Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NYUMA YA PAZIA: Tulimsubiri Maradona tukaletewa Salvatore ‘Toto’ Shillaci

Muktasari:

  • Kombe la Dunia lilipowadia mwaka 1990 pale Italia, dunia ilikuwa inamsubiri mchezaji mmoja tu aiweke michuano hiyo katika mfuko wake. Diego Maradona.

KABLA ya Fei Toto tayari kuna mtu aliwahi kuitwa Toto. Salvatore ‘Toto’ Shillaci. Mpira bwana. Mungu huwa anaamua tu kutupa njia tofauti na ile ambayo tunaifikiria.

Kombe la Dunia lilipowadia mwaka 1990 pale Italia, dunia ilikuwa inamsubiri mchezaji mmoja tu aiweke michuano hiyo katika mfuko wake. Diego Maradona.

Ndiyo, Maradona alikuwa ametoka kuiteka dunia miaka minne kabla ya hapo kule Mexico. Alipiga shoo ya peke yake na kuipeleka Argentina katika fainali dhidi ya Ujerumani Magharibi na kisha wakachukua ubingwa.

Ni michuano hiyo ndiyo ambayo ilisababisha watu waanze kubishana kuhusu ubora wa Maradona na ule wa Pele. ni kama ambavyo kwa muda mrefu watu wamekuwa wakibishana kuhusu ubora wa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Miaka minne baadaye dunia ilikuwa inamsubiri Maradona nchini Italia katika kombe jingine la dunia kuona akifanya miujiza yake, lakini ghafla akaibuka mtu mwingine kutoka kusikojulikana. Salvatore Toto Shillaci. Muitaliano.

Hata Waitaliano wenyewe walikuwa hawamfahamu Toto. Mechi yake ya kwanza katika kikosi cha Italia alicheza Machi 1990. Ina maana miezi mitatu tu kabla ya kuanza Kombe la Dunia. Mwenyewe hakutazamiwa kuitwa katika kikosi cha Italia. Mechi hiyo ndiyo ilikuwa pekee katika kikosi cha Italia kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia.

Alikuwa mchezaji wa mwisho kuitwa na kocha Azeglio Vicini. Kifupi ni kwamba alikuwa ameitwa kizalizali tu. Pambano la kwanza la Waitaliano dhidi ya Austria alikaa katika benchi na ilitazamiwa kwamba angekaa benchi. Hakuna aliyeshangaa.

Uwanjani mambo yakawa magumu kwa Waitaliano huku Toto akiitazama mechi akiwa katika benchi. Baadaye akaingia na hapo hapo katika dakika za majeruhi akafunga bao la ushindi. Hata yeye mwenyewe hakuamini kama alikuwa ameliokoa taifa lake.

Picha ya Toto akishangilia bao dhidi ya Austria ni moja kati ya picha maarufu duniani. Mechi ya pili dhidi ya Marekani, Italia walipata ushindi mwembamba. Toto hakufunga, lakini taifa likapiga kelele Toto awe anaanza pale mbele sambamba na Roberto Baggio.

Kweli Vicini akamuanzisha Toto kando ya Baggio katika pambano lililofuata dhidi ya Czechoslovakia. Wote wawili wakatupia. Baggio na Toto. Pambano likaisha kwa ushindi wa mabao 2-0. Toto alikuwa amehalalisha matakwa ya mashabiki wa Italia.

Mechi iliyofuata dhidi ya Uruguay Toto akafunga bao jingine na kisha kupika jingine. Dunia ikaanza kupagawa zaidi na Toto. Akanogewa zaidi. Akafunga katika pambano dhidi ya Ireland na kuitoa katika michuano. Lilikuwa bao la jioni ambalo mpaka leo linaumiza mioyo ya mashabiki wa Ireland.

Nusu fainali dhidi ya Argentina Toto akafunga tena, lakini ilikuwa siku ya huzuni kwa taifa hilo kwa sababu walitolewa katika michuano. Wenyeji wakapata huzuni kali kwa kutolewa katika hatua ya matuta. Pambano la mshindi wa tatu dhidi ya England Toto akafunga tena.

Akaibuka kuwa mfungaji bora wa Kombe la Dunia 1990. Lakini hapo hapo akaibuka kuwa mchezaji bora wa michuano. Nafasi ya pili na ya tatu zilikwenda kwa Diego Maradona na nahodha wa Ujerumani, Lothar Matthaus mtawalia. Hawa walikuwa manahodha ambao walikuwa wamezipeleka nchi zao fainali ya Kombe la Dunia kwa mara nyingine tena.

Kutoka kusikojulikana hadi kuwa mchezaji bora wa michuano kuliwaacha watu wengi midomo wazi. Watu ambao walikuwa wanaamini kwamba kwa mara nyingine tena hii ingeweza kuwa michuano ya Diego Maradona au mastaa wengine wakubwa waliong’ara 1986 au wale ambao waliibukia hapo njiani.

Habari ya kusikitisha ni kwamba Toto amefariki katikati ya wiki hii pale kwao Palermo, Italia, akiwa na umri wa miaka 59. Ugonjwa wa kansa ya utumbo mkubwa umehitimisha maisha yake huku hadithi ya kusisimua ya Kombe la Dunia 1990 ikiendelea kukumbukwa na watu wengi ambao walifuatilia kwa karibu michuano ya mwaka huo.

Kitu ambacho kinakumbukwa zaidi ni namna ambavyo kama ilivyo katika michuano fulani huwa inaweza kutokea timu ambayo inaweza kufanya mambo ya kushangaza, basi ndivyo vilevile katika michuano fulani anavyoweza kutokea mchezaji wa kushangaza.

Wote mnaweza kutazama upande wa kulia, lakini ghafla akaibuka mtu kutoka upande wa kushoto na kukimbia kwa kasi kiasi wote mkageuza shingo zenu. Ndicho alichofanya Salvatore Toto Shillaci. Hata miaka minne baadaye kitu kama hicho kilitokea, lakini siyo kwa staili ya Toto.

Mrusi Oleg Salenko aliibuka kuwa mfungaji bora wa Kombe la Dunia kando ya Hristo Stoichkov wa Bulgaria. Salenko alifunga mabao matano katika pambano moja la makundi dhidi ya Cameroon na baadaye akafunga jingine ambalo lilimuwezesha kufikisha mabao sita na kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo, huku akiwaacha midomo wazi mashabiki wa soka duniani ambao hawakumfahamu kabla ya hapo.

Akapumzike kwa amani Salvatore Toto Shillaci. Alizaliwa katika eneo la watu masikini pale kwao Palermo. Kilichobadilisha maisha yake yote kwa ujumla ni wiki nne tu za Kombe la Dunia katika ardhi ya kwao.

Hata baada ya kumaliza maisha ya soka la kulipwa alirudi kwao Palermo na kuishi kama mtu wa kawaida tu, lakini kwa yeyote ambaye alikutana naye barabarani alipenda kuzungumza naye na kumkumbusha kuhusu ushujaa wake wa Kombe la Dunia la mwaka 1990.

Amefia katika ardhi yao kwao Palermo akiwa shujaa wa Waitaliano. Shujaa wa kila mtu. Miongoni mwa mashujaa wa Kombe la Dunia ambalo walilipa hadhi kombe lenyewe kwa kutuletea mtu tofauti na wale ambao tulikuwa tunawategemea.