Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Unawakumbuka? Hawa jamaa walitisha, sasa hivi ni makocha

Muktasari:

  • Wanasoka wa zama hizo za ‘Barclays’ ni kama Michu na si Wayne Rooney. Morten Gamst Pedersen na si Cristiano Ronaldo. Unaelewa?

LONDON, ENGLAND: ZAMA za Barclays Premier League zilifika ukomo 2016 na kitu usichokijua ni kwamba mastaa kibao waliokuwa matata katika zama hizo kwa sasa wamekuwa makocha wa maana kabisa kwenye soka.

Wanasoka wa zama hizo za ‘Barclays’ ni kama Michu na si Wayne Rooney. Morten Gamst Pedersen na si Cristiano Ronaldo. Unaelewa?

Na kwa kurudi kwenye zama za Barclays Premier League, kuna mastaa wanane waliokuwa matata wakati wanacheza, ambapo kwa sasa wamejiingiza kwenye ukocha. Habari ndo hiyo.


Charlie Adam

Kiungo mmoja mgumu aliyekuwa na mambo mengi uwanjani, huku kitu chake matata kabisa ni yale mabao yake ya mashuti ya mbali. Charlie Adam alitamba na timu kama Blackpool na Stoke City. Aliichezea pia Liverpool. Alistaafu soka mwaka 2022 na hakutaka kuchelewa, moja kwa moja alijiingiza kwenye ukocha. Alipata ajira ya kuinoa Fleetwood Town, Desemba mwaka jana na licha ya kuishuhudia timu hiyo ikishuka daraja kutoka League One msimu uliopita, bado ameendelea kuaminika kwamba atawapandisha tena.


Ryan Shawcross

Mashabiki wa Arsenal watakuwa wanamfahamu vyema beki Ryan Shawcross kwa tukio alilowahi kulifanya kwa kiungo wao Aaron Ramsey alipomvunja mguu baada ya kumchezea rafu mbaya iliyomweka nje staa huyo kwa miezi tisa. Beki huyo wa kati alikuwa akicheza soka gumu sana Stoke City, mahali ambako kwa sasa anafanya kazi kama kocha. Shawcross alikuwa mtu hatari kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Tony Pulis. Lakini, baada ya kufanya kazi ya ukocha kwenye kikosi cha Stoke, mechi yake ya kwanza alikabiliana na Charlie Adam kwenye EFL Cup, ambapo Stoke iliichapa Fleetwood Town kwa penalti.


Emmerson Boyce

Ni kitu kisichopingika kwamba wachezaji wengi waliokuwa kwenye kikosi cha Wigan Athletic kati ya 2004 na 2013 ni wale wa ile Ligi Kuu England ya zama za Barclays. Boyce alikuwa mtu muhimu kwenye kikosi cha Wigan kwa muda wote waliokuwa kwenye Ligi Kuu England na tangu alipostaafu soka ameingia kwenye kazi ya ukocha. Na baada ya kuanza kazi ya kuwa kocha wa kipindi cha mpito kwenye timu ya Barbados, kwa sasa amepata kazi ya kuwa kocha wa timu ya soka ya wanawake ya klabu ya Wigan Athletic.


Martin Demichelis

Beki huyo Muargentina alitumikia miaka mitatu kwenye kikosi cha Manchester City kwenye zama za Barclays na kujipambanua kama moja ya wachezaji muhimu kabisa kwenye nyakati hizo. Tangu alipostaafu soka mwaka 2017, staa huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Argentina amepata kazi ya ukocha kwenye klabu nyingi tofauti. Alianzia kwenye ukocha wa timu ya vijana ya Bayern Munich, kisha akaenda kuinoa River Plate na sasa ni kocha wa Monterrey, ikiwa ni sehemu ya kujiweka kwenye ubora katika idara hiyo ya ukocha.


Tom Cleverley

Alizichezea Manchester United, Wigan Athletic, Aston Villa na Everton katika zama hizo za Barclays, huku akijipambanua kuwa mmoja wa viungo matata kabisa waliopata kutokea kwenye Ligi Kuu England. Umri wake bado ni miaka 35, hivyo anakuwa kocha kijana zaidi kwenye orodha hii. Baada ya kufanya kazi kwa muda Watford, alichaguliwa kocha rasmi mwishoni mwa msimu wa 2023–24. Akiitambua Watford kwa kuajiri na kufukuza makocha, Cleverley ameanza vizuri, timu yake ipo namba tano kwenye Championship.


Alberto Aquilani

Mtu ambaye alinaswa na Liverpool kwenda kuchukua mikoba ya Xabi Alonso huko Liverpool. Lakini, mambo hayakwenda sawa kwa mkali huyo kwa muda wake aliokuwa England kutokana na majeraha kumtibulia maisha katika miaka mitatu aliyokuwa Anfield. Sasa umri wake ni miaka 40 na amekuwa kocha wa mpira. Baada ya kuanza kama kocha wa timu ya vijana ya Fiorentina, alipata kazi ya kuinoa Pisa mwaka jana, kabla ya kuachana na timu hiyo kwenye majira ya kiangazi ya mwaka huu na sasa yupo huru, hana kazi, anasubiri simu ziite.


Angel Rangel

Beki huyo Mhispaniola ameendelea kuwa karibu na Swansea City tangu alipostaafu soka na sasa ni kocha wa Pontardawe Town kwa kikosi chao cha Under-12. Akiwa na umri wa miaka 41, huku dhamira yake kubwa ikiwa ni kufanya vizuri kwenye ukocha wa soka la kulipwa, Rangel anaonekana kufurahia maisha yake huko Pontardawe Town kwa sababu mambo yanakwenda vizuri. Rangel alikuwa mmoja wa wachezaji waliotamba sana kwenye Ligi Kuu England kwenye zama hizo za Big Four na si Big Six.


Craig Bellamy

Baada ya kuibukia kwenye benchi la ufundi kama kocha msaidizi chini ya Vincent Kompany huko Burnley, Bellamy sasa amenasa kazi ya kuwa kocha wa Wales. Bellamy ni moja ya wachezaji wa moto sana katika kipindi hicho cha Ligi Kuu England ya zamani, alipotamba kwenye timu kibao ikiwamo Liverpool na Manchester City. Alikuwa miongoni mwa wachezaji wakorofi ndani ya uwanja na kupenda soka la kibabe, lakini moja ya matukio yanayokumbukwa ni kiwango chake alichokionyesha kwenye mechi ya Manchester derby mwaka 2009 alipofunga bonge la bao kwa shuti ka mbali sana.