nafasi ya kucheza nje kama mimi walishazungumzia sakata hilo, kikubwa ni kupambana na kutimiza malengo yaliyokupeleka na sio vinginevyo.”


MSIMU BORA

Anasema moja ya msimu wake bora ni wa 2020-2021 akiwa na kikosi cha JKT Tanzania ambacho anakichezea kwa sasa kwa sababu alifunga idadi ya mabao 10, katika Ligi Kuu Bara, ikiwa ni mengi zaidi kwake kufunga kwani hajawahi kufikisha kama hayo.

“Nilikuwa sijawahi kufikisha idadi hiyo hivyo kwangu ulikuwa ni msimu bora sana, ningeweza kufunga zaidi ya hayo ingawa nakumbuka nilikosa penalti mbili hivi ambazo zingenifanya kufikisha 12, japo nashuruku kwa yote,” anasema na kuongeza:

“Msimu huu natamani kufikisha zaidi ya mabao 10 na ninaamini nina uwezo wa kuyafikia, kila jambo namuomba mwenyezi Mungu kwa sababu yeye ndiye muweza wa yote, ushirikiano uliopo hapa na wachezaji wenzangu naamini nitayafikia malengo hayo.”

Katika msimu huo, aliyekuwa nahodha wa Simba, John Bocco ambaye kwa sasa anaichezea JKT Tanzania aliibuka mfungaji bora baada ya kufunga mabao 16 akifuatiwa na Chris Mugalu aliyekichezea pia kikosi cha Msimbazi na kufunga jumla ya mabao 15.


BOCCO NI MLEZI

Lyanga anasema, moja ya jambo kubwa analojivunia katika maisha yake ni kucheza na aliyekuwa nahodha wa Simba, John Bocco kwa sababu mbali tu na uchezaji wa nyota huyo ila ni mlezi, kiongozi na mtu mwerevu anayeweza kuishi na kila mmoja wao.

“Bocco ni mchezaji ila kwangu namuangalia kama kiongozi. Jamaa amebarikiwa sana kujua namna ya kuishi na kila mmoja, sio mtu anayependa kujikweza, ukikosea anakuelekeza kwa upendo, yaani hapa tulipo naye najivunia sana uwepo wake,” anasema.


NYAYO ZA CR7

Anasema, moja ya mchezaji mkubwa anayemuangalia na kupenda kile anachokifanya ni nyota wa zamani wa timu za Manchester United, Real Madrid na Juventus, Cristiano Ronaldo ‘CR7’ ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya Al-Nassr ya Saudi Arabia.

“Ronaldo ni moja ya wachezaji ninaowakubali sana kwa sababu anajituma uwanjani, kwangu namuangalia kama mtu muhimu na anayenivutia, kwa hapa kwetu Tanzania siwezi kuweka wazi namkubali mchezaji gani tofauti na mimi mwenyewe,” anasema.


MAISHA BAADA YA SOKA

Lyanga anasema, kwa sasa ni ngumu kuweka wazi mipango yake ya baadae baada ya kuachana na soka ingawa anajiona bado ana muda wa kucheza.

“Kuna vitu vingi navifanya ila nisingependa kuviweka wazi, kwa sasa nimejikita kucheza soka na ikitokea nikistaafu ndipo ninaweza kuzungumzia maisha yangu mengine nje ya hayo, napenda hivyo kwa sababu nimetokea familia ya soka,” anasema Lyanga na kuongeza:

“Baba yangu mzee, Reuben Lyanga alikuwa mchezaji kipindi cha nyuma huko mkoani Moshi ndio maana imekuwa rahisi kwangu na mdogo wangu, Ayoub Lyanga kufuata nyayo zake, najivunia hilo kwani wametusapoti kwa kiasi kikubwa hadi hapa tulipo leo.”


CHANGAMOTO NI FURSA

Nyota huyo anasema, changamoto kwake anazichukulia kama fursa ya kujifunza na kupata elimu zaidi kwani zinazidi kumkuza kiakili.

“Kuna muda unakuwa na siku mbaya kazini lakini ikitokea hivyo kwangu naichukulia kawaida na naangalia mbele, huwezi siku zote ukafanya vizuri na kumridhisha kila mtu, kikubwa ni kuangalia ulipojikwaa na kujirekebisha ili kuwa bora zaidi.”