Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

LEBRON, BRONNY: Ni Baba na mwana mwezi ujao NBA

Muktasari:

  • LeBron ameshafanya makubwa NBA tangu 2003 akianzia  Cleveland Cavaliers iliyomchagua kama chaguo namba moja kwenye drafti wakati huo na baadaye akatimkia Miami Heat alikoenda kushinda taji la kwanza NBA. LeBron alibeba taji hilo 2012 akiwa na utatu wa Chris Bosh na Dwyane Wade, kabla ya kurudia tena kulibeba mwaka uliofuata 2013 na baadaye akasepa kurudi upya katika timu iliyomtambulisha NBA, Cleveland Cavaliers.

ACHANA na rekodi kibao alizoweka supastaa wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), LeBron James, tangu aanze kuichezea 2003, lakini miaka 21 baadaye anakaribia kuweka rekodi ambayo haipo kabisa ya kucheza pamoja na mwanaye Bronny James - tena katika timu moja.

LeBron ameshafanya makubwa NBA tangu 2003 akianzia  Cleveland Cavaliers iliyomchagua kama chaguo namba moja kwenye drafti wakati huo na baadaye akatimkia Miami Heat alikoenda kushinda taji la kwanza NBA. LeBron alibeba taji hilo 2012 akiwa na utatu wa Chris Bosh na Dwyane Wade, kabla ya kurudia tena kulibeba mwaka uliofuata 2013 na baadaye akasepa kurudi upya katika timu iliyomtambulisha NBA, Cleveland Cavaliers.

Akiwa Cavaliers, LeBron aliipeleka fainali nne mfululizo za NBA walizocheza dhidi ya Golden State Warriors, ambapo katika fainali hizo moja waliibuka mabingwa wakifanya ‘comeback’ ya kibabe 2016 kutokea 3-1 hadi kushinda 3-4 na kumaliza ukame wa mataji kwa timu hiyo ya Mashariki.

Baada ya kujaribu kwa misimu miwili mbele bila mafanikio, LeBron aliihama Cavaliers akihamia Los Angeles Lakers aliyopo hivi sasa na alimaliza pia ukame wa timu hiyo kutobeba taji tangu mara ya mwisho walipobeba 2010 ikiwa na hayati Kobe Bryant, lakini safari hii akawapa taji akiwa na Anthony Davis 2020.

BRONNY JAMES

Kwa upande wake, Bronny James amechaguliwa na Los Angeles Lakers kama chaguo la raundi ya pili akiwa namba 55 akishtua wengi kwa kuchaguliwa na timu hiyo tofauti na matarajio ya wengi.

Hiyo ni kutokana na kutokuwa na takwimu nzuri kabla ya drafti wakati akiwa chuo, akiandikisha pointi 4.8, ribaundi 2.8 na asisti 2.1 akifunga zaidi ya pointi 10 kwenye mechi tatu huku pointi nyingi zaidi kuwahi kufunga ilikuwa ni 15. Akiwa tayari mchezaji wa Lakers, kipindi cha majira ya kiangazi, Bronny alicheza mechi sita ambapo aliandikisha wastani wa pointi saba, ribaundi 3.5 na asisti 1.5 kabla ya kutisha kiasi kwa kufunga pointi 13 na ribaundi tano.


MCHEZO WA REKODI

KAMA mambo yatakwenda kama ilivyo, Oktoba 22, LeBron na Bronny wataweka rekodi ambayo haijawahi kutokea kabla ya baba na mtoto kucheza timu moja na kufanikiwa kucheza kwenye mchezo mmoja ambao watakuwa nyumbani. Licha ya kwamba Lakers watakuwa na shughuli pevu ya kuwakabili Minnesota Timberwolves inayopewa nafasi kubwa ya kuwa bingwa msimu ujao, taarifa za awali za ndani zinatoa uhakika wa siku hiyo Lakers chini ya kocha Jonathan Clay “JJ” Redick atampa nafasi Bronny kuingia kucheza na LeBron kwenye mchezo huo kama wote watakuwa fiti, na hapo ndipo rekodi mpya itakapowekwa kwa mara ya kwanza NBA.

WAKOSOAJI KAMA KAWA

Wakati hilo likisubiriwa kwa hamu kama litatokea Bronny, 19, atapewa nafasi ya kucheza mchezo akisubiri ile G - League itakayoanza Novemba, wapo wale ambao wanakosoa mpango huo kutokea.

Mashabiki wa NBA na wadau wameonekana kuikosoa timu hiyo kujali zaidi furaha ya LeBron wakiamini ndiyo sababu ya mwanawe kusajiliwa na timu hiyo wakiamini hastahili kuichezea huku pia wakiamini hana hadhi ya kuichezea Lakers wakati huu.

FAIDA NJE YA UWANJA

Wakati wanaoponda kinda huyo kuwa na nafasi ya kucheza mchezo wa ufunguzi wa ligi ndefu (regular season) Oktoba 22, upande wa pili wa hilo ni ukweli kwamba itainufaisha zaidi Lakers kuanzia mauzo ya tiketi na jezi na hata mchezo kutazamwa zaidi kwenye runinga ili kuwaona baba na mwana wakicheza pamoja dhidi ya Minnesota Timberwolves.

Tayari Bronny ameshakuwa na thamani ya aina yake kupitia tu mchezo wa majira ya kiangazi uliopigwa Julai 12, mwaka huu ambapo jezi aliyovaa siku hiyo iliuzwa kwenye mnada kwa Dola 38,400 kutoka thamani ya awali iliyokadiriwa ingekuwa kati ya Dola 6,000 hadi Dola 10,000.

Hii ilimaanisha kwamba, Bronny ndiye alikuwa na mauzo makubwa zaidi kwa wachezaji waliochaguliwa kwenye drafti ya mwaka huu akiwaacha mbali wenzake waliokuwa vinara akiwemo namba moja, Zaccharie Risacher ambaye jezi yake iliuzwa Dola 3,360 na Atlanta Hawks huku Reed Sheppard jezi yake angalau ilifikisha Dola 15,600.