Maajabu ya mikono mia
Muktasari:
- Ferguson alikuwa akiamini kwamba kama utakuwa na mabeki bora na washambuliaji bora basi kuna uwezekano mkubwa wa kushinda mataji kuliko kuwa washambuliaji bora na mabeki wabovu.
TURIN, ITALIA: KOCHA wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson aliwahi kusema 'washambuliaji wanashinda mechi, mabeki wanashinda mataji'.
Ferguson alikuwa akiamini kwamba kama utakuwa na mabeki bora na washambuliaji bora basi kuna uwezekano mkubwa wa kushinda mataji kuliko kuwa washambuliaji bora na mabeki wabovu.
Makipa wamekuwa nguzo muhimu ya timu na ndio maana huwa ni ngumu sana kuona wakitolewa bila ya sababu katika mechi.
Hata hivyo, sio makipa wote wanaopata wanaopata nafasi ya kuanza na kuzitumikia timu zao kwenye mechi nyingi, kuna wengine muda mwingi hawaonekani hata benchini. Hapa tumekuletea makipa sita ambao wameorodheshwa na tovuti ya Goal.com kama ndio bora kwenye karne ya 21.
10. Emiliano Martinez
Kipa huyu anatajwa kuwa bora zaidi linapokuja suala la kuokoa mikwaju ya penalti. Alionyesha kiwango bora mwaka 2022 akiwa na timu ya taifa ya Argentina kwenye fainali za Kombe la Dunia akiokoa penalti za kuamua katika michezo dhidi ya Uholanzi na Ufaransa, na mbali ya kuokoa mipira kupitia mikono, miguu yake pia inafanya kazi kubwa.
Kocha wa timu yake ya sasa ya Aston Villa, Mhispania Unai Emery alipoulizwa kuhusu uwezo wa staa huyu alisema: "Ni mtu muhimu katika mechi nyingi."
Martinez, ambaye sasa ameshinda tuzo ya Kipa Bora wa Dunia ya Yashin ambayo hutolewa na waandaaji wa Ballon d'Or ameshinda Kombe la Dunia na Copa America akiwa na Argentina.
9. Jan Oblak
Kipaji na mafanikio ya kipa huyu havitajwi sana na watu ingawa mashabiki Atletico Madrid wanafahamu vizuri.
Kocha wa Atletico, Diego Simeone amekuwa akisisitiza kuwa kipa huyu raia wa Slovenia ni kipa bora zaidi duniani, huku mchezaji wa zamani Juanfran akisema Oblak ana kipaji zaidi kuliko kipa wao wa zamani, Thibaut Courtois, ambaye sasa anadakia Real Madrid. Hakuna shaka kuhusu hadhi yake.
Katika La Liga mbali ya kushinda taji hilo mara moja, amewahi kushinda tuzo nne za kipa bora wa msimu akifanya hivyo kuanzia kati ya 2015 na 2019.
8. Edwin van der Sar
Edwin van der Sar alikuwa mchezaji muhimu katika timu kubwa ya Ajax ya katikati ya miaka ya 90 kutokana na uwezo wake wa kucheza kama kipa anayeweza kuucheza na mpira mguuni mbali ya kudaka.
Alikuwa kioo cha wachezaji wengi ambapo hata Manuel Neuer amekiri kwamba mchezaji huyu wa Kiholanzi alikuwa chanzo cha yeye kupenda kucheza soka.
Kilichowahi kushangaza kuhusu Van der Sar ni jinsi alivyoweza kudumisha kiwango chake cha juu sana akiwa na umri wa miaka 30 na akawa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kushinda taji la Ligi Kuu England mwaka 2011 akiwa na miaka 40. Hata hivyo, tukio lake maarufu zaidi akiwa Manchester United lilikuja miaka mitatu kabla ya hapo alipookoa mkwaju wa penalti muhimu katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Chelsea iliyopigwa huko Moscow, Russia.
Kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson aliwahi kusema: "Edwin ndiye kipa bora tuliyekuwa naye tangu kuondoka kwa Peter Schmeichel."
7. Oliver Kahn
Inawezekana hadi leo bado anajilaumu kwa bao la kuchomesha katika fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2002 ambapo taifa lake Ujerumani lilipoteza mbele ya Brazil kwa mabao 2-0.
Hata hivyo, katika michuano hiyo Kahn alifanya kazi ya ziada na akaweka rekodi ya kuwa kipa wa kwanza katika historia ya michuano hiyo kuwahi kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mashindano.
Kahn ambaye alishinda mataji yote kwa ngazi ya klabu na timu ya taifa isipokuwa Kombe la Dunia mbali ya Manuel Neuer anatajwa kuwa kipa bora kuwahi kutokea katika historia ya Bayern Munich na Ujerumani kiujumla.
Wakati fulani, mtendaji mkuu wa Bayern Munich, Karl-Heinz Rummenigge alisema: "Oliver amefanya mambo makubwa akiwa na Bayern na timu ya taifa na soka la Ujerumani kiujumla."
6. Alisson
Ni nadra kuona kipa ana uwezo wa kubadilisha mchezo, lakini Alisson anaweza akafanya hivyo.
Liverpool walijua hili kabla ya kumchukua kwa bei ya kuvunja rekodi kutoka Roma mwaka 2018. Wakati huo, jina lake la utani alikuwa akiitwa 'Messi wa Makipa'.
Alisson ameisaidia Liverpool kufanya mambo mengi makubwa katika kipindi chake ikiwa pamoja na kushinda taji lao la sita la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30.
Yeye ndiye kipa nambari moja wa Brazil mbele ya Ederson wa Manchester City na katika kuthibitisha ubora wake wa kuchezea mpira mguuni, msimu 2020/21 alishinda tuzo ya Bao Bora la Msimu.
5. Thibaut Courtois
Hajafanikiwa kushinda taji lolote akiwa na timu ya taifa ya Ubelgiji, lakini amefanya vizuri akiwa na timu mbalimbali barani Ulaya akishinda mataji yote makubwa kuanzia Ligi ya Mabingwa na Kombe la Dunia kwa upande wa klabu.
Kipa huyu mwenye umri wa miaka 32 baada ya kusajiliwa na Chelsea mwaka 2011 akitokea Genk, alijijengea jina kama kipa bora zaidi La Liga kwa kipindi cha mkopo wa miaka mitatu Atletico Madrid, kabla ya kurejea Chelsea na kufanya hivyo pia katika EPL.
Courtois pia amewahi kushinda tuzo ya Kipa Bora wa Dunia katika mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Russia ambapo aliisaidia Ubelgiji kumaliza mshindi wa tatu.
4. Petr Cech
Hadi leo rekodi zake alizoziweka katika Ligi Kuu England bado zinaishi na hazijafikiwa. Katika msimu wa 2004-05, alionyesha ufanisi mkubwa kwa kucheza mechi 24 kati ya 35 za EPL bila ya kuruhusu bao huku mechi zilizobakia akiruhusu mabao 12 tu.
Cech pia anashikilia rekodi ya kuwa kipa aliyecheza mechi nyingi zaidi katika EPL bila ya kuruhusu bao ambapo alifanya hivyo katika mechi 202 na kipa anayemfuatia David James ambaye amefanya hivyo mara 169.
Kwa levo ya klabu ameshinda mataji yote kuanzia ndani ya England na michuano ya kimataifa. Pia huyu ndio kipa pekee katika historia ya EPL kushinda tuzo ya kipa bora wa msimu akiwa na timu mbili mfululizo ambapo mbali ya kuonyesha ubora wake akiwa Chelsea alifanya hivyo pia katika kikosi cha Arsenal.
3. Iker Casillas
Kipa huyu wa zamani wa Hispania alikuwa kipaji cha kipekee, na alikuwa na umri mdogo pale aliposhinda Kombe lake la kwanza la Ligi ya Mabingwa akiwa na Real Madrid, mwaka 2000.
Alikuwa na uwezo mkubwa wa kuchezea mpira miguu, na pia alikuwa kiongozi mzuri na aliongoza Hispania kutwaa mataji katika Michuano ya Euro 2008 na 2010, pamoja na Kombe la Dunia la 2010.
Kipa huyu pia ameshinda kila taji kuanzia timu ya taifa na klabu.
Wakati fulani, Gianluig Buffon aliwahi kumzungumzia akasema:"Sihitaji kutumia maneno mengi kusema jinsi Iker alivyokuwa na ubora.Kila mtu anaona alivyofanya. Amekwisha shinda kila kitu kinachoweza kushindaniwa."
2. Manuel Neuer
Kwa kiasi kikubwa Manuel Neuer alibadilisha mchezo kutokana na staili yake yakuwa bora kucheza na mpira mguuni.
Kabla yake kulikuwa na makipa waliokuwa na ufanisi na mpira miguu, lakini Neuer alifanya jukumu hilo kwa kipekee na kuna wakati Pep Guardiola alipokuwa anaifundisha Bayern Munich alisema alikuwa na wazo la kumtumia kama kiungo.
Neuer pia ameweka rekodi nyingi za 'clean sheet' huku akishinda mataji yote makubwa akiwa na Bayern Munich na upande wa timu ya taifa ameshinda Kombe la Dunia mwaka 2014 ambapo alishinda tuzo ya kipa bora na bado anaendelea kucheza kwa sasa akiwa na umri wa miaka 38.
1. Gianluigi Buffon
Juventus walilipa Euro 53 milioni ili kumnunua Buffon mwaka 2001. Alidumu katika levo za juu na kutajwa kama mmoja kati ya makipa bora dunia kwa miaka 17.
Buffon ambaye amewahi kushinda Kombe la Dunia mara moja aliwahi kuchaguliwa na shirika la utafiti la IFFHS kama kipa bora duniani kwa miaka mitano.
Vilevile alichukua tuzo ya kipa bora Serie A mara 12 akiwa na Juventus.
Kipa huyu ambaye alistaafu mwaka 2023 akiwa na umri wa miaka 43, anatajwa kuwa mmoja kati ya makipa ambao hawakuwahi kuchuja ubora wao hadi anastaafu.
Mmoja kati ya wachezaji wenzake aliowahi kucheza naye, Federico Bernadeschi alipoulizwa kuhusu lejendi huyu alisema:"Gigi aliandika historia, pia Gigi ni historia."