Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: Manchester City katikati ya mtego mgumu England

Muktasari:

  • Man City inakabiliana na mashtaka 115 mbele ya jopo la majaji watatu wa Tume Huru ya Ligi Kuu (PL).

MABINGWA wa Ligi Kuu England (EPL), Manchester City,  juma hili wako katika mtihani mgumu  pengine kuliko yote waliyowahi kupitia katika historia ya klabu hiyo.

Man City inakabiliana na mashtaka 115 mbele ya jopo la majaji watatu wa Tume Huru ya Ligi Kuu (PL).

Ni mtihani mgumu unaoweza kutoa muelekeo wa klabu hiyo yenye mafanikio England na sasa inaanza kutengeneza jina lake kama moja ya klabu kubwa Ulaya.

Klabu ya Everton inayocheza pia EPL ilipata kupokwa pointi 10 katika msimamo wa Ligi Kuu hiyo maarufu duniani. Everton, moja ya klabu kongwe za England ikiwa imeanzishwa mwaka 1878, ilituhumiwa na ikakiri kosa na kutiwa hatiani kwa kuvuka mstari wa matumizi ya fedha (Financial Fair Play) kwa kuwa na madeni makubwa yakilinganishwa na mapato iliyokuwa nayo.

Inadaiwa, Everton ilipata hasara ya kiasi cha Pauni 371.8 milioni (karibu Sh1.8 trilioni) katika kipindi cha miaka mitatu, huku kiwango cha hasara kinachoruhusiwa ni kiasi kisichozidi Pauni 105 milioni (karibu ya Sh 335 bilioni) kwa miaka mitatu.

Kwa hatua hiyo, klabu hiyo ya viunga vya Merseyside jijini Liverpool, Kaskazini Magharibi mwa England ilifanya kazi ya ziada uwanjani, lakini ilikata rufaa mara mbili, huku adhabu ikipunguzwa hadi alama 6 na 2 mtawalia, hivyo kuweza kubaki katika daraja la Ligi Kuu.

Nottingham Forest pia walijikuta katika wakati mgumu msimu uliopita, lakini kama ilivyokuwa wenzao Everton, Notingham Forest pia walipambana na kubaki Ligi Kuu pamoja na kupokwa pointi nne.

Mashauri waliyokabiliana nayo Everton na Nottingham Forest katika msimu wa 2023/24 yanafanana  na yanayowakabili wenzao katika ligi hiyo, yaani Manchester City, ingawa mashitaka yao yanatajwa kufika zaidi ya 115.

Yawezekana mapito ya Manchester City, iwapo watapoteza shauri lao linalosikilizwa na majaji watatu juma hili, yakawa mabaya sana kuliko mapito ya wenzao wa Everton na Forest.

Man City si wageni wa mashauri yanayohusiana na kukiuka taratibu za matumizi ya fedha kiungwana kwani mwaka 2014 iliadhibiwa Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) kwa kupigwa faini ya Dola 82 milioni kwa kosa la kukiuka kanuni ya matumizi ya kiungwana yaani Football Financial Fair Play (FFFP).

Manchester City ililazimika kulipa kiasi hicho cha fedha zikigawanywa kwa miaka mitatu, pia kulazimika kucheza Ligi ya Mabingwa ya Ulaya na kikosi kilichopunguzwa cha wachezaji 21.

Mwaka 2020 Man City ilikutana tena na rungu la Uefa kwa kupigwa marufuku kushiriki mashindano ya shirikisho hilo kwa miaka miwili mfululizo kwa makosa ya kudanganya kuhusu mapato ya wadhamini na pia kutotoa ushirikiano kwa wachunguzi wa Uefa.

Hata hivyo, City ilikwenda Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Masuala ya Michezo (CAS) na kukata rufaa ambayo ilibadilisha adhabu kwa kuondolewa katazo la kucheza mashindano ya Ulaya na pia faini yao kupunguzwa kutoka Euro milioni 30 hadi Euro milioni 10.

CAS iliipa Manchester City karipio kubwa kwa kutotoa ushirikiano kwa wachunguzi wa Uefa.

Siku mbaya hazizoeleki, Manchester City ambayo imetawala EPL kwa miaka ya karibuni inaweza isiruke kiunzi hiki kama ilivyokuwa huko nyuma, kwani uzoefu wa kesi za Everton na Nottingham Forest unaonyesha Ligi Kuu ya England haina mzaha katika kutoa adhabu katika masuala ya ukiukwaji wa kanuni za matumizi ya fedha kiungwana.

Utajiri mkubwa wa Manchester City hasa baada ya ujio wa matajiri wa Abu Dhabi umechangia kwa kiasi kikubwa kwa timu hiyo kujikuta katika mtego wa matumizi mabaya ya fedha.

Tofauti na Everton au Forest ambao matatizo yao yanaweza kuwa yanatokana na ukosefu wa fedha, matatizo ya City yanatokana na kuogelea katika maburungutu ya fedha.

Wakati ni vigumu kutwaa ubingwa wa England kwa baadhi ya klabu kutokana na upungufu wa fedha, kwa matajiri wa Manchester City, mtihani ni namna gani ya kuingiza pesa za ziada ili kuweza kutwaa ubingwa.

Kwa maana nyingine wananunua ubingwa. Haishangazi Manchester City wamekuwa wababe wa Ligi Kuu ya England kwa miaka minne mfululizo, jambo ambalo ni geni kwa Waingereza. Fedha imeleta maajabu.

Man City inaweza kupigwa faini, kupokwa pointi hata ‘kunyang’anywa’ mataji iliyopata huko nyuma. Manchester City imekuwa sio tu ni chombo cha michezo cha mmiliki wake Sheikh Mansour Bin Zayed wa Abu Dhabi, bali pia imekuwa ni taswira yake na zana muhimu ya diplomasia kwa ufalme wake.

Kashfa kama hii haiwezi kumwacha salama Sheikh Mansour na uwezekano mkubwa pale likitokea la kutokea ni kwa tajiri huyo kuitelekeza City na kununua klabu nyingine, labda kwenye ligi nyingine itakayompa heshima anayoitaka.

Bado ni mapema mno kuiongelea City katika wakati uliopita na kesi dhidi yake haiwezi kuwa rahisi kwa sababu wana msuli wa kisheria, kifedha na mahusiano katika Uefa na Fifa.


HII FFP NI NINI?

Hii Financial Fair Play au mstari wa matumizi ya fedha kiungwana ni nini?

Hii ni kanuni iliyoanzishwa na shirikisho la vyama vya soka vya Ulaya (UEFA) mwaka 2009.

Lengo la kanuni hii ni kudhibiti matumizi ya klabu ili visiishi zaidi ya kipato chao. Nia ya jumla ni kudhibiti, kusimamia na kuendeleza uwezo wa kiuchumi wa klabu za soka.

Lengo lisilotajwa wazi katika kanuni hii ni pamoja na kuzuia mpira kuendeshwa na fedha zisizo mapato ya mpira na zaidi pesa chafu kama za mauzo ya dawa za kulevya, mauzo haramu ya silaha, usafirishaji haramu wa binadamu na shughuli nyingine za magenge ya kihalifu.

Mamlaka za soka katika mataifa wanachama wa Uefa zinatakiwa kuhakikisha nidhamu hii inazingatiwa na kuingizwa katika kanuni zao kulingana na mazingira yao.

Katika Ligi Kuu ya England, kanuni hizi zimedhibiti na kuzuia klabu zenye tamaa ya kununua mafanikio na kuingia katika hatari ya kufilisika.

Kumekuwa na mitazamo tofauti kuhusu umuhimu na tija ya FFFP. Baadhi ya wachambuzi wanaiona kanuni hii ya uungwana katika matumizi ya fedha kama kidhibiti mwendo katika maendeleo ya soka.

Wenye mtazamo huu wanaona soka kama sekta ambayo bado inahitaji uwekezaji mkubwa wa fedha ili iweze kupiga hatua.

Wanaoiunga mkono kanuni hiyo ya uungwana katika matumizi ya fedha wanaiona fedha kama tishio kwa utamaduni na uwepo wa klabu za soka. Wanasema fedha ikiachwa itembee basi mpira utatambaa.

Bila shaka hatma ya kesi ya Manchester City inaweza kuwa imeshikiria hatma ya kanuni ya uungwana katika soka kwenye ligi ya Englandna Ulaya kwa jumla.

Kushindwa kwa City katika kesi hii kunaweza kuwa na madhara ya kiwango cha tetemeko katika Ligi Kuu ya England (EPL).


Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.