Nusu fainali ya wageni Kagame Cup 2024
Muktasari:
Nusu fainali ya kwanza itazikutanisha APR ya Rwanda dhidi ya Al Hilal ya Sudan mechi itakayopigwa kuanzia saa 9:00 alasiri kwenye Uwanja wa KMC, kisha mchezo wa pili utapigwa saa 1:00 usiku Azam Complex kati ya Al Wadi ya Sudan na Red Arrows ya Zambia.
MICHUANO ya Kombe la Kagame 2024 imefikia patamu wakati leo zikipigwa mechi za nusu fainali ambazo hata hivyo zinakutanisha wageni watupu, baada ya wenyeji Coastal Union, Singida BS na JKU kutolewa mapema hatua ya makundi.
Nusu fainali ya kwanza itazikutanisha APR ya Rwanda dhidi ya Al Hilal ya Sudan mechi itakayopigwa kuanzia saa 9:00 alasiri kwenye Uwanja wa KMC, kisha mchezo wa pili utapigwa saa 1:00 usiku Azam Complex kati ya Al Wadi ya Sudan na Red Arrows ya Zambia.
Michuano hiyo iliyorejea tena baada ya kusimama tangu mwaka 2021 ilishirikisha klabu 12 zilizokuwa makundi matatu na timu zilizoongoza makundi hayuo, APR, Al Hilal na Al Wadi ziliiungana na Red Arrows iliyomaliza kama mshindwa bora na kuziacha timu nyingine nane zikiaga mashindano zikiwamo za wenyeji.
Licha ya kutokuwepo kwa wenyeji, lakini mechi hizo zinatararajiwa kuwa kali na hasa ile za APR na Al Hilal kwa namna zilizoonyesha soka tamu katika mechi zao za makundi, Wasudan wakiwa ndio pekee walioshinda mechi zote na kuvuna pointi tisa, huku nyota wao, Mohammed Abdelrahman akiongoza kwa ufungaji mabao.
Al Wadi iliongoza Kundi A ikiwa na pointi 7 kama ilivyofanya APR iliyokuwa kinara wa Kundi B, huku Al Hilal ikiongoza Kundi na pointi tisa ikifuatiwa na Red Arrows iliyomaliza na sita katika kundi hilo.
Washindi wa mechi hizo za nusu fainali za leo watavaana katika fainali itakayopigwa Jumapili, huku zitakazopoteza zitaumana katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu ambao pia utapigwa Jumamosi.