Gor Mahia, Al Ahly kazi ipo
Muktasari:
- Mechi hiyo itakayopigwa kuanzia saa 9:00 alasiri kwenye Uwanja wa Taifa wa Nyayo, jijini Nairobi ni kipimo kizuri cha K’Ogalo baada ya awali kuing’oa kwa kishindo Al Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini kwa mabao 5-2. Gor ilianza kwa kupasuka 1-0 ugenini kabla ya kuzindukia nyumbani na kushinda 5-1.
MASHABIKI wa soka nchini sambamba na wale wa ukanda wa Afrika Masharikia kesho watapata burudani ya aina yake ya kuwashuhudia Mabingwa wa Kenya, Gor Mahia watakapokuwa wakitunishiana misuli na watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ya Misri.
Mechi hiyo itakayopigwa kuanzia saa 9:00 alasiri kwenye Uwanja wa Taifa wa Nyayo, jijini Nairobi ni kipimo kizuri cha K’Ogalo baada ya awali kuing’oa kwa kishindo Al Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini kwa mabao 5-2. Gor ilianza kwa kupasuka 1-0 ugenini kabla ya kuzindukia nyumbani na kushinda 5-1.
Al Ahly iliyotwaa taji la 12 la Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuifunga Esperance ya Tunisia katika fainali iliyopigwa Mei mwaka huu, likiwa ni taji la pili mfululizo, kwa msimu huu imepangwa kuanzia raundi ya pili ya michuano hiyo na timu hiyo tayari ilishatua Nairobi tangu juzi tayari kwa mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu.
Kocha wa Gor, Leonardo Neiva alisema licha ya kwanza Al Ahly ni wababe wa soka Afrika na ni moja ya timu kubwa, lakini bado anaamini wana nafasi ya kufanya vizuri nyumbani kabla ya kwenda kurudiana na watetezi hao jijini Cairo, wikiendi ijayo ili kukata tiketi ya makundi.
“Misri ni nchi kubwa kisoka, lakini tutawaonyesha Al Ahly kwamba hata Kenya soka letu limeendelea na haitakuwa rahisi kwao kuchukua pointi hapa, “ alisema Neiva akielezea maandalizi ya mchezo huo.
Hii ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana, lakini Gor Mahia mwaka 2019 ikishiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ilishakutana na timu ya Misri, Zamalek na kila moja kushinda nyumbani, K’Ogalo ikilala ugenini 4-0 kisha kushinda Nairobi kwa mabao 4-2, kuonyesha lolote linaweza kutokea.
Mbali na mechi hiyo ya mapema, leo pia kuna michezo mingine ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ukiwamo ule wa Raja Casablanca ya Morocco itakayokuwa ugenini dhidi ya Samartex ya Ghana, huku Dekadaha ya Somalia itapepetana na mabingwa wa Kombe la Shirikisho msimu uliopita, Zamalek.
Mechi nyingine za leo ni kati ya San Pedro ya Ivory Coast itakayokuwa wenyeji wa Al Hilal ya Sudan, huku Stade Abidjan ya Ivory Coast itaumana na Milo FC ya Guinea.
Pia kwa michuano ya Kombe la Shirikisho ambao Simba itashuka uwanjani kuanzia saa 2:00 usiku dhidi ya Al Ahli Tripoli, jijini Tripoli Libya, mapema saa 11 jioni, Orapa Utd ya Botswana na Dynamos zitaumana.