Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vigogo Ulaya waanza kumnyemelea Isak

Muktasari:

  • PSG imekuwa ikijaribu kusuka upya safu yao ya ushambuliaji baada ya kuondokewa na Kylian Mbappe dirisha lililopita. Newcastle inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 83 milioni ili kumuuza Isak.

PARIS Saint-Germain inadaiwa kuwa katika hatua nzuri kwenye mazungumzo na Newcastle United kwa ajili ya kumsajili straika wa timu hiyo na Sweden, Alexander Isak ambaye wanaweza kumsajili dirisha la majira ya kiangazi au baridi mwakani kwa ajili ya kuboresha eneo lao la ushambuliaji.

PSG imekuwa ikijaribu kusuka upya safu yao ya ushambuliaji baada ya kuondokewa na Kylian Mbappe dirisha lililopita. Newcastle inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 83 milioni ili kumuuza Isak.

Katika dirisha lililopita, Arsenal ndiyo ilitajwa zaidi kutaka kumsajili lakini ikashindikana katika dakika za mwisho na inaelezwa Isak mwenyewe ndiye aliyegoma kuondoka.

Mkataba wa staa huyu mwenye asili ya Eritrea, unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 10 za michuano yote na kufunga mabao mawili.


Mason Greenwood

BARCELONA, Atletico Madrid na Bayern Munich zinadaiwa kuwa na uhitaji wa mshambuliaji wa Marseille na England, Mason Greenwood dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Greenwood mwenye umri wa miaka 22, mkataba wake na Marseille unatarajiwa kumalizika 2029 na amezivutia timu nyingi kutokana na kiwango bora alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu.



Axel Disasi

CHELSEA ipo tayari kumuuza au kumtoa kwa mkopo beki wao raia wa Ufaransa Axel Disasi dirisha lijalo la majira ya baridi na baadhi ya timu za England zinadaiwa kuhitaji huduma yake. Disasi amekuwa hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Chelsea hali inayosababisha kocha Enzo Maresca atoe ruhusa hiyo ya kutaka atolewe kwa mkopo mwakani.


Yarek Gasiorowski

REAL Madrid inataka kutoa Euro 45 milioni kwa ajili ya kuvunja mkataba wa beki wa Valencia na Hispania, Yarek Gasiorowski, 19, dirisha lijalo la majira ya baridi.

Yarek ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwakani, tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi mbili za michuano yote.


Lautaro Martinez

CHELSEA imeonyesha nia ya kutaka kumsajili mshambuliaji wa Inter Milan, Lautaro Martinez dirisha lijalo na inataka kuwatumia mastaa wake watatu ambao ni pamoja na Mykhailo Mudryk, 23, Carney Chukwuemeka, 20 na Benoit Badiashile, 23, kama sehemu ya ofa ya kumpata fundi huyo. Mabosi wa Chelsea wanahitaji huduma ya Lautaro kutokana na kiwango bora alichoonyesha kwa zaidi ya misimu mitatu akiwa na Inter.


Dominic Calvert-Lewin

MABOSI wa Everton wanatarajia kumpa ofa ya mwisho straika wao raia wa England, Dominic Calvert-Lewin kwa ajili ya kumsainisha mkataba mpya wakati ule wa sasa ukitarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Lewin mwenye umri wa miaka 27, anawindwa pia na timu nyingi za England tangu dirisha lililopita.


Jonathan David

JUVENTUS inaandaa ofa ya Euro 15 milioni itakayowasilisha Lille kwa ajili ya kumsajili straika wa timu hiyo na Canada, Jonathan David dirisha la majira ya baridi mwakani. David ambaye mkataba wake wa sasa unamalizika dirisha la majira ya kiangazi mwakani, tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi tisa za michuano yote na kufunga mabao matatu.


Kyle Walker-Peters

MAZUNGUMZO ya mkataba mpya baina ya wawakilishi wa  Southampton na beki wao wa pembeni raia wa England, Kyle Walker-Peters yanadaiwa kukwama kutokana na masuala ya masilahi. Inaelezwa Southampton imekuwa katika mazungumzo na wawakilishi wa fundi huyu tangu Agosti mwaka huu, lakini inaelezwa ni ngumu kufikia mwafaka kutokana na mahitaji ya mchezaji huyo.