Taifa Stars kanyaga twen’zetu Afcon 2025
Muktasari:
- Mechi hii inatarajiwa kuwa kama fainali kwa Taifa Stars ambayo inazihitaji pointi tatu za mchezo huo ambao utachezwa Martyrs, Kinshasa ili kufufua matumaini ya kufuzu kwa mara ya nne.
TAIFA Stars itakuwa na mtihani muhimu Jumamosi hii Novemba 16, 2024, dhidi ya wenyeji wao, Ethiopia huko DR Congo katika mchezo kuwania nafasi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, Morocco.
Mechi hii inatarajiwa kuwa kama fainali kwa Taifa Stars ambayo inazihitaji pointi tatu za mchezo huo ambao utachezwa Martyrs, Kinshasa ili kufufua matumaini ya kufuzu kwa mara ya nne.
Taifa Stars ipo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi H ikiwa na pointi nne, huku Guinea ikishika nafasi ya pili kwa pointi sita na vinara ni DR Congo ambao wameshafuzu wakiwa na pointi 12. Ethiopia, ambayo itakuwa mwenyeji, ipo katika nafasi ya mwisho ikiwa na pointi moja tu.
Kwa Tanzania, ushindi katika mchezo huu ni muhimu kwa sababu utawapa nafasi nzuri kuelekea mchezo wa mwisho dhidi ya Guinea.
Kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ amekuwa akijaribu kutengeneza kikosi kilichosheheni vipaji na nidhamu ya kimchezo ili kukabiliana na changamoto za kufuzu. Katika mchezo huu, Tanzania itahitaji kutegemea sana uzoefu wa wachezaji wake wa kimataifa kama Simon Msuva na Mbwana Samatta, ambao wanatarajiwa kuwa na jukumu kubwa la kuongoza safu ya ushambuliaji na kuleta ufanisi.
Kwa upande mwingine, Ethiopia ina hamasa ya kutaka kuboresha matokeo yake na kutoa changamoto kwa Taifa Stars. Kikosi cha Ethiopia kinatambulika kwa uchezaji wao wa pasi fupifupi na uwepo wa wachezaji wenye uzoefu kama Shimelis Bekele unaweza kuipa nguvu timu hiyo.
Nafasi ya Tanzania kwenye kundi H ipo wazi endapo itashinda, mchezo huu utahitaji nidhamu ya hali ya juu na umakini, hasa katika safu ya ulinzi na kiungo. Taifa Stars itahitaji kujihadhari na mashambulizi ya Ethiopia, huku wakipanga mikakati madhubuti ya kuzuia nafasi za hatari na kutengeneza nafasi za kufunga mabao.
UDHAIFU WA ETHIOPIA
Katika michezo mitano iliyopita huku Ethiopia ikiwa nyumbani kwa mujibu wa ratiba, wamefungwa michezo mitatu ambayo ni dhidi ya Lesotho (2-1), DR Congo (2-0) na Guinea (3-0), huku wakishinda mara mbili dhidi ya Eritrea (3-0) na Lesotho waliporudiana katika mchezo wa kirafiki (2-1).
Takwimu hizi zinaonyesha picha ya timu inayokutana na changamoto kubwa hasa wanapocheza uwanja wa nyumbani.
Ethiopia, ambao hadi sasa hawana makazi maalum ya kudumu kwa michezo yao ya nyumbani, wamekuwa na muda mgumu katika michezo ya kufuzu, na kwa mujibu wa takwimu, wamefungika kwa urahisi katika baadhi ya mechi zao.
Katika michezo mitano iliyopita wameruhusu jumla ya mabao manane, na kwa wastani ni karibu mabao mawili kwa kila mchezo.
Ethiopia wamekuwa wakicheza michezo yao ya nyumbani kwenye viwanja mbalimbali, walianza kutumia uwanja wa Alassane Ouattara huko Abidjan, Ivory Coast, na sasa wamehamia Martyrs huko Kinshasa, nchini DR Congo.
Hii inadhihirisha kwamba timu hiyo inakutana na changamoto ya kutokuwa na uwanja wa nyumbani maalum, jambo ambalo linaweza kuwaathiri kisaikolojia na kimkakati. Kwa kuongezea, Ethiopia inaonekana kuwa ni timu inayofunguka hasa katika kipindi cha kwanza cha michezo yao.
Kati ya mabao manane waliyoruhusu wakiwa nyumbani, sita ya hayo yamefungwa kipindi cha kwanza, na hii ni dalili kuwa kuna mwanya mkubwa ambao Taifa Stars inaweza kuutumia.
Morocco atahitaji kuwajengea wachezaji wake mbinu za kutumia mwanya wa ulinzi dhaifu wa Ethiopia, hasa katika kipindi cha kwanza. Ethiopia wamekuwa wakifungwa haraka kipindi cha kwanza, na katika kipigo cha mwisho dhidi ya Guinea kwenye kinyang’anyiro cha kufuzu kwa AFCON, walifungwa mabao yote matatu ndani ya dakika 23 tu za kipindi cha kwanza. Wakati huo, Guinea walikamilisha kazi yao mapema na kutawala mchezo. Hii ni ishara kuwa Ethiopia inapokutana na timu inayokuwa makini na yenye kasi, wanaweza kupoteza mapema.
SAMATTA NA MSUVA
Kwa hiyo, Taifa Stars ikiongozwa na wachezaji wake wenye uzoefu kama Mbwana Samatta ambaye alifanya kazi nzuri na kubwa kwenye michezo miwili dhidi ya DR Congo na Simon Msuva ambaye amerejea kikosini, itahitaji kuanzisha mashambulizi ya haraka na kutumia vizuri nafasi za mapema.
Kwanini? Ili kuweka presha kwa Ethiopia na kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata pointi tatu muhimu. Kuwa na umakini na kutumia vizuri uwezo wao katika kipindi cha kwanza kunaweza kuwa na manufaa makubwa kwa Taifa Stars, kwani itawezesha timu kupata matokeo mazuri.
STARS UGENINI
Katika michezo mitano ya hivi karibuni ya Taifa Stars wakiwa ugenini kwenye mashindano mbalimbali, timu hiyo imeshinda mechi mbili muhimu, ikiwa ni dhidi ya Guinea kwa mabao 2-1 ya Feisal Salum na Mudathir Yahya, na pia dhidi ya Zambia kwa bao 1-0 la Wazir Junior.
Ushindi huu ni ishara kwamba Taifa Stars inaweza kufanikiwa kushinda michezo ya ugenini, hasa inapofanya maandalizi mazuri na kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu, licha ya changamoto zinazoweza kujitokeza.
Mbali na ushindi huo, Taifa Stars pia ilipata sare ya bila kufungana dhidi ya Indonesia, jambo linaloonyesha kuwa kikosi hicho kinaweza kudhibiti kasi na kuzuia mashambulizi ya wapinzani hata katika mazingira ya ugenini. Hii ni dalili kuwa Taifa Stars ina uwezo wa kubadilika kulingana na hali ya mchezo na mpinzani, hasa ikizingatia kuwa michezo ya ugenini mara nyingi huhitaji nidhamu ya juu kwenye safu ya ulinzi.
Hata hivyo, Taifa Stars ilikumbana na vipigo katika mechi mbili mfululizo za ugenini hivi karibuni dhidi ya DR Congo na Sudan, ambapo walifungwa kwa bao 1-0 kila mchezo.
Katika mchezo huu dhidi ya Ethiopia, Taifa Stars itahitaji kuongeza umakini, siyo tu kwa kuzingatia mafanikio yao ya awali ya ugenini, bali pia kwa kujifunza kutokana na makosa yao kwenye mechi walizopoteza. Ushindi dhidi ya Guinea na Zambia unaonyesha kwamba Taifa Stars inaweza kuhimili presha na kujilinda kwa ufanisi, lakini mechi dhidi ya DR Congo na Sudan ni funzo kwamba ugenini, kila nafasi inahitaji kutumiwa vizuri.