Gor Mahia yatawala tuzo Ligi Kuu Kenya
Muktasari:
- Timu hiyo ilinyakua tuzo nne katika vipengele tofauti huku kocha wao Jonathan Mckinstry akinyakua tuzo ya kocha bora wa mwaka baada ya kuiongoza K'Ogalo kutwaa ubingwa wake wa 21.
Timu ya Gor Mahia imetawala katika tuzo za Ligi Kuu Kenya (KPL) baada ya wachezaji wake kubeba tuzo muhimu kwenye vipengele tofauti jana usiku katika usiku wa tuzo.
Timu hiyo ilinyakua tuzo nne katika vipengele tofauti huku kocha wao Jonathan Mckinstry akinyakua tuzo ya kocha bora wa mwaka baada ya kuiongoza K'Ogalo kutwaa ubingwa wake wa 21.
Alikiongoza kikosi hicho kwenye michezo 34 huku kikipoteza mechi tatu tu kati ya 34 walizocheza msimu uliopita, na kutwaa Ngao ya Jamii ambayo aliitwa dhidi ya Kakamega Homeboyz katika mechi ya ufunguzi wa msimu.
Tuzo yake ilipokewa kwa niaba yake na meneja wa utendakazi wa Gor Mahia, Jolawi Obondo, huku Mckinstry akikimbilia kwenye majukwaa yake ya mitandao ya kijamii kushukuru shirikisho kwa tuzo kwani kwa sasa amejiunga na timu ya taifa ya Gambia.
Kevin Omondi alitwaa tuzo ya kipa bora baada ya kupata ‘clean sheet’ 22, na kuruhusu idadi ndogo ya mabao kwenye kwenye Ligi Kuu.
Benson Omalla alifanikiwa wakati huu baada ya kushindwa msimu uliopita kwa mabao 2 pekee. Alitwaa tuzo ya kiatu cha dhahabu kwa kufunga mabao 20 kwenye msimu wa 2023/24 huku akifunga mabao 18 Ligi Kuu, moja timu ya taifa na moja kwenye Ngao ya Jamii. Omalla sasa ameifungia Gor Mahia FC mabao 43 katika misimu 2 iliyopita.
Austin Odhiambo almaarufu Austo yeye amebeba tuzo ya mchezaji bora (MVP) akifunga mabao jumla 14. 11 Ligi Kuu, mawili timu ya Taifa, na bao 1 kwenye Ngao ya Jamii huku akiwa na asisti zaidi ya 10 kwenye mashindano yote.
Gor Mahia ilimaliza msimu wa 2023/24 ikiwa bingwa kwa kuvuna pointi 73.