Mateso ya Barca kwa Madrid yalipoanzia
Muktasari:
- Katika mechi kali ya Ligi Kuu ya Hispania 'La Liga’ iliyochezwa kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu na wenyeji Real Madrid ilipasuliwa kwa mabao 4-0 nyumbani.
MOJA ya mechi bora ya soka duniani iliyowashika wadau wote wa soka hivi karibuni ni ile ya El Clasico iliyokutanisha miamba ya soka wa Hispania Real Madrid na Barcelona.
Katika mechi kali ya Ligi Kuu ya Hispania 'La Liga’ iliyochezwa kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu na wenyeji Real Madrid ilipasuliwa kwa mabao 4-0 nyumbani.
Katika mchezo huo, muhimu zaidi kwa Madrid msimu huu 2024/2025 ilikuwa ni lazima kushinda ili kujiweka pazuri kutetea ubingwa wa La Liga.
Madrid ilihitaji kushinda ili iwafikie Wakatalunya hao ambao tayari wapo juu wakiongoza msimamo wa ligi, hivyo kutishia nafasi ya watetezi hao.
Mtaani, vijiweni na mtandaoni kumekuwa na mjadala kati ya mashabiki wa Real Madrid ni nani wa kulaumiwa kwa kushindwa kwa aibu, hali isiyokukubalika na kuiumiza mioyo yao?
Nani anawajibika kwa mashabiki kuona kinyume cha walivyotarajia Real Madrid ilipotangaza, siku mbili tu baada ya kushinda taji la 15 la Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiwa wamemsajili Kylian Mbappe ambaye katika usiku huo alitupia mabao mawili ambayo yote yalikataliwa, kwani alikuwa ameshaotea na kukosa mengine mawili ya wazi mbayo yalitia shaka umakini wake katika siku hiyo.
Je, wachezaji vijana wenye utimamu kiafya wa Barcelona wa bei chee na kukulia Catalunya akademia ni bora zaidi kuliko wachezaji vijana nyota wakubwa duniani wa Madrid walionunuliwa kwa bei mbaya?
Wataalamu wa ufundi katika soka wanasema itakuwa na maana zaidi ikiwa Madrid ingekuwa timu inayoendelea kujengwa upya, bila pesa nyingi za kutumia na bila nyota wakubwa zaidi duniani.
Kikundi cha wachapakazi wa utimamu wa vijana wa Barcelona kinajumuisha wataalamu wakongwe wanne ambao ni Julio Tous, Pepe Conde, Rafael Maldonado na German Fernandez.
Hicho kikundi ndicho unachokiona baada ya mchezo wachezaji huwa wanawakumbatia kwa furaha wakipongeza kazi yao ya kusimamia utimamu wa miili na hatimaye kucheza wakiwa imara.
SIRI NZIMA HII HAPA
Ukiacha Madrid kuzidiwa kiufundi, jicho la Spoti Dokta linaona kilichowaangusha pia ni ubora wa Barcelona katika utimamu kiafya, umri, uimara wa kisaikolojia, ustawi bora wa hisia na utamaduni.
Barcelona walisajili mchezaji mmoja au wawili wazuri, tena walio na majeraha makubwa kwa wachezaji wao bora ikiwamo Robert Lewandowski aliyezeeka.
Lakini siku hiyo akiwa chini ya kocha mpya, Hans Flick aliyetokea klabu ya zamani Buyern Munich alifanikiwa kufunga mabao mawili kati ya manne. Hii ina maana waliweza kutibu majeraha na kumrudisha akiwa imara.
Watu wa utimamu wa mwili kiafya kwa wanasoka wa Barcelona waliwazidi ujanja wa Madrid, wengi wao ni wachanga kiumri wameonekana kukomaa kimwili na kiakili.
Mchanganyiko wa umri kwa Barcelona uliwabeba, ni kama vile kuweka gari la zamani lenye uzoefu wa njia na jipya lililo imara.
Itakumbukwa Barcelona ni moja ya klabu ambayo inazalisha makinda wenye uwezo wa hali ya juu wakiwa timamu kiafya ikiwamo kutopata majeraha, wepesi wenye kunyumbulika wakiwa na kasi.
Ukilinganisha na makinda ambao walizalishwa na klabu ya Madrid wengi wao wameuzwa, hawapo, waliopo sasa wamenunuliwa wa pesa ndefu kutoka klabu zingine.
Ni mchanganyiko wa kuzaliwa upya, uamsho na ujana kwa wakatalunya ambao sasa wamepata mchanganyiko wa ajabu wa kile kilichohitajika muda mrefu.
Ndani ya mechi mbili utumamu wa makinda ndiyo ambao unawabeba kwani wamefunga mabao nane katika mechi mbili ambazo wamecheza na timu kubwa yaani Madrid na Buyern Munich.
Mafundi wa utimamu wa mwili ndio sasa wamewatupa wahitimu wao wa La Masia kwenye mwisho wa kina na kuona ni nani anayeweza kuogelea.
Kwa sasa, kila mtu katika Katalunya anaogelea, huku Madrid klabu inayoendeshwa vyema na wachezaji bora na yenye mafanikio zaidi katika muongo uliopita, inaonekana kama meli inayozama.
Hilo ni jambo ambalo limekuwa likiwasumbua mashabiki wa Real Madrid na ni kisa cha wivu unaostahili kwa jinsi Barcelona inavyoweza kuwaanzisha vijana wa miaka 17 kwenye michezo mikubwa na kuwaona wakifanikiwa, huku Madrid ni ngumu zaidi.
Katika miaka 10 iliyopita Real Madrid imekuwa na wachezaji wazuri sana waliotoka katika akademia yao ya Castilla na baadhi yao wameuzwa na waliopo bado kuthibitisha uwezo wao katika kikosi cha kwanza.
Wakati wale wa Barcelona karibu kila mara wanapewa nafasi na kuaminiwa katika utimamu wao katika umri mdogo ikiwamo kinda wa miaka 17 Lamine Yamal aliyefunga bao la tatu na kutoa pasi bao la nne.
Makinda hao wa Barcelona katika mechi mbili walizoshinda wameonekana wakiwa timamu kiafya ikiwamo kuwa wepesi wenye kasi, hivyo kuwa wajanja katika mashambulizi ya kushtukiza.
Utulivu wao wa kiakili kunawafanya kuwa na maamuzi sahihi ya uhakika katika wakati sahihi. Tazama pasi zao ndefu zilizokuwa zinatua kwa mshambuliaji msaidizi Raphinha.
Wataalam wa Afya ya akili ikiwamo wanasaikolojia na walimu wao katika benchi la ufundi limewajengea saikolojia nzuri makinda wao kiasi cha kucheza bila hofu wakijiamini kupita kiasi.
Kuingia kwa kocha mpya Barcelona kumeleta hamasa mpya, gea aliyoingia nayo imeleta ari ya ushindi kwa makinda hao ambao na wao wanaota kuwa kama Lionel Messi.
Akademia yao huwa ina utamaduni wa kipekee, mchezaji kijana anapolelewa hapo anaota mpira wa soka tu, anahamasika kucheza soka la kasi, pasi fupi, kunyumbulika na kushambulia kwa akili.
CHUKUA HII
Wachezaji makinda katika akademia angali wadogo wanahitaji kujengwa kimwili na kiakili, kutamanishwa kupata mafanikio katika njia sahihi na kuwa na nidhamu ya mazoezi na mafunzo ya soka.
Ustawi wa kiakili na kihisia chanya ni muhimu kujengwa, kuboreshwa na kulindwa kila wakati.
Kuepushwa na mkazo wowote wa kiakili kupita kiasi, kuwa na mazungumzo chanya ya kibinafsi wakati wote na kuwa ujajasiri wa mawazo chanya ikiwamo kukutanishwa na mastaa waliostaafu.
Utii wa maelekezo wanayopewa ikiwamo mazoezi ya kupasha moto kabla ya kucheza, mazoezi ya uponaji baada ya mechi, kupumzika na kulala, mpango wa lishe na mbinu za kuepuka majeraha.
Hii inaweza kusaidia kuzuia kuumia, kuchangia kucheza kwa kijiamini kwa kiwango cha juu, kuwa na maisha marefu katika mchezo pasipo kukumbana na majeraha mabaya, hatimaye kushinda kwa kiwango.